Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko kushiriki Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 2019 Panama

Papa Francisko kutembelea Panama kuanzia tarehe 23.27 Januari 2019 ili kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019. - REUTERS

10/07/2018 09:35

Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama, yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 22 – 27 Januari 2019, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kama ulivyonena” Lk. 1:38. Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa na Serikali ya Panama pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini humo la kutembelea Panama kuanzia tarehe 23 Januari 2019 hadi tarehe 27 Januari 2019 ili kuweza kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani. Taarifa hii imethibitishwa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito” ni muda muafaka sana kwa Mama Kanisa kujenga utamaduni na sanaa ya kuwasikiliza vijana, ili kudumisha umoja na mshikamano. Maendeleo makubwa ya mawasiliano ya jamii ni fursa nyingine muhimu sana inayowawezesha waamini kubomoa kuta za umbali ili kuimarisha imani na sala, mambo yanayowaunganisha waamini katika safari na maisha yao ya kiroho. Kwa njia ya imani moja katika sala, waamini wamekuwa ni waasisi wa teknolojia ya digitali hata bila wao kufahamu. Kanisa linapenda kuwashukuru na kuwapongeza viongozi ambao tangu mwanzo wa maisha na utume wao, wamejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume wa vijana, kiasi hata cha kuweza kuwashirikisha vijana hatua kwa hatua katika maandalizi na maadhimisho ya Sinodi ya Vijana.

Bikira Maria, katika ujana wake, alibahatika kushirikishwa na Mwenyezi Mungu mpango wa Ukombozi, kwa kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Hata baada ya kumzaa mwanaye wa pekee, akaendelea kupeta katika “ujana wake” kwa kuwa ni mwanafunzi mahiri wa Mwanaye Kristo Yesu, akaandamana naye kwenye Njia ya Msalaba, hadi akadiriki kusimama chini ya Msalaba, akimwona Mwanaye akiinamisha kichwa na kukata roho! Hata baada ya Kupalizwa mbinguni mwili na roho, Bikira Maria ameendelea kuwa kijana kutokana na utakatifu wa maisha ulioko ndani mwake!

Bikira Maria ni kielelezo na mfano wa ujana uliotukuka na kwamba, upya huu wa maisha unafumbatwa katika Fumbo la Ufufuko. Mtakatifu Gabrieli wa mateso, msimamizi wa wanafunzi alitambua jambo hili katika maisha yake, kiasi hata cha kuonesha upendo na ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu. Mtakatifu Gabrieli aliyekuwa amempoteza mama yake mzazi, aliona kwamba, mbinguni, alibahatika kuwa na mama wawili, kiasi cha kukuza na kudumisha Ibada ya Rozari Takatifu, kiasi kwamba, akiwa na umri wa miaka 18, akawekwa wakfu kwenye Shirika la Mapadre wa Mateso na tangu wakati huo, akajulikana kama Gabrieli wa mateso!

Baba Mtakatifu anaendelea kukazia umuhimu wa utakatifu kama kielelezo makini cha maisha na utume wa Kanisa kinacholiwezesha Kanisa kuwa ni Jumuiya ya waamini wanaopendana hata katika ujana wao. Vijana hawana sababu ya kuogopa kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha, kwani inawezekana kabisa kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na hata kwa Mtakatifu Gabrieli wa mateso, ambao wametangulia ili kuwaonesha dira na mwongozo wa maisha.

Baba Mtakatifu anasema, kamwe hataacha kuwahimiza vijana kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana badala ya kugubikwa na ubinafsi kwa kujenga kuta zinazowatenganisha na kuwagawa watu. Vijana wanahamasishwa kushirikisha upendo kwa kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi ili kudumisha maridhiano kati ya watu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana yanaendelea kushika kasi katika hatua mbali mbali, kwani hivi karibuni, vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliadhimisha utangulizi wa Sinodi na sasa tayari hati ya kutendea kazi imekwisha tolewa na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Kwa sasa inapitiwa na Maaskofu mahalia, tayari kufanyiwa kazi Mwezi Oktoba, 2018.

Huu ni wakati wa vijana kujisemea wenyewe, ili kuibua yale yanayowakera pamoja na mambo yanayowafurahisha ili kuonesha matamanio yao halali katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana ni matumaini na jeuri ya Kanisa. Baba Mtakatifu anawataka vijana kutambua kwamba, wanaweza kukosa na hatimaye, kutenda dhambi, lakini daima wakumbuke kwamba, ukupigao ndio ukufunzao, vijana wajenge utamaduni wa kujifunza kutokana na makosa! Ulimwengu na Kanisa linawahitaji vijana, ili kuweza kulipyaisha na kwamba, utakatifu wa maisha ndiyo siri kuu inayoliwezesha Kanisa kuendelea kupeta katika ujana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

10/07/2018 09:35