2018-07-09 08:32:00

Kashfa ya Fumbo la Umwilisho, sababu ya Yesu kukataliwa nyumbani kwao


Sehemu ya Injili ya Marko, Jumapili XIV ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa inamwonesha Kristo Yesu akirejea mjini Nazareti na kuanza kufundisha kwenye Sinagogi, Siku ya Sabato! Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa Yesu kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyumbani kwake, kwani hapo awali alitangaza Injili kuzunguka viunga vya Nazareti! Aliporejea, watu wengi wakapata hamu ya kumsikiliza kwa makini kutokana na umaarufu wake uliojitokeza katika mji wa Galaliya na viunga vyake! Walisikia sifa kwamba, alikuwa ni Mwalimu mwenye hekima isiyokuwa na kifani, alikuwa na nguvu za kuponya magonjwa ya watu! Matukio haya ambayo yangeonekana kumpatia umaarufu Yesu nyumbani kwake, yakageuka kuwa ni kikwazo, mashaka na mshangao mkubwa, kiasi hata cha watu wa nyumbani mwake kumkataa!

Na hapa Yesu hakutenda miujiza bali aliwawekea mikono wagonjwa wachache, akawaponya. Mwinjili Marko anadadavua siku hii kwa umakini mkubwa kwa kusema kwamba, kwanza wananchi wa Nazareti walimsikiliza Yesu kwa makini, wakashangaa na mwishoni wakakwazika kwa kumtambua kwamba, alikuwa ni Mtoto wa Seremala, Mwana wa Maria waliomwona akiishi na kukulia katika mazingira yao! Lakini Yesu, anahitimisha matukio yote haya kwa kusema “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika nchi yake, kwa jamaa zake na nyumbani mwake”. Huu ni msemo ambao umesheheni hekima na busara!

Jambo la msingi hapa kujiuliza ni kwanini watu wa Nazareti wanapigwa na mshangao kwa matendo makuu yaliyofanywa na Yesu, lakini baadaye, wanageuka kuwa na mashaka na hatimaye, kutomwamini na kumkataa katu katu? Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 8 Julai 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wananchi wa Nazareti wanalinganisha unyenyekevu wake na uwezo wa kutenda mambo makuu kwa wakati huu; wanamwona kuwa ni Mtoto wa Seremala, hana elimu kubwa lakini cha kushangaza ni kwamba, alikuwa anahubiri zaidi na kutenda miujiza kuliko hata Makuhani wakuu na waalimu wa sheria! Lakini, badala ya kujiweka wazi ili kufaidika na matendo makuu ya Mungu katika maisha yao, wakakwazika, kwa kuona kwamba, Mwenyezi Mungu ni mkuu kiasi kwamba, hawezi hata kidogo kujinyenyekesha na kujitwalia hali ya ubinadamu!

Hii ndiyo Kashafa ya Fumbo la Umwilisho: Mwenyezi Mungu amejitwalia hali ya binadamu na kuwa sawa na binadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi! Kristo Yesu anafanya mageuzi makubwa katika fikira za watu na Mitume wake, Yeye ambaye ni Bwana na Mwalimu akathubutu kuwaosha Mitume wake miguu yao, kielelezo cha huduma ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Kashfa ya Fumbo la Umwilisho bado inaendelea hata kwa watu wa nyakati hizi anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa masikitiko makubwa! Hii ni changamoto endelevu inayotolewa na Kristo Yesu kwa wafuasi wake wa nyakati zote kufanya mang’amuzi katika ngazi ya mtu binafsi na Jumuiya katika ujumla wake, ili kuondokana na maamuzi mbele yanayowanyima fursa ya kuuangalia ukweli kwa macho makavu, bila kupepesa pepesa macho!

Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu anawaalika waja wake kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini na katika hali ya unyenyekevu, kwani, mara nyingi sana, neema ya Mungu inajitokeza katika hali ya kushangaza, kiasi hata cha kwenda kinyume kabisa na matarajio ya kibinadamu. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Mama Theresa wa Calcutta, aliyekuwa mfupi kwa kimo, lakini kwa njia ya sala na huduma makini kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii amefanya mageuzi makubwa katika huduma ya upendo ndani ya Kanisa, kiasi kwamba, ameacha amana na urithi wa kudumu katika akili na nyoyo za watu wa nyakati hizi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu hawezi kufungwa na vipimo vya maamuzi mbele, kumbe kuna haja ya kujibidisha ili kufungua akili na nyoyo ili kupokea ukweli wa Kimungu unaowajia waamini. Hapa jambo la msingi ni kuwa na imani, kwani ukosefu na utepetevu wa imani ni kikwazo cha neema ya Mungu. Kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu, Wakristo wengi wanaishi kana kwamba, Kristo hana tena nafasi katika maisha yao; ni watu wanaofikiri na kutenda kwa mazoea katika masuala ya imani; wala hawajibidishi kujishikamanisha na Kristo Yesu pamoja na Injili yake. Kila Mkristo anahamasishwa na kuwajibishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba anatangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, ili kwa maombezi ya Bikira Maria, awasaidie kuondokana na mioyo ya mawe na shingo ngumu pamoja na masikitiko ya kiakili, ili kuwa wazi kwa neema, ukweli na utume wa kutekeleza wema na huruma kwa watu wote, bila mtu awaye yote kutengwa na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.