2018-07-14 16:13:00

Papa Francisko ateuwa Marais wawakilishi wa Sinodi ya Vijana 2018


Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo anataka kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwasikiliza, kuambatana na kuwasindikiza vijana ili kuweza kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazopatikana katika maisha yao. Kanisa linataka kushuhudia imani ya vijana, kusikiliza wasi wasi na mashaka wanayoyafumbatwa katika sakafu ya nyoyo zao! Kanisa linataka kusikiliza hata “mahangaiko” yanayowakera vijana katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo, ili kuboresha sera na mikakati ya utume kwa vijana wa kizazi kipya.  

Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu tayari imekwisha kuchapisha “Hati ya Kutendea Kazi” “Instrumentum Laboris” itakayowasilishwa kwa Mababa wa Sinodi, Mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican. Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inaongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito. Baba Mtakatifu Francisko ameteuwa Marais wawakilishi wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Makardinali wafuatao ndio walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko:

Kardinali Louis Raphaël I SAKO, Patriaki wa Kanisa Katoliki la Wacaldea wa Babeli (Iraq).

Kardinali Désiré TSARAHAZANA, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Toamasina (Madagascar).

Kardinali Charles Maung BO, S.D.B., Askofu mkuu wa Jimbo Katoliki Yangon (Myanmar).

Kardinali John RIBAT, M.S.C., Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Port Moresby (Papua New Guinea).

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.