2018-07-14 16:28:00

Diplomasia ya Vatican inasimikwa katika haki, amani, utu na heshima!


Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican anasema, Korea kwa sasa inapitia kipindi muhimu sana katika historia na maisha yake, kumbe, huu ni wakati wa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa matumaini na upatanisho wa kitaifa. Huu ni ujumbe ambao umeacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa familia ya Mungu nchini Korea ya Kusini wakati wa safari ya kikazi nchini humo iliyofanywa na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher kwa mwaliko wa viongozi wa serikali kutoka Korea ya Kusini, kuanzia tarehe 4-9 Julai, 2018.

Ziara hii imekuwa ni wakati muafaka wa kuonesha sala na mshikamano wa dhati kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato mzima wa amani, upatanisho na maridhiano yanayoendelea kati ya Korea ya Kusini na Korea ya Kasikazini, kiasi cha kutia matumaini ya amani ya kudumu katika nchi hizi mbili ambazo kwa takribani miaka hamsini zimekuwa zikiangaliana kwa mashaka makubwa. Imekuwa ni nafasi ya kuimarisha pia juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na Kanisa mahalia kwa ajili ya ujenzi wa misingi ya haki, amani na huduma endelevu kwa wananchi wa Korea ya Kusini.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher katika ziara hii, amekazia umuhimu wa ujenzi wa utamaduni wa amani miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kulinda, kujenga na kutetea amani kama kikolezo cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utamaduni wa amani unafumbatwa kwa namna ya pekee katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru wa wana wa Mungu. Askofu mkuu Gallagher amebahatika kutembelea eneo la kijeshi ambalo limebaki kuwa ni alama ya utengano, chuki na uhasama kati ya Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini! Hapa wachunguzi wa mambo wanasema, wananchi wa pande hizi mbili wanapata taabu sana hata kusalimiana tu!

Askofu mkuu Gallagher anasema, umefika wakati kwa sehemu kama hii, kuwa ni eneo la matumaini, umoja na upatanisho wa kitaifa. Akizungumza na wanadiplomasia wanaowakilisha mataifa mbali mbali nchini Korea ya Kusini,  anasema kwamba, amefurahishwa na uhusiano mwema wa kidiplomasia kati ya Vatican na Korea ya Kusini, ambao umedumu kwa takribani miaka 55 si haba! Hii ni changamoto kwa nchi hizi mbili kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani, ushirikiano, maendeleo pamoja na usitishaji wa utengenezaji, usambazaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia kwani ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa.

Askofu mkuu Gallagher katika ziara yake ya kikazi nchini Korea amebahatika kukutana na kuzungumza na Bi Kang Kyung-wha, Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa nchini Korea ya Kusini. Wamegusia masuala mbali mbali ya kitaifa na kikanda; majadiliano yanayoendelea kati ya Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini kama sehemu ya jitihada za ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa. Amepata pia bahati ya kuzungumza na Wabunge Wakatoliki kutoka Korea ya Kusini na hivyo kubadilishana mawazo, mang’amuzi na vipaumbele vya kitaifa na kimataifa. Wabunge wamehamasishwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Korea ya Kusini.

Akizungumzia kuhusu dhana ya diplomasia ya Vatican anasema, Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amekazia kuhusu umuhimu wa diplomasia ya Vatican kufumbatwa katika amani, kwa kusimama kidete kupambana na baa la njaa na umaskini duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote kwani kuna mamilioni ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo endelevu! Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu, ili kuweza kukabiliana na changamoto katika ulimwengu mamboleo.Mataifa yatambue kwamba, yanategemeana na kukamilishana na kwamba, binadamu ni kiumbe jamii. Kwa njia, hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa ni alama ya matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha kutokana na sababu mbali mbali.

Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa kidiplomasia na uhusiano wa mambo ya nchi za nje anakazia kwa namna ya pekee: Mosi, umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Jambo la pili, ni uhamasishaji wa familia ya binadamu kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana, ili kujenga na kuimarisha: haki, umoja na udugu ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Vatican inakazia: ujenzi wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kutatua migogoro ya kivita na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia!

Lengo la tatu la diplomasia ya Vatican ni kukuza na kudumisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani. Katika sehemu hii, Vatican imekuwa ni sauti ya kinabii na hasa zaidi sauti ya watu wasiokuwa na sauti! Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu wote bila ubaguzi. Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata maendeleo ya kweli na endelevu, basi binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu!

Kanisa linapenda kudumisha mchakato wa haki, amani na utulivu, kwa kuzimisha moto wa machafuko, kinzani na vita kwa maji ya baraka, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni mchakato wa majadiliano ya kidiplomasia unaojikita katika kubainisha mbinu mkakati wa mawasiliano, vikwazo na vizingiziti vinavyoweza kujitokeza pamoja na kuunda mazingira ya kuaminiana na kuthaminiana, ili kuendeleza majadiliano. Diplomasia inayotekelezwa na Vatican sehemu mbali mbali za dunia inajikita kwa namna ya pekee, katika msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Ni diplomasia inayojipambanua kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Askofu mkuu Gallagher katika ziara yake ya kikazi nchini Korea amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki chini ya uongozi wa Askofu mkuu Hyginus Kim, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Korea, bila kumsahau Kardinali Andrew Yeom Soon-jung, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Seoul. Katika hotuba yake, amekazia zaidi umuhimu wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayomwilishwa katika huduma makini kwa familia ya Mungu nchini Korea, hususan katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu.

Akiwa nchini Korea, Askofu mkuu Gallagher amepata pia fursa ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa katika baadhi ya majimbo nchini humo hasa katika Madhabahu ya Mashahidi wa Korea. Ametembelea na kusali kwenye kaburi la Kardinali Stefano Kim Sou-hwan, aliyewahi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Seoul. Huyu ni Kardinali wa kwanza kutoka Korea aliyeteuliwa na Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1969. Huyu ni kiongozi wa Kanisa aliyejipambanua katika mchakato wa kutafuta, kutunza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Tarehe 9 Julai 2018, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher akarejea tena mjini Vatican kuendelea na utume wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.