2018-07-05 14:11:00

Kumbu kumbu ya miaka mitatu ya "Laudato si" dira na mwongozo wa maisha


Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki na amani kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato Si” ambao ulizinduliwa rasmi mwezi Mei, 2015. Kichwa cha Waraka huu kinapata chimbuko lake kutoka katika wimbo wa Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa ajili ya viumbe na unaweza kutafsiriwa kuwa ni “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Waraka huu umegawanyika katika sura kuu sita na una mwelekeo wa umoja na mshikamano ambao unadhihirishwa na mchango uliotolewa na Mabaraza mbali mbali ya Maaskofu Katoliki. Baba Mtakatifu anahitimisha Waraka wake kwa sala mbili, moja ni ile ya dini zote na sala ya pili ni ya Kikristo kwa ajili ya kutunza mazingira.

Baba Mtakatifu Francisko anaonekana kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi, kwa kuimba utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia na kwa kukazia umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu, anapembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika katika  usawa, ustawi na mafao ya watu wote duniani.

Kardinali Pietro Parolin, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka mitatu tangu Waraka huu uchapishwe na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 5 Julai 2018 amekazia kwa namna ya pekee kabisa: umuhimu wa kujikita katika ekolojia fungamanishi, kwa kutambua kwamba, binadamu amepewa dhamana ya kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Huu ni Waraka ambao umekuwa na mchango mkubwa sana kwa wanasayansi pamoja na wadau mbali mbali kwani umekuwa kama jukwaa la majadiliano linaloonesha utashi wa kutaka kumwilisha waraka huu katika uhalisia wa maisha ya watu!

Katika hotuba yake elekezi, Kardinali Parolin amejikita zaidi katika ekolojia fungamanishi, inayowataka watu kuishi kwa furaha na katika ukweli, kwa kutambua kwamba, kuna uhusiano wa karibu sana kati ya mazingira, haki kwa maskini, amani na utulivu wa ndani, kiasi kwamba, kilio cha dunia mama ni sawa na kilio cha maskini duniani! Baba Mtakatifu anawachangamotisha walimwengu kushikamana kwa dhati ili kuweza kuzikabili  changamoto hizi kwa umoja, kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo vya Mwenyezi Mungu katika utunzaji wa mazingira. Utunzaji wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya Injili ya mazingira, kielelezo makini cha umoja na mafungamano ya kijamii kati ya binadamu. Mafungamano haya yamejikita katika mambo makuu matatu: Uhusiano na Mwenyezi Mungu; Uhusiano na Jirani na hatimaye, Uhusiano na dunia yenyewe. Mwanadamu amejeruhiwa kwa dhambi ya asili na matokeo yake yanayojionesha ardhini, majini, hewani na katika aina mbali mbali za mifumo ya maisha sanjari na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Changamoto hizi zinahitaji kwa namna ya pekee kabisa mageuzi kuhusu mtazamo wa maendeleo endelevu ya binadamu, uratibu wa shughuli za kiuchumi pamoja na mitindo ya maisha. Mafundisho ya Kanisa kuhusu kazi ya uumbaji yanakazia kwamba, kama ulivyo uumbaji hata maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini kwa bahati mbaya, mwanadamu anaelemewa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kazi ya uumbaji ni hatua ya kwanza katika wito wa mwanadamu yaani: Uumbaji, Umwilisho na Ukombozi.

Hii inaonesha kwamba, Mwenyezi Mungu anakazia ajenda mbili yaani ulimwengu na mwanadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kumbe, kuna haja ya kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye Muumbaji, binadamu anapaswa kushikamana na kufungamana na wengine katika udugu na kwamba, dunia ni makazi ya wote! Mwanadamu anashirikishwa katika kazi ya uumbaji anayopaswa kuiitekeleza kwa ukamilifu. Kumbe, Waraka wa Kitume wa “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni dira na mwongozo wa maisha kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.