2018-07-11 16:44:00

Rais Sergio Mattarella awapongeza Makardinali wapya kutoka Italia


Rais Sergio Mattarella wa Italia, Jumatano, tarehe 11 Julai 2018 ameandaa Chai ya Asubuhi kama sehemu ya mapokeo ya kuwakaribisha na kuwapongeza Makardinali wapya kutoka Italia waliotunukiwa heshima na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 28 Juni 2018 katika Mkutano wa Baraza la Makardinali. Makardinali wapya walikuwa wameandamana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Makardinali hawa ni Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu; Kardinali Giuseppe Petrocchi, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Aquila. Tafrija hii, imehudhuriwa pia na Askofu mkuu Emil Paul Tsherrig, Balozi wa Vatican nchini Italia pamoja na Bwana Pietro Sebastian, Balozi wa Italia mjini Vatican.

Hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko, alipokuwa akiwatunukia heshima Makardinali wapya 14 aliwakumbusha kwamba, Kristo Yesu alipokua anatangaza kuhusu Fumbo la Pasaka aliwaambia kwamba, anawatangulia na mtu yoyote anayetaka kuwa mkubwa kati yao, anapaswa kuwa mtumishi wao! Ujumbe huu ni matokeo ya malumbano yaliyojitokeza miongoni mwa Mitume wa Yesu, waliokuwa wanatafuta nafasi za kwanza na upendeleo; wengine wakaelemewa na wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko! Baba Mtakatifu anakaza kusema, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kipaumbele cha kwanza kinatolewa kwa ajili ya utume wa Kanisa!

Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kujikita katika toba na wongofu wa ndani; mabadiliko ya maisha ya kiroho na mageuzi ya Kanisa mintarafu mwanga wa umisionari, ili kuondokana na tamaa ya mambo binafsi, tayari kuanza kuchakarika ili hatimaye, kujikita katika utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha. Toba na wongofu wa ndani, uwasaidie waamini kuondokana na dhambi pamoja na ubinafsi, ili kuambata uaminifu na uwajibikaji, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Changamoto hii ni kubwa hasa nyakati za mateso kwa watoto wa Kanisa, ambao wanapaswa kuwawajibikia, kuwapokea pamoja na kuwasindikiza, bila ya kujitafuta wao wenyewe pamoja na mambo yao! Utume wa Kanisa uwawezeshe viongozi wa Kanisa kuona sura za watoto wa Kanisa wanaoteseka badala ya kujifungia katika tamaa na usalama wa maisha binafsi. Matokeo yake ni chuki, hasira pamoja na kukosa utulivu na amani ya ndani, hali inayopelekea mtu kushindwa kutoa nafasi kwa ajili ya wengine, maisha ya Kikanisa, maskini pamoja na kushindwa kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.