2018-07-09 15:48:00

Kongamano la Kimisionari Amerika ya Kusini laanza kuwasha moto Bolivia


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, kuanzia tarehe 9 -14 Julai 2018 linaadhimisha Kongamano VI la Kimisionari Amerika ya Kusini linaloongozwa na kauli mbiu “Furaha ya Injili, kiini cha utume wa kinabii, chemchemi ya upatanisho na umoja”. Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko anawakilishwa na Kardinali Ferdinando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilsihaji wa watu.

Baba Mtakatifu Francisko katika barua ya uteuzi aliyomwandikia Kardinali Filoni anakumbusha kwamba, hili ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ndiyo maana, Baba Mtakatifu anapenda kuwapatia baraka zake za kitume wale wote wanaoshiriki kwa namna mbali mbali. Hii ni dhamana inayolenga kupyaisha dhamana ya kimisionari kwa furaha, imani na matumaini kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani wenye mvuto na mashiko.

Kanisa limeanzishwa na kutumwa ili kuinjilisha, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Lengo la Kongamano ni kuimarisha utume na maisha ya Kanisa la Amerika ya Kusini; Utambulisho na dhamana yao katika mchakato mzima wa uinjilishaji hasa pembezoni mwa mambo msingi ya maisha; kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, mshikamano na udugu. Tema kuu zinazofanyiwa kazi kwa wakati huu ni Injili ya Kristo, Furaha; Utume, Unabii, Upatanisho, Umoja na Uinjilishaji wa awali.

Askofu mkuu Sergio Gualberi wa Jimbo kuu la Santa Cruz, katika ujumbe wake, amewakaribisha wajumbe 2, 500 kutoka sehemu mbali mbali za Amerika ya Kusini, ili waweze kujisikia kuwa kweli wako nyumbani! Familia ya Mungu Jimboni, huko imeamua kutoa malazi kwa wajumbe hawa katika familia zao kama kielelezo cha mshikamano na furaha ya kutangaza na kushudia Injili ya Kristo katika upendo na ukarimu kwa njia ya vitendo! Familia ya Mungu Amerika ya Kusini, inataka kufanya hija ya furaha inayojikita katika ujasiri unaopania kupyaisha ari, moyo na dhamana yao ya kimisionari, ili kweli waweze kuwa vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, tayari kutangaza na kuishuhudia kati ya watu wa Mataifa. Jumapili, tarehe 8 Julai 2018, Makanisa Amerika ya Kusini yamesali kwa ajili ya kuombea ufanisi wa Kongamano la VI la Kimisionari Amerika ya Kusini.

Kongamano la Kwanza la Kimisionari Amerika ya Kusini, COMLA1 liliadhimishwa huko Mexico kunako mwaka 1977: Mababa wa Kanisa wakaamua kuanzisha Mfuko wa Amerika ya Kusini kwa ajili ya kuhamasisha shughuli na mikakati ya kimisionari. Viongozi wakajizatiti zaidi katika kukuza na kudumisha miito mbali mbali ndani ya Kanisa, yaani miito ya: Kipadre, kitawa na maisha ya ndoa pamoja na kuanzishwa kwa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kwa kila Parokia.

Kongamano la Pili la Kimisionari Amerika ya Kusini COMLA 2, liliadhimishwa huko Mexico kunako mwaka 1983. Mkazo ukawekwa katika mchakato wa kuwaenzi Mapadre Zawadi ya Imani, “Fidei donum” kama kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kikanisa sanjari na ushiriki mkamilifu katika mchakato mzima wa Uinjilishaji na ushuhuda wa maisha katika uhalia wenyewe. Huu ukawa ni mwanzo wa Mapdre zawadi ya Imani kutoka Amerika ya Kusini na kwenda kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo sehemu mbali mbali za dunia.

Kongamano la Tatu la Kimisionari Amerika ya Kusini, COMLA 3 liliadhimishwa huko mjini Bogota, nchini Colombia kunako mwaka  1987, kwa kujikita katika changamoto ya kuinjilisha na kuendelea kuwa ni Bara ambalo ni chemchemi ya matumaini ya kimisionari, licha ya umaskini na changamoto mbali mbali zilizokuwepo huko Amerika ya Kusini. Hapa waamini walei, wakapewa dhamana na wajibu wa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama kielelezo makini cha kuyatakatifuza malimwengu. Kongamano la Nne la Kimisionari Amerika ya Kusini, COMLA 4 liliadhimishwa mjini Lima, huko Perù kwa kujikita zaidi katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake, kati ya watu wa Mataifa. Tangu wakati huo, Amerika ya Kusini, ikawa mstari wa mbele kutuma waamini walei sehemu mbali mbali za dunia ili kusaidia juhudi za uinjilishaji.

Kongamano la 5 la Kimisionari Amerika ya Kusini, COMLA 5, liliadhimishwa huko Brasile nchini Brazil, kwa kujielekeza zaidi katika utamadunisho, ili kweli Injili ya Kristo iweze kuwa ni chemchemi ya maisha mapya na matumaini, licha ya changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza huko Amerika ya Kusini. Kumbe, utamadunisho, uinjilishaji na ushuhuda vikapewa upendeleo wa pekee katika sera na mikakati ya uinjilishaji Amerika ya Kusini, daima maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza. Familia ya Mungu, Amerika ya Kusini ikapewa wajibu wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwa wale wasiomjua bado. Waamini pamoja na mambo mengine, wakatakiwa kuwa ni mashuhuda wa huruma, upendo na ukarimu wa Mungu kwa waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.