2018-07-13 16:33:00

Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani inayotangazwa na kushuhudiwa!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, kuanzia tarehe 9 -14 Julai 2018 linaadhimisha Kongamano la Kimisionari Amerika ya Kusini linaloongozwa na kauli mbiu “Furaha ya Injili, kiini cha utume wa kinabii, chemchemi ya upatanisho na umoja”. Lengo kuu la kongamano hili ni kuweza kujenga jamii inayosimikwa katika haki, udugu na mshikamano huko Amerika ya Kusini. Maisha ya sala, ushuhuda wa imani katika matendo, umoja na mshikamano wa Kanisa katika maisha na utume wake; majadiliano katika ukweli na uwazi, utamadunisho na uinjilishaji ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kupewa msukumo wa pekee katika maadhimisho ya kongamano hili, sanjari na kusoma alama za nyakati, ili kutambua changamoto mamboleo, tayari kuzivalia njuga kwa mwanga na tunu msingi za Kiinjili.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Askofu Ricardo Ernesto Centellas, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Bolivia kama sehemu ya mchango wake katika maadhimisho haya. Rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni saratani inayopaswa kushughulikiwa bila huruma pamoja na kuondokana na vita, ghasia na machafuko yanayokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayozingatia ari na mwelekeo wa kimisionari ni kati ya mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee, ili kuhakikisha kwamba, vyama vya kitume vinachangia katika ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu huko Amerika ya Kusini.

Waamini watambue kwamba, wao kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanashiriki: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo, kumbe, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa mataifa, lakini zaidi, kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao, waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kielelezo cha imani tendaji. Familia ya Mungu Amerika ya Kusini, inapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha uinjilishaji mpya kwa kusoma alama za nyakati, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo zinazomwandama mwanadamu! Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka ndiye jeuri na matumaini yao, yanayowawezesha kutoka kifua mbele ili kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili. Ushuhuda iwe ni sehemu muhimu sana mchakato wa uinjilishaji mpya.

Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Bolivia ili kujitambulisha na kuangalia changamoto wanazokabiliana nazo kwani ameteuliwa tu hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Amekazia umuhimu wa Kanisa mahalia kushirikiana kwa karibu zaidi na Kanisa la Kiulimwengu, ili kuweza kujibu kilio cha maskini na matamanio halali ya binadamu. Amesema, Mashirika ya Kipapa la Kimisionari yanalenga kuhamasisha mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kumbe Mashirika haya ni muhimu sana katika maisha na utume wa Makanisa mahalia sehemu mbali mbali za dunia.

Makanisa mahalia yaendelea kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari, kwa njia sala, hali na mali, ilikuchangia juhudi za maboresho ya majiundo awali na endelevu ya mihimili ya Injili yaani: wakleri, watawa na makatekista. Kumbe, ni wajibu wa Makanisa mahali kuchangia katika Mfuko wa Mshikamano, kielelezo cha sadaka na majitoleo ya waamini kutoka sehemu mbali mbali za duani na kwamba, hata majimbo maskini kiasi gani yanapaswa kuchangia katika kutunisha mfuko huu. Ni katika Mfuko wa Mshikamano kwamba, majimbo yanaweza kuchapisha vitabu vya liturujia, katekesi na majiundo endelevu ya waamini wake. Msaada unaotolewa na Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari unapaswa kuwafikia walengwa wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.