2018-07-13 07:11:00

Ufukara wa Kiinjili uwawajibishe kutangaza na kushuhudia Injili!


Neno utume linaashiria kutumwa. Hivyo katika utume kuna pande mbili: yupo anayetuma na anayetumwa. Yeye anayetuma anamtumia mtu mwingine ambaye anamtegemea kumfikishia vema ujumbe wake. Hivyo atampatia ujumbe huo kikamilifu na kumwezesha kwa nyenzo zote ili kuufikisha ujumbe wake. Anayetumwa anatumika kama chombo cha kuubeba ujumbe anatumwa kuupeleka. Haitarajiwi hata mara moja kwa anayetumwa kuanza kuelezea mambo yake nje na yale anayotumwa, vinginevyo ataisaliti kazi yake. Katika hali ya kawaida mmoja hawezi kujituma mwenyewe; ama atatuma mtu mwingine au atatekeleza mwenyewe na katika hilo la pili hauwi utume. Sisi Wakristo tumetumwa kwenda kutangaza Neno la Mungu. Hili ndilo ambalo Kristo anatutaka na pia kutuwezesha: kutangaza habari njema ya wokovu na kuwafanya mataifa yote, yaani watu wote kumrudia Mungu na kuwa wanafunzi wake.

Utume wa kutangaza habari njema ni mwendelezo wa historia ya wokovu wa mwanadamu. Mwenyezi Mungu anatumia watu mbalimbali tangu zamani za mababu zetu ili kuufikisha ujumbe wake wa wokovu wa wanadamu. Ujumbe huu unawaendea wanadamu ambao wapo katika hali ya dhambi ili waokoke na kumrudia Mungu. “Utume wa Kristo na wa Roho Mtakatifu unakamilika katika Kanisa… utume huu wa pamoja unawahusisha waamini wa Kristo katika ushirika wake pamoja na Baba ndani ya Roho Mtakatifu: Roho hutayarisha watu, akiwaendea kwa neema yake ili kuwapeleka kwa Kristo. Anamdhihirisha kwao Bwana Mfufufka, anawakumbusha neno lake, anafumbua akili zao na kutambua kifo chake na ufufuko wake” (KKK 737). Hivyo tunapokwenda kuitangaza kazi ya Mungu, utume tunaoupokea kama wana kanisa, hatuna budi kuiona nafasi ya Roho Mtakatifu ambaye hututayarisha, hutuandaa, hutudhihirishia Kristo na kufumbua akili zetu.

Katika Injili ya dominika hii tunamwona Kristo anawatuma wafuasi wake. Maudhui ya utume huo yanajionesha wazi: kuutangaza ufalme wa Mungu ambao unafika kwetu kwa njia ya Kristo: kuhubiri toba, kuponya waliopagawa na pepo na kuwapaka mafuta. “Kanisa lasadiki katika uwepo unaohuisha, mganga wa roho na miili. Uwepo huu hutenda kazi kwa namna ya pekee kwa njia ya sakramenti, na kwa namna iliyo ya pekee kabisa kwa njia ya Ekaristi Takatifu, mkate uletao uzima wa milele, na ambao Mt. Paulo hudokeza uhusiano wake na afya ya mwili” (KKK 1509). Kristo anatuambia: “hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele” (Yoh 6:58). Uhai na ufanisi wa utume wetu unafumbatwa katika fumbo la Ekaristi Takatifu ambalo ni ufunuo wa upendo wa Mungu na sababu ya umoja wa kikristo. Utume wetu wa kimisionari unatudai kuiishi Ekaristi Takatifu.

Chemchemi au chanzo cha utume wetu ni upendo wa Utatu Mtakatifu. Kutoka humo ndimo tunachota yale ambayo tunatumwa kwenda kuyatekeleza kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Nje ya chanzo hicho hujikuta tunajitafutia vyanzo vya kidunia ambavyo hutupeleka katika kifo. Kutokana na hilo Kristo anatutaadharisha kutokuandamana na vitu vya kidunia: “msichukue kitu njiani… wala mkate… wala mkoba… wala fedha za kibindoni… msivae kanzu mbili”. Huu ni wito wa “ufukara wa kimisionari” ambao kwa sehemu kubwa leo hii unaathiriwa na upepo wa “biashara za kimisionari”. “Biashara za kimisionari”  ni hatari kubwa inayoiandama jumuiya ya waamini leo hii. Nguvu kubwa inaelekezwa sana katika kujiimarisha kiuchumi hata kama itaua utume halisi wa kutangaza habari njema na kuponya wagonjwa. Hatari hii kwa namna fulani huwa haionekani kwa urahisi na mwishoni tunaishia kuwapora watu fursa ya kuuona uso wa huruma ya Mungu.

Hili linaweza kudhihirishwa na namna ambavyo tunatumia nyenzo mbalimbali za kujipatia ridhiki kama vichaka vya kuwanyonya na kuwakandamiza watu wengine. Mara nyingi tunajidanganya kujitafutia mahitaji msingi na kujikita zaidi katika dhuluma ya utu wa mtu. Sharti la Kristo ni moja: “msichukue kitu njiani”. Hii haimaanishi msile au msijipatie yaliyo muhimu. Katika ukarimu wa asili wa kibinadamu mmoja anapotoa huduma kwa hali ya upendo atapokea huduma muhimu kwa utumishi wake. Ndiyo maana Kristo anawaagiza akisema: “mahali popote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale”. Mmisiaonari anapaswa kujikabidhi katika ukarimu wa wenyeji wake. Ni agizo ambalo lilinuia kuwaepusha mitume kujihangaisha na kutafuta mahitaji ya kijamii kama chakula na malazi.

Na hivyo wito unatolewa kwa yeyote anayempokea mtume wa Mungu ambaye amefika kumtolea huduma kufanya ukarimu kwa kuwapatia mahitaji ya kawaida ya kibinadamu. Si rahisi kwa wananchi kukubali kuona tabibu wao anaishi maisha ya dhiki na njaa kubwa wakati wao wanacho chakula cha kutosha. Katika hali hiyo watampatia chakula kwa sababu kwa upande mwingine nao huitaji huduma yake. Kwa maneno mengine hapa tunaambiwa tuitangulize huduma ya kuustawisha kwanza ufalme wa Mungu na mengine tutapewa kwa ziada (Rej. Lk. 12:22 – 41). Kristo anaongeza kuwa hata kwa wale wasiokuwa na ukarimu jibu lisiwe la vurugu na lawama bali bali kuwaachia ushuhuda wa uchoyo wao katika hali ya amani.

Mwarobaini wa kuepuka “umisionari wa kibiashara” na kuukumbatia “ufukara wa kimisionari” unapatikana katika undugu wa kikristo. Katika mkusanyiko wa viongozi wakubwa wa Wamisionari Wafransiskani Wakapuchini na Maaskofu wote wa jumuiya za kikapuchini uliofanyika huko Assisi mwaka 2017, Mhashamu Askofu Yuda Thadeus Ruwaichi, Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam, Tanzania alitoa ujumbe mzuri kwa vijana, ujumbe ambao unatoa njia ya namna ya kuustawisha undugu wa kikristo kama dawa kupingana na “biashara za kimisionari”. Mhashamu Ruwaichi alisema: “Undugu wa kikristo unajikita katika udogo, kujikatalia, kujitolea katika huduma na nia ya kuwakumbatia watu wote wa Mungu hasa hasa walio fukara zaidi”. Hivyo aliwaasa watu wote hasa vijana “kuwa na uwezo wa kuzitambua sura mbalimbali za ufukara katika jamii ya leo na kuwa ndugu kwa watu wote ambao wana hamu ya kukutana na Kristo”.

Ulimwengu wa leo ambao unajidadavua katika mambo ya mali na vitu vya kuonekana; katika madaraka na sifa za kidunia ni kinzani kwa wito huu wa Mhashamu Ruwaichi na matokeo yake ni kupindisha malengo ya utume tunaopewa na Kristo. Nguvu na ukuu wa mtu umejikita katika uwezo wa kifedha. Mambo haya yanatuadaa na kutufumba macho kiasi cha kutomwona Lazaro anayeteseka chini ya meza yangu ya chakula. Habari tunayoipeleka kwao si habari njema ya wokovu; huduma tunayowapatia si ya uponyaji. Tunageukia upepo wa kidunia wa nipe nikupe; tunakubaliana na msemo wa “mwenye nguvu mpishe”. Tunamwacha kila mmoja ahangaike na hali yake. Katika hali hii kwa hakika tunausaliti utume wetu. Sauti ya Kristo inaendelea kutuonya ikisema: “msichukue kitu njiani”.

Somo la kwanza linatufunulia upinzani wa ulimwengu katika kuupokea ujumbe wa Mungu. Amazia anaizuia sauti ya Mungu na hivyo kuendelea kubariki uovu wa mwanadamu ambao husambaratisha undugu. “Biashara za kimisionari” zinatuzuia kutokuwa tayari kuusikiliza ukweli na kujikinaisha kuwa tunatenda sawasawa. Ung’ang’anizi katika mali unatuondolea haiba ya kumvaa Kristo kama urithi wetu. Mtume Paulo katika somo la pili anatuambia kuwa katika Kristo “Mungu atavijumlisha vitu vyote, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani”. Tunapoupindisha ukweli huu tunaingia katika kishawishi cha kuuchakachua utume tunapewa na kufanya mambo yetu. Tuupokee utume tunaopewa kwa kumweka Kristo kama chanzo na kielelezo chetu na pia ndiye kilele cha utume wetu, yaani kuufanya utume wetu unaoanzia katika Yeye na kuishia katika Yeye.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.