Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Dhamana na wajibu wa Maaskofu Jimbo katika kesi za ndoa

Papa Francisko anapenda kukazia umuhimu wa ushuhuda wa Injili ya familia katika maisha na utume wa Kanisa na kuwataka viongozi wa Kanisa kuwa karibu zaidi na waamini wao ili kuwasaidia katika safari ya maisha ya ndoa na familia.

08/07/2018 11:15

Mnamo mwezi Agosti 2015, Baba Mtakatifu Francisko alitoa Barua binafsi, motu proprio, Mitis iudex Dominus Iesus, yaani Bwana Yesu Hakimu Mwema na mwenye Haki (Pia Mitis et misericors Iesus kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki) kwa ajili ya mabadiliko ya sheria taratibu za uendeshaji wa kesi za ndoa katika mahakama za Kanisa. Lengo la Baba Mtakatifu ni kuhakikisha kwamba Mama Kanisa anakuwa karibu na watoto wake wenye changamoto kubwa za ndoa, ili kuwagusa na kuwahudumia kwa ukarimu na huruma.

Katika Barua hiyo, Mitis iudex Dominus Iesus, Baba Mtakatifu habadirishi Mafundisho Tanzu ya Kanisa ili kuruhusu watu kupeana talaka, kwani fundisho juu ya ndoa moja na isiyotenguliwa bado lipo pale pale, na utoaji talaka ni kufuru kwa mwamini mkatoliki. Hata hivyo, hapo awali, sheria taratibu za Kanisa kuhusu kesi za ndoa, zilipelekea kesi kushughulikiwa kwa muda mrefu na kwa gharama ambazo mara nyingi zilikuwa mzigo kwa walengwa, huku wakibaki muda mrefu katika hali ya sintofahamu juu ya hatima ya mashauri ya ndoa zao kisheria. Katika kupunguza mahangaiko hayo, barua hiyo Mitis iudex Dominus Iesus: inamuelekeza Askofu jimbo kutazama namna ya kupunguza gharama za uendeshaji kesi; inafuta ule utaratibu wa thibitisho la pili la hukumu, hivyo hukumu ya kwanza inatosha iwapo hakutakuwa na rufaa; na inamuweka Askofu jimbo kuwa hakimu mwenyewe kuamua kesi za ndoa zenye kuashiria ubatili ulio wazi.  

Tangu kutolewa utaratibu huo mpya wa mabadiliko ya uendeshaji wa kesi za ndoa katika mahakama za Kanisa, kumekuwa na hoja kwanza kabisa juu ya uwezo wa kila Askofu jimbo wa ufahamu wa sheria na taratibu za uendeshaji na uamuzi wa kesi za ndoa; na pili kumekuwa na mashaka juu ya hatari ya kuweka matatani fundisho juu ya thamani na hadhi ya ndoa na familia kadri ya mipango na mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Kama tulivyofafanua awali juu ya fundisho la ndoa moja isiyotenguliwa linabaki na kusimamiwa na Mama Kanisa katika ubora wake. Sasa tutadadavua ule uwezo wa Askofu jimbo kufahamu na kushughulikia kesi za ndoa yeye binafsi.

Sheria ya Kanisa nambari 378 §1, 5° kuhusu wasifu kielimu wa anayestahili kuteuliwa kuwa Askofu, inamhitaji awe na shahada ya uzamili au uhimili kwenye Maandiko Matakatifu au Taalimungu au Sheria za Kanisa kutoka katika Chuo kikuu cha Kanisa au Taasisi za elimu ya juu za Kanisa, ama walau awe na ufahamu wa kutosha juu ya masomo hayo. Kwa sababu hiyo, kila Askofu anatarajiwa, pamoja na Neema ya kuwekwa wakfu kuwa Askofu, awe walau na ufahamu wa kutosha wa Maandiko Matakatifu, Taalimungu na Sheria za Kanisa, ambavyo vinamuwezesha kuendesha kesi za ndoa katika Kanisa, hata zile zenye mchakato mfupi zaidi.

Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, hapo tarehe 29 Aprili 2018 limetoa Mwongozo kwa vitivo na taasisi za Sheria za kikanisa ili kuweka mafunzo maalum kuwaelimisha maparoko, Baraza la ushauri la ndoa kijimbo, na mawakili waweze kupata ufahamu wa kutosha juu ya mabadiliko yaliyofanywa kwenye uendeshaji wa kesi za ndoa katika mahakama za Kanisa. Mwongozo huo ulimuelekeza Askofu jimbo kusimamia mwenyewe nafasi ya Hakimu mmoja kwenye kesi fupi zenye ushahidi wa wazi, bila kukabidhi moja kwa moja jukumu hili kwenye ofisi za mahakama ya ndoa kijimbo; jambo ambalo lilileta mkanganyo kiasi fulani juu ya uendeshaji wa kesi za ndoa majimboni. 

Kwa sasa, Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki limerekebisha pia kipengele kinachohusu nafasi na wajibu wa Askofu jimbo akiwa hakimu wa kesi za ndoa. Kardinali Giuseppe Versaldi ameeleza kwamba, aliomba rukhsa kutoka kwa Baba Mtakatifu kufanya marekebisho hayo, na alipatiwa rukhsa hiyo kwenye kikao alichofanya naye mnamo tarehe 5 Juni 2018. Marekebisho hayo yanalenga kutoa nafasi kwa Askofu kukabidhi au kushirikisha wataalam wa sheria za Kanisa jimboni ama kutoka majimbo jirani, ili uendeshaji wa kesi uwe wa kitaalam zaidi na uhakika, ikiwa ni pamoja na kuepuka hatari ya kufanya maamuzi kinyume cha taratibu ama Mafundisho Tanzu ya Kanisa.

Kwa sababu hiyo, Askofu jimbo anabaki kuwa ni Hakimu wa kwanza ndani ya jimbo lake, lakini kwa hekima na busara yake, atatumia waandamizi wenye utaalam wa kutosha katika sheria za Kanisa, ili kuhakikisha lengo la wokovu wa roho za watu linafikiwa, katika roho ya haki, kweli, huruma na ukarimu. Mwongozo wa mafunzo juu ya mchakato wa uendeshaji kesi za ndoa ndani ya Kanisa, unawaalika kwanza kabisa maaskofu wahakikishe maparoko, wajumbe wa Baraza la ushauri la ndoa kijimbo, pamoja na mawakili katika mahakama ya ndoa kijimbo ama kikanda, wanaandaliwa vema kufahamu mabadiliko haya na kuyatilia maanani katika utendaji wao. Kardinali Giuseppe Versaldi, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki anafafanua kwamba, Baraza limependelea mafunzo hayo yawafikie pia maparoko kwa sababu wao ndio wachungaji makasisi walio karibu zaidi na wana ufahamu mkubwa wa taabu na mahangaiko ambayo waamini wao wanayapitia katika ndoa na familia.

Na Padre Celestine Nyanda.

Vatican News!

 

 

 

08/07/2018 11:15