Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko asikitishwa na maafa makubwa ya watu na mali zao, Japan

Papa Francisko asikitishwa na maafa makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa pamoja na maporomoko ya udongo. - REUTERS

10/07/2018 10:05

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na taarifa za maafa makubwa yaliyotokea nchini Japan kutokana na mvua kubwa zilizonyeesha nchini humo hivi karibuni na kusababisha watu zaidi ya mia moja kupoteza maisha. Taarifa zinaonesha kwamba zaidi ya watu milioni nne wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mvua kubwa pamoja na maporomoko ya udongo huko Kusini Magharibi mwa Japan. Miji iliyoathirika zaidi ni Hiroshima, Ehime, Okayama na Kyoto!

Baba Mtakatifu katika salam zake za rambi rambi kwa familia ya Mungu nchini Japan zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, anawaombea marehemu wote waweze kupata pumziko na maisha ya uzima wa milele. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuwaponya majeruhi na kuwafariji wale wote walioguswa na maafa haya mazito. Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii pia kuwatia shime wale wote wanaofanya jitihada za kuokoa maisha ya watu na mali zao pamoja na kuwahudumia waathirika.  Wote hawa, Baba Mtakatifu anawapatia baraka zake za kitume!

Wakati huo huo, Waziri mkuu wa Japana Bwana Shinzo Abe amelitaka Baraza la Mawaziri nchini Japan, kuhakikisha kwamba, linaongeza juhudi za kuokoa maisha na mali za watu, kwani kwa sasa hali ya Japan ni tete sana. Hadi sasa taarifa zinaonesha kwamba, kuna watu wengi ambao bado hawajulikani mahali walipo. Inahofiwa kwamba, pengine, watu hawa wamefunikwa na kifusi cha udongo. Zaidi ya wanajeshi 21, 000 wametengwa kwa ajili ya kazi ya uokoaji na wengine zaidi, wanatarajiwa kuongezwa ili kuharakakisha kazi za uokoaji. Mvua hizi zinatarajiwa kuendelea hadi Jumapili, tarehe 15 Julai 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

10/07/2018 10:05