Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Tanzia: Kardinali Jean Louis Tauran, amefariki dunia, 5 Julai 2018

Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidni amefariki dunia tarehe 5 Julai 2018 huko nchini Marekani. - AFP

07/07/2018 16:30

Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, kilichotokea tarehe 5 Julai 2018. Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuungana na familia nzima ya Kardinali Tauran kuomboleza msiba huu mzito uliolikumba Kanisa pamoja na wale wote walioguswa kwa namna mbali mbali na msiba huu. Baba Mtakatifu anapenda kumkabidhi Marehemu Kardinali Tauran kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, kwa mtumishi wake, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Kristo!

Kardinali Tauran alianza utume wake katika diplomasia ya Kanisa, akakabidhiwa nyadhifa mbali mbali kati yake ni ule wadhifa wa kuwa Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Akateuliwa na Papa Mstaafu Benedikto XVI kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini. Hapa akaonesha umahiri wake kwa kuwa ni mshauri aliyesikilizwa na wengi, akajenga imani na matumaini na waamini wa dini ya Kiislam katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini.

Kutokana na moyo wake wa sadaka, majitoleo na huduma kwa Kanisa anasema Baba Mtakatifu Francisko akamteua kuwa Camerlengo wa Kanisa Takatifu Katoliki. Ni kiongozi aliyekuwa na imani thabiti, akalihudumia Kanisa kwa juhudi, maarifa, bidii na weledi wa hali ya juu kabisa, hata dakika ya mwisho, licha ya ugonjwa wake uliokuwa unamsumbua kwa muda mrefu! Sasa vita imekwisha, imani ameilinda, Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kumpokea mtumishi wake katika amani na furaha ya milele. Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa familia ya Kardinali Tauran, Baraza la Makardinali, ndugu, jamaa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema bila kuwasahau waamini wa Jimbo kuu la Bordeaux, nchini Ufaransa na wale wote watakaoshiriki katika maziko ya Kardinali Tauran.

Historia yake kwa ufupi kabisa! Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini na Camerlengo wa Kanisa Katoliki, amefariki dunia, tarehe 5 Julai 2018, akiwa na umri wa miaka 75 huko Connecticut, nchini Marekani, ambako alikwenda kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa Parkinson. Itakumbukwa kwamba, tarehe 13 Marchi 2013 baada ya Makardinali kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro, akamtangaza hadharani Baba Mtakatifu Francisko. Kardinali Jean Louis Tauran alizaliwa kunako tarehe 5 Aprili 1943 huko Bordeaux, nchini Ufaransa.

Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 20 Septemba 1969. Tarehe 1 Machi 1975 akajiunda na Diplomasia ya Vatican na kushika nafasi mbali mbali katika masuala ya kidiplomasia.  Tarehe 6 Januari 1991 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu na Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Mwaka 2003 akateuliwa kuwa Mkutubi mkuu wa Maktaba ya Kanisa Katoliki. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali kunako mwaka 2003. Mwaka 2007 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Tarehe 20 Desemba 2014, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Camerlengo wa Kanisa Katoliki.

Kutokana na kifo cha Kardinali Jean Louis Tauran, Baraza la Makardinali kwa sasa linaundwa na Makardinali 225 kati yao wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa ucahguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni124 na wengine 101 hawana tena haki ya kupiga kura wala kuchaguliwa wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 

 

07/07/2018 16:30