Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko: Lampedusa: Changamoto ya Wakimbizi na Wahamiaji

Papa Francisko: Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi ishughukiwe kwa njia ya mshikamano unaoongozwa na kanuni auni.

06/07/2018 15:37

Imekwisha gota miaka mitano tangu Baba Mtakatifu Francisko atembelee Kisiwa cha Lampedusa, kilichoko Kusini mwa Italia, tukio ambalo limeacha alama ya kudumu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kama sehemu ya kumbu kumbu hii, Baba Mtakatifu, Ijumaa, tarehe 6 Julai 2018 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kuwaombea wale wote waliofariki dunia wakiwa kwenye safari ya matumaini; kuwakumbuka wakimbizi na wahamiaji katika shida na changamoto wanazokabiliana nazo kwa wakati huu pamoja na kuendelea kuwatia shime wale wanaowahudumia wakimbizi na wahamiaji katika mazingira magumu na tete!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amekazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa kusikiliza kilio cha damu ya maskini na kukijibu kwa dhati kwa njia ya mshikamano na huruma! Katika somo la kwanza, Nabii Amosi anawaonya wafanya biashara wenye jeuri kwamba, wao wanaopenda kuwameza wahitaji na kuwakomesha maskini wa nchi, iko siku watakiona cha mtema kuni, kwani Siku ya Bwana itakuwa ni ya maombolezo! Mwenyezi Mungu ataleta njaa katika nchi, si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana. Baba Mtakatifu anakaza kusema, maneno ya Nabii Amosi bado ni hai hata katika mazingira ya wakati huu, kwani, kuna maskini wanaonyanyaswa, kudhulumiwa na hata kuuwawa kikatili! Hawa ndio wale waathirika wa utamaduni wa kifo unaowagusa hata wakimbizi na wahamiaji, wanaoendelea kubisha hodi katika mataifa yenye ustawi na maendeleo makubwa! Baba Mtakatifu anasema, miaka mitano iliyopita alitembelea Kisiwa cha Lampedusa, ili kusikiliza na kujibu kilio cha damu ya maskini, wakimbizi na wahamiaji!

Majibu ambayo yametolewa hadi wakati huu, hata kama yanafumbatwa katika ukarimu, lakini bado hayatoshelezi, kwani hata leo hii, bado familia ya Mungu inaendelea kuwalilia maelfu ya wakimbizi na wahamiaji wanaokufa maji na utupu wakiwa njiani kutafuta usalama na maisha bora zaidi. Kristo Yesu katika Injili, anatoa mwaliko kwa wale wote wanaoteseka; wanaodhulumiwa na kunyanyaswa, wamwendee naye atawapumzisha! Lakini, Kristo Yesu anatenda kwa njia ya wafuasi wake. Anahitaji macho yao ili kuangalia mahitaji ya jirani zao; anahitaji mikono yao, ili kutoa huduma ya kuokoa maisha na kwamba, anahitaji sauti zao ili kutoa taarifa za ukosefu wa haki msingi za binadamu zinazotelekezwa katika hali ya ukimya na pengine kwa kufanya kazi kwa mazoea. Kristo Yesu anahitaji mioyo ya waamini, ili kuwaonesha upendo wenye huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Hawa ndio wale: maskini, wanaonyanyaswa, wanaotengwa, wanaopuuzwa na hatimaye, kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Katika Injili, Kristo Yesu anawataka Mafarisayo waliokuwa wanalalamika kwa vile alikuwa anakula na watoza ushuru na wenye dhambi kwamba, Mwenyezi Mungu anataka rehema na wala si sadaka!

Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wahitaji kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema. Hiki ni kishawishi kikubwa hata kwa watu wa nyakati hizi, wanaotaka kujifungia katika ubinafsi wao, kwa kisingizio cha usalama wa taifa, ustawi na maendeleo ya wananchi wao lakini kwa kusahau kwamba, hata watu wengine wanazo haki zao msingi; wanahitaji usalama; utu na heshima badala ya kujenga kuta za utengano! Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu na wala si kuta za kuwatenganisha!

Jibu makini la kilio na changamoto kubwa ya wakimbizi na wahamiaji kwa wakati huu, anasema Baba Mtakatifu ni: mshikamano na huruma; kwa kushirikiana na kushikamana katika kutekeleza dhamana na majukumu ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji katika ukweli na uwazi, pamoja na kuangalia njia mbadala zinazoweza kutumika. Sera na mikakati makini inayosimikwa katika haki ile inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma ya binadamu; pamoja na kuwaangalia wahusika wote; ili kuweza kutoa suluhu inayojikita katika usalama, haki msingi za binadamu, utu na heshima ya wote. Sera makini zinaangalia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na mshikamano na nchi jirani, kwani katika ulimwengu wa utandawazi, kuna mwingiliano mkubwa wa watu! Huu ndio mwelekeo ambao una mvuto na mashiko kwa vijana wengi! Mzaburi anasema, “Nimechagua njia ya uaminifu, na kuziweka hukumu zao mbele yangu”. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hiki ni kielelezo cha uaminifu na hukumu ya haki inayopaswa kutekelezwa na wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kujibu changamoto za wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa kujikita katika mshikamano unaoongozwa na kanuni auni; kwa kuangalia rasilimali zilizopo na uwajibikaji mkamilifu! Mwishoni, anamwomba Roho Mtakatifu aweze kuwangazia akili na nyoyo zao ili kuondokana na mashaka yasiokuwa na mvuto wala mashiko, ili hatimaye, aweze kuwageuza kuwa ni mashuhuda na vyombo vya upendo wenye huruma wa Baba wa milele, tayari kujisadaka kwa ajili ya maisha ya jirani zao, kama alivyofanya Kristo Yesu, kwa kila mmoja wao! Kardinali John Ribat, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Port Moresby, Maaskofu pamoja na Padre Fabio Baggio na Padre Michael Czerny wamehudhuria pia kwenye Ibada hii, kwani wao wako mstari wa mbele katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, utume unaotekelezwa na Idara ya Wakimbizi na Wahamiaji katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 

 

06/07/2018 15:37