Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Utume wa Bahari: Mateso, changamoto na mchango wa mabaharia na wavuvi

Jumapili ya Utume wa Bahari: Kanisa limewakumbuka na kuwaombea mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao kutokana na changamoto, matatizo na mchango wao katika kukuza uchumi fungamani. - AP

09/07/2018 15:01

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 8 Julai 2018, amekumbusha kwamba, Mama Kanisa alikuwa anaadhimisha Jumapili ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2018, ambao unajielekeza zaidi kwa mabaharia, wavuvi pamoja familia zao. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewakumbuka mabaharia na wavuvi wanaofanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi. Amewapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya utunzaji bora wa bahari dhidi ya uchafuzi wake.

Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika ujumbe wake kwa Jumapili ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2018 amekazia: changamoto wanazokabiliana nazo mabaharia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku; ghasia na uharamia baharini; vyombo na mabaharia kutelekezwa pamoja na uchafuzi wa mazingira baharini. Katika maadhimisho ya Jumapili ya Utume wa Bahari, Mama Kanisa anawakumbuka mabaharia zaidi milioni 1.2 kutoka katika mataifa na dini mbali mbali wanaolazimika kuishi maisha ya shida sana katika vyombo vya usafiri baharini kiasi hata cha kushindwa kusherehekea matukio muhimu katika maisha ya familia zao.

Mabaharia wanachangia usafirishaji wa bidhaa zinazotumika sehemu mbali mbali za dunia kwa asilimia 90%. Mama Kanisa kwa kuthamini huduma na mchango wao, ndio maana ametenga Jumapili ya Utume wa Bahari kwa ajili ya kuwakumbuka, kuwaombea na kuwashukuru kutokana na mchango wao katika ustawi na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu! Pamoja na shukrani zote hizi, lakini mabaharia na wavuvi wanakabiliwa na changamoto zifuatazo:

Mosi, ni mabaharia kunyimwa fursa za kutembelea maeneo yanayozunguka bandari kutokana na madai ya usalama wa meli na bandari, hali ambayo inapaswa kuboreshwa zaidi ili kuondokana pamoja na mambo mengine sera na sheria za kibaguzi zinazotekelezwa na baadhi ya nchi duniani. Mtindo huu wa ubaguzi, wanafanyiwa pia hata wahudumu wa maisha ya kiroho, wanapotaka kutoa huduma ya msaada wa maisha ya kiroho, baada ya kukaa baharini kwa muda mrefu. Mtazamo huu tenge, unapingana kabisa na sheria, kanuni na taratibu za Mkataba wa Kazi wa Mabaharia, ulioanza kutumika kunako mwaka 2013 unaopania pamoja na mambo mengine, kuboresha hali ya maisha ya mabaharia. Kardinali Turkson anakaza kusema, mabaharia pamoja na wahudumu wa maisha ya kiroho, hawapaswi kunyimwa fursa ya kutembelea bandari na kuwahudumia mabaharia.

Pili, ni ghasia na uharamia baharini, ingawa kwa sasa hali inaendelea kuboreka zaidi, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita, kwani uharamia ulisababisha majanga makubwa kwa mabaharia, vyombo na bidhaa walizokuwa wakisafirisha na matokeo yake, waathirika walikuwa ni watumiaji wa bidhaa hizi. Chanzo kikuu cha uharamia sehemu mbali mbali za dunia ni machafuko ya kisiasa yanayogusa na kupekenyua sekta ya uvuvi hali inayochangia uvuvi haramu pamoja na uharibifu wa mazalia ya samaki. Mambo yote haya yanachangia kwa kiasi kikubwa kukua na kuongezeka kwa baa la umaskini duniani, hali ambayo inatumiwa na “wajanja wachache” ambao dhamiri zao zimekufa kuwatumbukiza wavuvi wasiokuwa na ajira rasmi kujiingiza katika mchakato wa uvuvi haramu na uharamia! Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu linaziomba Serikali na wamiliki wa meli kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya ulinzi na usalama wa mabaharia na wavuvi ili kupunguza gharama za kiuchumi.

Tatu, ni vyombo vya usafiri majini pamoja na mabaharia kutelekezwa, tatizo ambalo linaanza kuwa sugu katika sekta ya usafirishaji na uvuvi baharini. Kadiri ya taarifa ya vyombo vya habari inaonesha kwamba, kati ya mwaka 2012 hadi mwaka 2017 zaidi ya mabaharia 1,300 walitelekezwa baharini kutokana na sababu mbali mbali, wakiwa kwenye bandari za kigeni, mbali kabisa na nchi zao wenyewe. Wakati mwingine, mabaharia hawa wamekuwa wakiishi kwa muda wote huo bila ya kupata mshahara wao, chakula wala mafuta ya kuendeshea vyombo hivi.

Kunapotokea hali kama hii, mabaharia na wavuvi wanaachiwa kupambana na hali zao wenyewe, ili kuweza kujipatia chakula; fedha ya kujikimu; nyaraka na vibali vya uhamiaji pamoja na mambo mengine kadhaa, ikiwa kama hawataweza kupata msaada wa mashirika ya kijamii kuwahudumia watu hawa! Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu linapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa wahudumu wa maisha ya kiroho pamoja na watu wa kujitolea, Utume wa bahari kutoka Malta, Afrika ya Kusini, Uingereza na Marekani, wanaoendelea kutoa huduma ya maisha ya kiroho, msaada wa kisheria na huduma ya kisaikolojia kwa mabaharia pamoja na familia zao, pale inapotokea kwamba, wametelekezwa baharini!

Nne, ni uchafuzi wa mazingira baharini, changamoto ambayo imevaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si”, yaani  “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”,  anakazia sana utunzaji bora wa mazingira kuwa ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki, amani na mshikamano, kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya kutunga sheria na sera makini zitakazodhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa angani kwa kuwekeza katika teknolojia na nishati rafiki na mazingira. Kuwepo na udhibiti madhubuti wa uchafuzi wa mazingira na uzalishaji wa hewa ya ukaa.

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu linapenda kuunga mkono sera na mbinu mkakati wa Shirika la Kimataifa la Shughuli za Majini,  IMO, linalopambana na uchafuzi wa mazingira kwa njia ya Plastiki zinazozaliwashwa kutoka kwenye sekta ya usafirishaji baharini pamoja na kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kutoka katika meli sanjari na utekelezaji wa sera na mikakati mbali mbali ya kimataifa kwa ajili ya utunzaji wa mazingira ya bahari. Kardinali Peter Turkson, anahitimisha ujumbe wake kwa Jumapili ya Utume wa Bahari kwa kuomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Nyota ya Bahari, kwa mabaharia na wavuvi wote, ili aweze kuwaepusha na hatari zote, ili hatimaye, awafikishe bandarini salama!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

09/07/2018 15:01