2018-07-04 15:40:00

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Ulaya: Utamaduni wa kukutana muhimu


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, linayounganisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki 33, hivi karibuni, limehitimisha mkutano wa Makatibu wakuu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, uliokuwa unafanyika huko Nicosia, nchini Ugiriki, kwenye “visiwa vya kujidai” vya Mtume Paulo na Barnabas. Makatibu wakuu, wamejizatiti kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana ndani ya Kanisa, kwa kuendeleza majadiliano ya kiekumene na kidini na wadau mbali mbali.

Changamoto hii inahitaji kwa namna ya pekee kabisa, fadhila ya upendo, inayowasukuma waamini kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao, daima wakijitahidi kubakiza uhuru na utambulisho wao binafsi. Ni wajibu wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na nchi pamoja na jirani zao, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Kwa njia hii, Kanisa litaendelea kuwa ni shuhuda na chombo cha Injili ya matumaini Barani Ulaya; tayari kutoka kimasomaso kushuhudia Injili ya matumaini; kwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayojikita katika mchakato wa haki na amani duniani!

Monsinyo Duarte da Cunha, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, ambaye baada ya kulitumikia Shirikisho kwa muda wa miaka kumi sasa na ambaye anatarajiwa kuhitimisha muda wake wa uongozi mwezi Septemba 2018, ndiye aliyepembua mada ya juu ya utamaduni wa kukutana! Askofu mkuu Youssef Soueif wa Kanisa la Wamaronite nchini Ugiriki amepembua kuhusu “Chakula cha kiroho kinachohitajika kwa sasa Barani Ulaya”. Baadaye, Makatibu wakuu waligawanyika katika makundi ili kujadili mada hizi pamoja na kusikiliza shuhuda zilizotolewa na wajumbe kutoka Shirikisho la Makanisa ya Ulaya, COMECE Shrika la Misaada ya Kanisa Katoliki Barani Ulaya, Caritas Europe, Haki na Amani! Wajumbe pia wameshirikishana tema mbali mbali kuhusu siasa, tamaduni na mapambano ya umaskini Barani Ulaya, kielelezo cha mshikamano wa pekee katika imani.

Wajumbe wamekiri kwa dhati kwamba, Bara la Ulaya linakabiliana na changamoto changamani na kwamba, hiki ni kipindi mahususi cha kuweza kutembea kwa pamoja, daima wakiongozwa na kauli mbiu kutoka kwa Kristo Yesu anayewaambia wafuasi wake “Msiogope ninyi…Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi, siku zote hata ukamilifu wa dahari”. Umoja na huduma ya upendo ni kati ya mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha pekee kama kielelezo cha ushuhuda katika mchakato mzima wa uinjilishaji na alama ya matumaini inayotolewa na Mama Kanisa Barani Ulaya.

Hii ni changamoto ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, binadamu anapaswa kuwa ni kiini cha maendeleo fungamanishi na endelevu. Wajumbe wanakiri kwamba, amani na utulivu ni vichocheo vikubwa vya maendeleo ya binadamu, kumbe kuna haja ya kujenga na kukuza utamaduni wa kujadiliana na kusikilizana katika ukweli, haki na upendo. Mwishoni, wajumbe walitembelea sehemu mbali mbali za kihistoria nchini Cyrpus na kujionea utajiri, rasilimali na maliasili iliyomo visiwani humo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.