2018-07-14 17:12:00

Ethiopia na Eritrea katika mchakato wa amani na upatanisho!


Tarehe 8 Julai 2018 katika uwanja wa ndege wa Asmara, mji mkuu wa Eritrea ilitua ndege ya Ndugu Abiy Ahmed, Waziri mkuu wa Ethiopia na Ujumbe alioambatana nao, takribani miaka ishirini ya migogoro kati ya nchi hizo mbili. Wakazi wa mji wa Asmara wakiongozwa na Rais Isaias Afwerki wa Eritrea waliupokea ujumbe huo kutoka Ethiopia kwa shangwe, nderemo na vifijo. Viongozi wakuu wa nchi hizo mbili walikumbatiana kwa moyo wa urafiki na udugu, bila hila wala hiana. Wiki mbili kabla, Abiy Ahmed, Waziri mkuu mpya wa Ethiopia alitoa mwaliko kwa Eritrea kutuma ujumbe Addis Ababa kwa ajili ya mazungumzano ya upatanisho, jambo ambalo liliafikiwa na Rais Isaias Afwerki wa Eritrea.

Habari hii njema ilimgusa hata Baba Mtakatifu Francisko, ambaye katika sala ya Malaika wa Bwana hapo tarehe 1 Julai 2018 akasema kwamba, baada ya mtafaruku wa muda mrefu, mkutano huo kwa nia ya upatanisho, unawasha mwanga wa matumaini makubwa kwa amani na maendeleo ya watu wa Pembe ya Afrika, na Bara zima la Afrika. Mgogoro kati ya nchi hizi mbili ulianza baada ya Eritrea kudai na kupata uhuru wake mnamo mwaka 1998, kutoka chini ya utawala wa Ethiopia, ambapo mipaka ya Eritrea ilikuwa imemezwa kiasi fulani ndani ya Ethiopia tangu mwaka 1962. Kisa kikubwa cha mgogoro huo kilikuwa kupigania mpaka wa ukanda wa Tigray, na hasa mji wa Badme. Kwa upande wa Rais Isaias Afwerki wa Eritrea, alijaribu kuishawishi serikali ya Ethiopia kuachia mji wa Badme ili aweze kukuza uchumi wa Eritrea na hivyo kubaki na mahusiano mazuri na Ethiopia. Kwa upande wa Ethiopia, ikawa ngumu kuachia eneo hilo sababu maafisa wengi wa serikali ya Ethiopia wanatokea eneo hilo la Tigray, ikiwa ni pamoja na aliyekuwa waziri mkuu wa Ethiopia kipindi hicho Ndugu Meles Zenawi.

Kwa kugoma kwa Waziri mkuu Zenawi, kukapelekea Eritrea kutumia nguvu naye Ndugu Meles Zenawi akapata shinikizo la kujibu mashambulizi kwa mtutu kupigania mji wa Bedme. Ndipo vita ikalipuka tangu mwaka 1998 hadi 2000 iliyopelekea takribani watu 80,000 toka pande zote mbili kupoteza maisha. Tume ya Kimataifa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Uhaini, The Hague, iliamua kwamba Eritrea ilifanya makossa kuvamia eneo la Ethiopia. Pamoja na juhudi nyingi za upatanisho, bado nchi hizi mbili hazikufikia muafaka, na hivyo kubaki katika hofu na kutazamana kwa jicho la uadui kwa muda wa miaka ishirini.

Ethiopia imepitia historia na matukio mazito kwa hivi karibuni ambayo bila shaka yamekuwa fundisho na kuwasha hamu ya mtazamo na mabadiliko kwa raia wa nchi hiyo. Baada ya kifo cha ghafla cha Waziri mkuu Meles Zenawi mnamo Agosti 2012, Bwana Hailes Mariam Desalegn alichukua dhamana hiyo ya kuliongoza taifa la Ethiopia. Hata hivyo mnamo mwaka 2016 yakaanza maandamano yaliyoongozwa na kabila la Oromo yakiishinikiza serikali kubadili sera zake na kutoa fursa kwa mgawanyo sawa wa malighafi za nchi ya Ethiopia, ikizingatiwa pia kwamba kabila la Oromo ni lenye idadi kubwa ya watu na wanapatikana katika maeneo mengi nchini humo.

Maandamano haya yakapelekea serikali ya Hailes Mariam Desalegn kuwashambulia waandamanaji na kupelekea vifo vya takribani watu 300. Hali ikaendelea kuwa tete kwa takribani miaka miwili, ambapo ilipofika Februari 2018, Hailes Mariam Desalegn akajiudhuru. Kitendo hiki kikawa kimewanyong’onyesha na kuwavunja nguvu watu wenye asili ya kabila na eneo la Tigray. Baada ya Hailes Mariam Desalegn kubwaga manyanga ili kuruhusu amani itawale nchini humo, ndipo tarehe 2 Aprili 2018, ndugu Abiy Ahmed wa kabila la Oromo, akachukua dhamana ya kuwaongoza watu wa Ethiopia. Tangu Waziri mkuu Abiy Ahmed kuingia madarakani, kawashangaza waethiopia na jumuiya ya Kimataifa kwa juhudi zake kujenga mahusiano mazuri ya kidiplomasia na kukuza uchumi wa nchi hiyo. Kati ya malengo aliyoanza nayo ni pamoja na kurudisha uhusiano mzuri kati ya Ethiopia na Eritrea na kati ya Ethiopia na Misri.

Kwa mahusiano ya kidiplomasia na Eritrea, tarehe 9 Julai 2018, Waziri mkuu Abiy Ahmed pamoja na Rais Isaias Afwerki, wametia mkwaju Tamko la Makubaliano ya kumaliza kinzani kati ya nchi hizo mbili. Makubaliano haya yanapania kuanza kipindi kipya cha urafiki na amani, ambapo watafungua tena Ofisi za Mabalozi katika nchi hizo mbili; safari za ndege na meli zitaruhusiwa tena kwa pande zote mbili; raia wa nchi zote mbili wataruhusiwa kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo; na yataheshimiwa sasa makubaliano ya kimataifa ya mwaka 2002 kuhusu mipaka ya eneo la Tigray. Mambo haya yataruhusu ukuwaji wa mahusiano na maendeleo katika siasa, uchumi, biashara, usafirishaji, mawasiliano, tamaduni na usalama. Abiy Ahmed, Waziri mkuu wa Ethiopia, kamwomba Ndugu Antonio Guterres, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuondoa vikwazo vilivyokuwa vimewekewa nchi ya Eritrea kwa shutuma kwamba mji wa Asmara ulikuwa unafadhili kikundi cha kigaidi cha Somalia, Al Shabaab.

Kwa upande wa mahusiano na Misri, Waziri mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia anapania kurudi mezani na serikali ya Misri ili kukubaliana kugawana matumizi ya maji ya mto Nile. Mnamo mwaka 2011 Ethiopia ilitupilia mbali makubaliano ya kidiplomasia ya nchi zilizoko katika ukanda wa mto Nile, kutumia kwa uwiano stahiki maji yanayotiririka katika mto huo. Ethiopia kwa kukaidi hilo, ilianza kujenga bwawa kubwa, Grand Renaissance Dam, la kuteka maji mengi ya mto huo kwa manufaa yake zaidi. Kwa sasa kuna matumaini ya kurudia makubaliano ya awali. Waziri mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia amekuwa pia na mawasiliano na Saud Arabia, ili kuboresha mahusiano katika sekta za uchumi, biashara, utalii na kushirikiana kupambana na biashara haramu ya binadamu, dawa za kulevya na utumwa mamboleo.

Maaskofu Katoliki nchini Eritrea wametenga muda wa mwezi mzima, kuanzia tarehe 8 Julai hadi 6 Agosti 2018, kwa ajili ya kuombea amani kati ya nchi ya Eritrea na Ethiopia, ili juhudi za viongozi wa serikali hizi mbili ziweze kuzaa matunda mema na yanayo dumu. Novena hii inaoongozwa na tema: Ee mfalme wa amani, Kristo Yesu mtulivu, tujalie amani yako. Hivyo katika parokia zote, nyumba za watawa wa kike na wa kiume, kutakuwa na sala maalumu kila siku kwa ajili ya kuombea amani. Askofu mkuu Abune Menghesteab Tesfamariam wa Asmara katika barua ya maelekezo hayo anasema, ili kufanikisha mchakato wa amani kuna hitajika kila mmoja avae utu wema, haki, msamaha, roho ya kweli ya upatanisho na huruma. Kwa hiyo mbali ya sala hiyo kila siku wakati wa Misa Takatifu, kutakuwa pia na tafakari juu ya amani, haki na upatanisho. Tafakari hizi zitafanyika kila jumamosi na jumapili, kwa kuongozwa na Neno la Mungu pamoja na Hati za Mafundisho ya Kanisa kuhusu amani, haki na upatanisho. Askofu Abune Menghesteab Tesfamariam, kwa niaba ya Maaskofu nchini Eritrea, anawaalika waamini na wote wenye mapenzi mema, kuguswa na ujumbe wa Kristo kwa heri za mlimani anapofundisha: heri wenye kutafuta amani, maana wataitwa wana wa Mungu (Rej. Mathayo 5:9).

Tukio la Waziri mkuu Abiy Ahmed pamoja na Rais Isaias Afwerki, kutia mkwaju Tamko la Makubaliano ya kumaliza kinzani kati ya nchi hizo mbili, limefanyika siku chache kabla ya mkutano mkuu wa 19 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki na Kati, AMECEA; mkutano unaoongozwa na tema Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA. Maaskofu wa AMECEA kupitia mkutano wao mkuu wa 19, wanapenda kutuma ujumbe wa amani kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika eneo la Afrika Mashariki na Kati kwamba, tofauti zilizopo kati yao ni zawadi ya thamani kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kukumbatiwa vema; nao ni uzuri unaotoa fursa ya kujifunza kutoka kwa wengine, kushirikiana, kushikamana na kushirikishana utajiri wa tofauti zilizopo kwa lengo la kufikia amani na utulivu kati ya watu katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Eritrea na Ethiopia ni wanachama wa AMECEA, hivyo makubaliano ya kurejesha urafiki na amani kati ya nchi hizo mbili, yanaashiria wazi kwamba sauti ya kinabii ya mababa wa AMECEA, tayari inatoa mwanga wa matumaini kwa matunda ya malengo ya mkutano wao mkuu wa 19. Hakika Mwenyezi Mungu aibariki Afrika, awabariki na viongozi wake wote wa serikali, vyama na dini; hekima, umoja na amani vitawale, kwani hizi ni nguzo za Bara hili tangu vizazi, kwa wana wa Afrika na wakazi wake wote.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.