Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Mkutano Mkuu wa 19 wa AMECEA kutimua vumbi Addis Ababa, Ethiopia

AMECEA inaadhimisha Mkutano mkuu wa 19 huko Addis Ababa nchini Ethiopia kwa kukazia hadhi sawa, umoja na amani ndani ya Mwenyezi Mungu kwenye Kanda ya AMECEA. - REUTERS

11/07/2018 08:23

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, watakuwa na Mkutano mkuu wa 19 huko Addis Ababa, Ethiopia, kuanzia tarehe 13 – 23 Julai, 2018, wakiongozwa na tema: Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA. Maaskofu wa AMECEA wamechagua tema hii kuongoza mkutano wao mkuu wa 19, ili kusisitiza ukweli kwamba katika tofauti za tamaduni, mila na desturi za kabila au watu mbalimbali, kuna uzuri wenye thamani kubwa unaopaswa kuenziwa, kuheshimiwa na kushirikishana; na wala isiwe chanzo cha kinzani na migogoro. 

Eneo la AMECEA kwa muda sasa linashuhudia mapigano, ghasia na kinzani katika baadhi ya nchi wanachama kwa vigezo vya tofauti za makabila, tamaduni, mila na desturi.  Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, linajumuisha nchi 9 wanachama rasimi ambazo ni Ethiopia, Eritrea, Kenya, Tanzania, Uganda, Sudan, Sudan ya kusini, Zambia na Malawi. Wakati Djibouti na Somalia ni wanachama washirikishwaji.

Maaskofu wa AMECEA wanapenda kutuma ujumbe wa amani kwa waamini na watu wenye mapenzi mema katika eneo la Afrika Mashariki na Kati kwamba, tofauti zilizopo kati yao ni zawadi ya thamani kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kukumbatiwa vema; nao ni uzuri unaotoa fursa ya kujifunza kutoka kwa wengine. Kumbe Kanisa Katoliki katika eneo hilo, kupitia Mkutano mkuu wa AMECEA linalenga kushirikisha waamini na watu wenye mapenzi mema, kutenda kwa pamoja ili kuifikia amani na utulivu kati ya watu katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Padre Ferdinand Lugonzo, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, akitoa ratiba elekezi ya Mkutano mkuu huo anasema, Misa Takatifu ya ufunguzi rasmi itafanyika tarehe 15 Julai 2018, ambayo itaadhimishwa kwa kufuata madhehebu ya Kanisa la Mashariki, Ethiopia. Maamuzi ya kuadhimisha Misa Takatifu kwa madhehebu ya Kanisa la Mashariki, yamezingatia sababu kuu mbili: kwanza kabisa ni uhalisia kwamba waamini wengi wa Ethiopia ambako ndiko kunafanyika Mkutano huo ni waamini wa madhehebu hayo, hivyo inatoa fursa ya ushiriki wao kwa wingi; na pili ni kushuhudia ule uzuri wa tofauti kiluturjia katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.

Kardinali Berhaneyesus Souraphiel, Mwenyekiti wa AMECEA, ndiye atakayetoa hotuba ya ufunguzi rasmi wa Mkutano huo; naye Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Propaganda Fide, atatoa salamu za kiini cha ujumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu, kwa namna ya pekee AMECEA. Kati ya mada zitakazotolewa ni pamoja na Roho na Utume wa AMECEA, itakayotolewa kwa ushirikiano wa Askofu mkuu mstaafu Telesphore Mpundu, kutoka Lusaka-Zambia, pamoja na Padre Ferdinand Lugonzo, Katibu mkuu wa AMECEA.

Mada juu ya Mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko akiwa Khalifa wa mtume Petro, itatolewa na Kardinali Joseph Tobin, Askofu mkuu wa Newark, Marekani. Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu litakuwa na wawakilishi katika kuongoza warsha yenye tema, AMECEA kuwania maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Dr. Camillus Kassala wa Tanzania, atawasilisha mada juu ya kutetea utu wa mwanadamu katika kutafuta umoja wa kweli. Padre Christopher Sichinga, Mlezi wa chama cha kimataifa cha Vijana Wakristo Wafanyakazi atazungumzia utambulisho na changamoto za vijana; wakati Sr Kayula Lesa, mjumbe wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya kuwalinda watoto atatoa mada juu ya kutetea na kulinda watoto wadogo.  

Mkutano mkuu wa AMECEA huwa na vikao vya aina mbili: Kwanza ni mada na hoja ambapo hushiriki maaskofu, maaskofu wakuu, makardinali na wajumbe kutoka sekreteriet za mabaraza ya maaskofu Afrika Mashariki na Kati. Wengine ni pamoja na uwakilishi kutoka Vatican, Symposium ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu ya Afrika na Madagascar (SECAM), Baraza la Maaskofu Marekani, na wadau wengine wa misaada na waandishi wa habari; Pili ni taarifa kutoka kwa taasisi mbali mbali za AMECEA na uchaguzi wa viongozi wa Umoja na taasisi hizo. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, litawakumbuka pia maaskofu marehemu waliofariki dunia katika kipindi cha miaka minne tangu mkutano mkuu wa mwisho, yaani kati ya 2014 na 2018.

Na Padre Celestine Nyanda.

Vatican News!

 

 

11/07/2018 08:23