Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko aguswa na upweke na mahangaiko ya Mapadre wake!

Papa Francisko katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Julai, 2018 anasema kwamba, anaguswa sana upweke pamoja na mahangaiko ya mapadre wake!

05/07/2018 09:14

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Julai 2018 anapenda kuwakumbuka Mapadre ambao katika maisha na utume wao wamekuwa mstari wa mbele katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa pamoja na kutoa huduma makini kwa watu wa Mungu! Lakini, kwa bahati mbaya sana, kuna baadhi ya Mapadre wanaokumbana na upweke hasi, kiasi hata cha kujikatia tamaa ya maisha na utume wa Kipadre! Kuna baadhi yao, waamini wanashindwa kuwaelewa pamoja na kuelemewa na mchoko na msongo wa mawazo! Katika mazingira kama haya, Baba Mtakatifu anasema, Mapadre wanapaswa kukumbuka kwamba, waamini wao wanawapenda sana; wanawathamini na kwamba, wanahitaji sana huduma na uwepo wao! Hivi ndivyo Baba Mtakatifu anavyopenda kuwahakikishia Mapadre wake wanaokumbana na changamoto mbali mbali katika maisha kwamba, wasikate wala kujikatia tamaa. Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu kwa njia ya video unasambazwa na mtandao wa utume wa sala kimataifa.

Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema, anaguswa sana na mchoko pamoja na upweke wa Mapadre na kwamba, hawa ni wahudumu wa Injili ambao hawana mbadala! Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za Kanisa; ni viongozi wa Jumuiya ya waamini waliokabidhiwa kwao, lakini zaidi wanapaswa kuwa ni mwandani wa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anawapongeza Mapadre wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa; wanaoteseka na kuhangaika kutokana na sababu mbali mbali. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwasindikiza Mapadre wao kwa njia sala na majitoleo yao, ili kweli wajisikie kwamba, wanasaidiwa na kufarijika kutokana na urafiki wao wa dhati na Kristo Yesu pamoja na ndugu zao katika Kristo!

Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka wake kwa Mapadre, miaka 50 iliyopita anasema kwamba, anatambua fika: matatizo na changamoto zinazowakabili Wakleri sehemu mbali mbali za dunia, kiasi kwamba, hawaoni tena ile furaha ya maisha na wito wa kipadre, kiasi hata cha kujiachilia na hatimaye, kumezwa na malimwengu. Mapadre wakumbuke kwamba, mageuzi makubwa yanayoendelea kufanyika duniani, hayatawaacha salama, ikiwa kama hawatakuwa imara katika imani, maadili na utu wema! Itakuwa ni vigumu sana kwa watu wasiokuwa na imani, kuelewa ubinadamu na udhaifu wa Mapadre katika maisha na utume wao! Kumbe, hii ni changamoto kwa wakleri kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kufa na kupona kuwa ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake; watu wenye mvuto na mashiko; watu wasiokuwa ni kikwazo cha imani kwa wale wanaowaona na kukutana nao katika safari ya maisha yao!

Katika shida na mahangaiko yao ya ndani, Mapadre, wasipate kishawishi cha hofu kuhusu maisha na wito wao, bali watambue kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Daraja takatifu, wanashiriki Ukuhani wa Kristo! Kumbe, wao kimsingi ni watu wa Mungu na watumishi wa Kristo Yesu na Kanisa lake! Wao wanatenda kwa niaba ya Kristo “Agunt in persona Christi” kwa njia ya Roho Mtakatifu na hivyo wanakuwa ni madaraja kati ya Mungu na binadamu kwa njia ya huduma ya Mafumbo ya Kanisa! Wakleri ni watu wanaoishi si kwa ajili yao binafsi, bali kwa ajili ya jirani zao, lakini zaidi kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Katika changamoto za maisha, kashfa na udhaifu wa kibinadamu unaoshuhudiwa na Wakleri sehemu mbali mbali za dunia, watu wanajiuliza, Je, bado kuna sababu ya kuwa na Mapadre ndani ya Kanisa? Mwenyeheri Paulo VI anadadavua kwa kusema, katika Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake, bado kuna kiu na hitaji kubwa la Mapadre wema, watakatifu na waadilifu; watu watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Kweli za Kiinjili kati ya watu wa Mataifa! Watu wana kiu ya: Imani, matumaini na mapendo; wanataka kuonja huruma na msamaha wa Mungu katika maisha yao! Watu wa Mungu wanataka kuwaona Mapadre wanaojichanganya kwa ajili ya malezi na utume kwa vijana wa kizazi kipya; Wakleri watakaosaidia kufundisha dini, maadili na utu wema shuleni; Mapadre watakaochakarika kila siku kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na wazee!

Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu anakaza kusema Mwenyeheri Paulo VI na kwamba, ulimwengu unalihitaji Kanisa na wala hakuna Kanisa lisilokuwa na wahudumu walioandaliwa vyema, wakawekwa wakfu kama alama ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake na kutumwa kutangaza na kushuhudia uwepo wa Ufalme wa Mungu kati ya watu wa Mataifa. Wao ni vyombo na mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake, lakini wanapaswa kutambua kwamba, wito na maisha yao yamehifadhiwa katika vyombo vya udongo! “Habemus...thesaurum istum in vasis fictibus, ut sublimitas sit virtutis Dei et non ex nobis” (Rej. 2 Kor. 4:7).

Tiba ya magonjwa ya kiroho katika maisha na utume wa Mapadre ni: Sala ya Kanisa ndio msingi wa majadiliano ya maisha ya kiroho kati ya Mapadre na Mwenyezi Mungu, ni nguvu ya maisha ya ndani inayojenga na kuimarisha utashi na dhamiri nyofu. Ni mwaliko wa kukuza na kudumisha usafi kamili kama sadaka na utimilifu wa upendo na huduma kwa Mungu, Kanisa sanjari na mpango wa Mungu wa wokovu kwa ulimwengu. Mapadre wakuze na kudumisha umoja, udugu, upendo na mshikamano katika maisha ya kijumuiya, kwani wanaitwa na kutumwa kama Jumuiya na wala si kama mtu binafsi!

Mapadre ni sehemu ya Jimbo na Kanisa la Kiulimwengu, changamoto na mwaliko wa kuwa na imani kwa Kristo na Kanisa lake. Watambue kwamba, Kanisa linaundwa na wadhambi wanaojibidisha kwa toba na wongofu wa ndani ili kuweza kupyaisha maisha yao! Kanisa linaundwa na watakatifu, wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu na kwa neema ya Mungu leo hii wamekuwa kama walivyo! Mapadre walipende Kanisa katika utakatifu na udhaifu wake; washiriki kikamilifu katika mchakato wa utakatifu, ili kuboresha ile sura ya Kanisa ambalo ni Mchumba wa Kristo!

Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu inayoongozwa na Roho Mtakatifu inayohitaji umoja na ushirikiano wa watoto wake wote! Waamini wote wawe na ujasiri wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kupyaisha maisha yao kwa kukabiliana na changamoto mamboleo kwa mwanga wa Injili. Waendelee kujikita katika mchakato wa mageuzi ya Kiliturujia na kwamba, Kanisa liwe ni chombo makini cha huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa liendelee kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Liwe ni chombo cha amani na maridhiano kati ya watu kwa kujikita katika majadiliano ya kiekumene na kidini; ili kudumisha uhuru wa kidini, nguzo msingi ya haki za binadamu. Mapadre wakuze na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Kristo na Kanisa, ili aweze kuwafariji na kuwategemeza kwa ulinzi na tunza yake ya kimama!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

05/07/2018 09:14