Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Sala ya Malaika wa Bwana

Papa Francisko asema, Siku ya Sala ya Kiekumene imefanikiwa sana!

Papa Francisko awashukuru viongozi wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kwa kushiriki kikamilifu katika Siku ya Sala ya Kiekumene kwa ajili ya Mashariki ya Kati.

09/07/2018 08:52

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 8 Julai 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amerejea tena kwenye Siku ya Sala ya Kiekumene iliyoadhimishwa Jumamosi, tarehe 7 Julai 2018 huko Bari, Kusini mwa Italia kwa kuwakutanisha viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kwa ajili ya tafakari na kuombea amani na umoja huko Mashariki ya Kati. Siku hii imeongozwa na kauli mbiu “Amani ikae nawe: Umoja wa Wakristo kwa ajili ya Mashariki ya Kati”. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuifanikisha Siku ya Sala ya Kiekumene, alama makini ya umoja wa Wakristo na ushiriki wa familia ya Mungu katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo pamoja na wawakilishi wote katika ujumla wao. Anasema, ameimarishwa sana na uwepo pamoja na ushuhuda wao. Anamshukuru Askofu mkuu Francesco Cacucci wa Jimbo kuu la Bari-Bitonto, lililoko Kusini mwa Italia, Mwenyeji wa Siku ya Sala ya Kiekumene, kwa moyo wake wa unyenyekevu na huduma, bila kuwasahau wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kufanikisha siku hii maalum ya sala na tafakari. Baba Mtakatifu anawashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema waliowasindikiza viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kwa njia ya sala, sadaka na uwepo wao wenye furaha!

Wakati wa kufunga Siku ya Sala ya Kiekumene, Baba Mtakatifu Francisko alisema, amani inapaswa kutafutwa kwa udi na uvumba, kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano, ili kudumisha utashi wa majadiliano na sanaa ya kusikilizana kwa dhati! Viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo wanasema, wanataka kutembea, kusali na kufanya kazi kwa pamoja kama kielelezo cha mshikamano wa dhati. Hakuna sababu ya kuogopana kuzungumza katika ukweli na uwazi; kukubali na kuridhia maoni na changamoto kutoka kwa wengine pamoja na kusumbukiana kwa hali na mali, ili kujenga na kudumisha uekumene wa huduma inayosimikwa katika mahitaji msingi, utu na heshima ya binadamu; kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini na amani, ili kilio cha vita kigeuke na kuwa ni wimbo wa amani! Ili kuweza kufanikisha yote haya, kuna haja kwa Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa amani duniani, kwa kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wote! Ni wakati wa kujikita katika ukweli na matumaini badala ya kutafuta kujinufaisha na hali ya kinzani na migawanyiko huko Mashariki ya Kati.

Madonda ya vita huko Mashariki ya Kati yanaendelea kuwaathiri wananchi wa kawaida huko Siria kiasi hata cha kuwatumbukiza katika majanga ya maisha: umaskini, magonjwa na njaa! Vita imekuwa ni sababu ya kuibuka kwa misimamo mikali ya kidini na kiimani, kiasi hata cha kufanya kufuru ya matumizi ya jina la Mungu. Lakini, vita hii, imeendelea kukuzwa kutokana na biashara haramu ya silaha, changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa, lakini zaidi na Nchi tajiri zaidi duniani.

Madhara ya vita ya Hiroshima na Nagasaki, bado hayajaweza kutoa fundisho kwa binadamu kutokana na uchu wa mali na faida kubwa; ni watu wanaotafura malighafi kama vile madini na gesi asili, bila kujali uharibifu wa mazingira nyumba ya wote! Hapa mafao ya kiuchumi ndiyo yanayotawala na wala si utu na heshima ya binadamu. Umefika wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani anasema Baba Mtakatifu Francisko ili kukuza na kudumisha umoja, udugu na maridhiano kati ya watu kwa kuhakikisha kwamba, watu wote wanahakikishiwa haki ya kuendelea kuishi huko Mashariki ya Kati kwa kutambua kwamba, hata Wakristo wanayo haki ya kuishi huko Mashariki ya kati, wakiwa na haki sawa.

Mji wa Yerusalemu ni mji wa kale, mahali patakatifu pa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam, kumbe ni kitovu cha majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani! Mji wa Yerusalemu ni chemchemi ya amani, ustawi na maendeleo endelevu ya familia ya Mungu. Kumbe, unapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote na wala usiwe ni chanzo cha mipasuko ya kisiasa isiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa na hasa amani na matumaini kwa wananchi wanaoishi huko Mashariki ya Kati! Majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya Israeli na Palestina ni muhimu sana ili kupata amani ya kudumu kwa kuwezesha uwepo wa Mataifa mawili yanayojitegemea!

Injili ya Matumaini imeandikwa kwenye nyuso za watoto wadogo huko Mashariki ya kati! Hawa ni watoto wanaolia na kuomboleza kutokana na madhara ya vita, kiasi cha kudhani kwamba, kukimbia nchi yao ndiyo suluhu iliyobaki mbele yao! Vita ni kifo cha matumaini ya watu, kwani badala ya shule, watoto wanashuhudia magofu ya majengo yaliyobomolewa; ni watoto ambao milipuko ya mabomu imekuwa ni sehemu ya maisha yao ya kila siku, lakini, umefika wakati kwa Mashariki ya Kati kuwa ni sanduku la amani, linalowakusanya na kuwahifadhi watu wa dini mbali mbali!

Jua la haki, liangazie giza la Mashariki ya Kati ili kuondokana na uchu wa mali na madaraka; vita na misimamo mikali ya kidini na kiimani; unyonyaji na dhuluma; iwe ni fursa ya kupambana na umaskini, ukosefu wa haki na pamoja na kutambua haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake ya shukrani kwa kusema, amani ikae nawe, haki ikae ndani mwake na baraka za Mwenyezi Mungu ziwashukie watu wote huko Mashariki ya Kati!

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ya ufunguzi wa Siku ya Sala ya Kiekumene amesema, Mwenyezi Mungu ni mwangaza utokao juu na mionzi yake imeujaza ulimwengu kwa imani na hivyo ukawa ni chemchemi ya tasaufi ya imani kwa Mungu mmoja huko Mashariki ya Kati. Ni mwanga unaobeba Ibada za kale na ambazo ni za pekee kabisa; ni mahali penye amana na utajiri mkubwa wa sanaa takatifu, taalimungu na urithi mkubwa wa Mababa wa imani. Mapokeo haya ni utajiri na amana inayopaswa kulindwa na kudumishwa kwa nguvu zote, kwani huko Mashariki ya Kati kuna mizizi ya nyoyo zao.

Lakini eneo la Mashariki ya Kati katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni limegeuka kuwa ni uwanja wa fujo: vita, ghasia na uharibifu mkubwa; uvamizi, chimbuko la misimamo mikali ya kidini na kiimani, uhamiaji wa shuruti pamoja na baadhi ya watu kutelekezwa. Kumekuwepo na kimya kikuu kwa watu wengi na baadhi yao kuhusika moja kwa moja. Mashariki ya Kati limekuwa ni eneo ambalo watu wake wanalikimbia, kiasi cha kutishia uwepo wa imani ya Kikristo katika eneo hili, lakini, ikumbukwe kwamba, bila Wakristo utambulisho wa Mashariki ya Kati unaingia “mchanga”.

Uekumene wa Sala na huduma: Baba Mtakatifu anasema, wameianza Siku ya Sala ya Kiekumene kwa kuwasha taa alama ya umoja wa Kanisa na kwamba, kwa pamoja wanataka kuwasha taa ya matumaini itakayofukuzia mbali giza la usiku katika historia. Lengo ni kuwasha moto wa matumaini kwa mafuta ya sala na upendo. Huu ni mchakato wa sala kwa Mwenyezi Mungu inayomwilishwa katika huduma kwa jirani na huu ndio uekumene wa huduma makini kwa watu wa Mungu, kwa kutafuta: ustawi, maendeleo na mafao yao. Kwa njia hii, moto wa Roho Mtakatifu utaweza kung’ara katika umoja na amani!

Sala ya Umoja: Baba Mtakatifu anaendelea kusema, viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo wanasali ili kumwomba Mwenyezi aweze kuwakirimia amani ambayo viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wameshindwa kuwapatia watu wao. Kilio cha amani kinaendelea kusikika huko Mashariki ya kati. Wanaombea amani kwa mji wa Yerusalemu unaopendwa na Mwenyezi Mungu lakini umeharibiwa na binadamu. Sala ya amani: bado kuna damu ya watu kama Abeli inayomlilia Mwenyezi Mungu na kamwe kilio cha watu hawa hakiwezi kufumbiwa masikio kwa kulalama kuwa wao si  walinzi wa ndugu zao. Kutojali kunaua! Wakristo wanataka kuwa ni sauti inayopingana na mauaji kwa kutojali. Kanisa linataka kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti; watu ambao wamelia sana kiasi kwamba, sasa machozi yamekauka mashavuni mwao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, leo hii Mashariki ya Kati, watu wanalia sana; wanateseka na kukaa kimya, wakati kuna watu wengine wanaoendelea kuwanyanyasa na kuwadhulumu haki zao msingi, kutokana na uchu wa mali na madaraka! Kwa watu wadogo na waliojeruhiwa; watu wa kawaida, ambao kimsingi ni watu wa Mungu; hao ndio wanao ombewa amani, faraja, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kuganga na kuponya majeraha na hatimaye, aweze kusikiliza sala na dua zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

09/07/2018 08:52