Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Tafakari ya Neno la Mungu: Ujumbe wa Mungu si rahisi sana kupokelewa!

Mwenyezi Mungu anatumia watu, mazingira na historia ili kuweza kufikisha ujumbe wa habari Njema kwa waja wake. - EPA

07/07/2018 07:26

UTANGULIZI: Nabii ni mtu yule aliyeitwa na Mungu na akatumwa kupeleka ujumbe kwa watu ambao Mungu mwenyewe amewakusudia. Nabii ni mdomo wa Mungu. Katika historia ya ukombozi Mungu amewainua manabii na akawatuma kwa watu wake ili kuwarudia katika Agano. Naye Kristo nabii wa Agano Jipya na la milele ameliachia Kanisa utume huo wa kinabii nalo linauendeleza kwa njia ya wote wanaozaliwa kwa maji na Mtakatifu na kwa njia ya wahudumu wa daraja Takatifu. Maandiko Matakatifu katika dominika hii ya 14 ya mwaka B wa Kanisa yanauangazia utume huu wa kinabii katika mpango wa Mungu.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Eze. 2:2-5) linaeleza kutumwa kwa nabii Ezekieli. Mungu anamwita Ezekieli na kumwambia “mwanadamu nakutuma kwa wana wa Israeli...” Katika mazingira ya kawaida, mtu anayetumwa na mkubwa au anayefanywa mjumbe wa kiongozi mkubwa naye anashiriki ukubwa huo. Lakini huyu ambaye Mungu anamtuma anamwita “mwanadamu” au “mwana wa mtu” kumwambia kuwa utume huu anaompa haumwinui juu ya wengine bali anabaki bado kuwa mwanadamu na mwana wa mtu kama wao. Anamjalia roho wake aweze kusimama imara aupokee utume. Kisha Mungu anamwambia “ninakutuma kwa wana wa Israeli, mataifa wanaoasi... hawataki kusikia...” Hawa ni wana wa Israeli ambao tayari Mungu alishawapelekea manabii wengi awali hawakuwasikia na kwa kupuuzia maonyo yao tayari wakapelekwa utumwani. Ni kwa hao hao Mungu anamtuma tena nabii Ezekieli. Tangu mwanzo Mungu anamwonesha Ezekieli kuwa kazi yake sio ndogo na haitakuwa ndogo, ndio maana anapomtuma anamwambia “usiogope”.

 

Somo la pili (2Kor. 12:7-10) mtume Paulo kisha kueleza fadhili nyingi alizojaliwa na Mungu; maono na ufunuo, anaeleza namna ambavyo Mungu amenyenyekesha. Anasema kuwa ili asijivune, alipewa mwiba mwilini, mjumbe wa shetani ili ampige. Hakueleza zaidi mwiba huo ulikuwa ni nini hasa. Huenda ulikuwa ni ugonjwa aliokuwa nao, au ulemavu wa kimwili, au namna yake ya kuongea kwa kigugumizi ambao manabii wa miungu mingine waliokuwapo Korintho walimcheka na kuwa wanamshambulia kwa kebehi na dharau. Paulo anatafsiri yote haya kama ni namna anavyotumia Mungu kuwanyenyekesha watumishi wake. Kuwafanya wasijivune kwa sababu ya utume waliojaliwa na hii yote iwawezeshe kutekeleza utume huo kama anavyokusudia Mungu mwenyewe. Anasema pia kuwa alimsihi sana Bwana amwondolee jambo hilo ila Bwana akamwambia “Neema yangu yakutosha”. Ndiyo kusema Mungu ana namna yake ya kujibu maombi ya mwombaji. Anaweza asiiondoe shida bali akampa mwombaji neema ya kuibeba na kukabiliana na shida yake; anaweza asiiondoe shida ila akampa mwombaji faraja kubwa ya neema yake, faraja ambayo huenda hata wale wasio na shida wasiwe nayo; anaweza akatumia shida hiyo kama namna ya kumfundisha mwombaji kumtegemea zaidi Yeye na kutafuta zaidi neema yake maishani. Mwisho anaeleza “uwezo wangu hutimia katika udhaifu”. Ni wazi udhaifu unaozungumziwa hapa sio ule wa dhambi kwa sababu Mungu haifurahii dhambi japo hamtupi mdhambi. Ni udhaifu wa kutokuwa kuwa na uwezo wa kuyatenda ya kimungu ili daima mkono wake Mungu uonekane katika watumishi anaowachagua na kuwatumia.

 

Injili (Mk. 6:1-6a) Yesu anarudi Nazareti, nyumbani kwake alipokulia na siku ya sabato anaanzakufundisha katika sinagogi. Tofauti na maeneo mengine ambako watu walipomwona hata njia wakamzunguka akaanza kuwafundisha, inaonekana huku kwake walimwona wa kawaida tu ndio maana akasubiri hadi siku ya sabato walipokuja katika sinagogi. Hata siku hiyo walipomsikia akifundisha hawakumwona kama nabii bali walihoji kwa mshangao “amepata wapi huyu haya yote?” wakimwita kwa jina la kazi ya baba yake mlishi seremala na ndugu zake waliowafahamu. Ndipo Yesu akasema “nabii hana heshima katika nchi yake, katika jamaa zake na nyumbani kwake.

 

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, maandiko haya matakatifu yanatuonesha kuwa utume wa unabii ni utume ambao una madai yake. Kwanza kabisa unamdai anayeupokea utume akumbuke daima hali yake kwamba anaitwa na Mungu ilhali yeye mwenyewe akiwa na mapungufu yake kama binadamu. Mapungufu hayo yaweza kuwa ni ya kimwili kama vile udhaifu wa afya ya mwili, yaweza kuwa ni ya kiroho kama vile kusongwa na vishawishi hadi kuanguka dhambini na wakati mwingine kuanguka mara kwa mara au yaweza kuwa ni madhaifu ya kijamii kutokana na jamii yake na ile inayomzunguka. Ndivyo alivyokuwa Mtume Paulo na ndivyo anavyoeleza katika somo la pili. Hivyo anaalikwa kuupokea utume na kujitahidi kuutekeza kwa unyenyekevu mkubwa huku akitumia neema zinazoambatana na utume wake kwa ajili ya kutiisha vilema vyake na kuzidisha mapambano yake binafsi dhidi ya madhaifu aliyonayo.

Ujumbe wa Mungu huwa si ujumbe unaopokeleka kwa urahisi. Historia na hulka ya binadamu imeonesha hayo. Wako manabii wengi tangu enzi la Agano la kale waliofukuzwa, waliofungwa, waliopigwa na hata kuuawa kwa sababu ya kutekeleza utume wao. Hata sasa mjumbe wa Mungu na utume wake kwa ujumla haupokeleki kirahisi, si na watu binafsi, si na taasisi hasa za watawala. Watu wako tayari kukabidhi hatima ya maisha yao kwa mfano kwa mwanasiasa kuliko kwa mjumbe wa Mungu, watakuwa tayari kushiriki katika sherehe na starehe mbalimbali na hata kugharimika sana kwa ajili yake kuliko kusaidia utume wa mjumbe wa Mungu na wengine watakuwa tayari hata kusaliti imani kwa Mungu na kusaliti utume wa wajumbe wake ili kulinda maslahi binafsi. Ujumbe wa Mungu si ujumbe unaopokeleka kwa urahisi. Hii inamdai mjumbe wa Mungu kumkazia macho daima Yeye aliyemtuma; kumtanguliza Yeye mbele na kuweka matumaini yake yote kwake. Neno la Mungu kwa wajumbe wake wote daima ni “usiogope”: ndiyo kusema usiyumbeyumbe, usitetereke kwa maana Mungu aliyekutuma atakuwezesha kukamilisha utume wake.

Kristo Nabii wa Agano jipya na la milele ameunganisha utume wa unabii katika ukuhani wake na katika ufalme wake. Yeye anawashirikisha kazi hizi tatu za unabii, ukuhani na ufalme wote wanaobatizwa na kukiri imani kwake. Kwa namna ya pekee wale wanaopokea daraja takatifu anawawezesha kuzitenda kazi hizi kwa nafsi yake mwenyewe ndani ya kanisa. Tuliombee Kanisa liendelee kuwa ni sura ya kinabii katika ulimwengu wa leo. Tuwaombee wahudumu wa daraja wanaotekeleza utume wa unabii kwa nafsi ya Kristo wajazwe na fadhila ya unyenyekevu na ya ujasiri wa kitume ili wasiyumbe, wasitishwe na wasiogope kutekeleza utume wao wa kinabii na tuwaombee wote wanaoshirikishwa utume wa unabii kwa ubatizo ili wawe ushuhuda katika ulimwengu wa leo.

Padre William Bahitwa.

Vatican News!

07/07/2018 07:26