2018-07-03 14:31:00

Uekumene wa damu na sala unaliunganisha Kanisa zaidi!


Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kutoka Mashariki ya Kati, tarehe 7 Julai 2018 wanaungana pamoja katika Siku ya Sala ya Kiekumene kwa ajili ya kuombea amani na umoja huko Mashariki ya Kati. Siku hii inaongozwa na kauli mbiu “Amani ikae nawe: Umoja wa Wakristo kwa ajili ya Mashariki ya Kati”. Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema, wazo la Siku ya Sala ya Kiekumene kwa ajili ya Mashariki ya Kati ni la muda mrefu.

Hii inatokana na ukweli kwamba, Baba Mtakatifu amekuwa na jicho la pekee sana kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati kutokana na mateso, nyanyaso na dhuluma wanazokabiliana nazo, kiasi kwamba, kwa sasa wamekuwa kweli ni mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake! Kardinali Koch anakaza kusema, huu ni ushuhuda wa uekumene wa sala, kielelezo cha mshikamano na Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaoishi na kuteseka huko Mashariki ya Kati!

Kardinali Koch anakaza kusema, kwa miaka ya hivi karibuni amebahatika kutembelea kambi za wakimbizi na wahamiaji nchini Yordan na Ugiriki na kila mahali wameonesha ile kiu ya kutaka kusindikizwa kwa njia ya sala katika shida na mahangaiko yao. Sala ni ushuhuda wa uwepo wa karibu kwa wahanga wa vita, wakimbizi na wahamiaji bila kuwasahau wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali za maisha.

Barua za mwaliko zimeandikwa na Baba Mtakatifu Francisko mwenyewe na kwamba, viongozi wengi wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo wamekubali na kutikia mwaliko huo. Inasikitisha kuona kwamba, kutokana na mateso makali na hali ngumu ya maisha, Wakristo wengi wameamua kuondoka huko Mashariki ya Kati! Lakini ikumbukwe kwamba, bila Wakristo, utambulisho wa Mashariki ya Kati unaingia dosari. Wakuu wa Makanisa wanahimiza mshikamano wa umoja na upendo, utakaowajengea uwezo Wakristo kuendelea kubaki huko Mashariki ya Kati, huku wakipambana na hali zao, kama kielelezo cha ushuhuda!

Hiki ndicho kiini cha uekumene wa damu unaozungumziwa na Baba Mtakatifu Francisko. Damu ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, itaendelea kuwa ni mbegu ya Ukristo na mchakato wa umoja wa Wakristo. Wakristo wote wanateseka na kudhulumiwa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; kumbe, uekumene wa damu una nguvu sana kama kielelezo cha ushuhuda wa imani yenye mvuto na mashiko! Takwimu zinaonesha kwamba, leo hii kuna wafiadini wengi zaidi duniani, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo anasema Kardinali Koch.

Mashuhuda na wafiadini wanaliunganisha Kanisa na kamwe si chanzo cha mpasuko. Hii ni changamoto kwa Wakristo hata katika mazingira tete kama haya, wanapaswa: kusamehe na kusahau, kama sharti muhimu sana la kuweza kupokea huruma, msamaha na upendo wa Mungu katika maisha yao. Kristo Yesu, awe ni mfano wao bora wa kuigwa kwani hata katika mateso makali, bado alithubutu kuwasamehe watesi wake, kwani walikuwa hawajui wanalotenda. Huu ndio ushuhuda uliotolewa pia na Stefano shahidi na mfiadini wa kwanza, wakati akiwa kufani akawasamehe watesi wake.

Kardinali Koch anakaza kusema, Sala ndiyo silaha pekee ambayo Wakristo wanayo kibindoni mwao dhidi ya dhuluma, nyanyaso na vita dhidi ya Wakristo. Sala ina uwezo mkubwa wa kutenda maajabu kama inavyojionesha kwenye Arusi ya Kana, Yesu aliposikiliza kwa dhati kabisa ombi la Bikira Maria kwa wanaharusi. Kwa njia ya sala, waamini wanataka kujiaminisha mbele ya Mungu kwa kumwekea mbele ya macho yake yenye huruma: matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika kukuza na kudumisha Ukristo huko Mashariki ya Kati.

Kardunali Kurt Koch anahitimisha mahojiano maalum na Shirika la Habari la Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, SIR. Kwa kusema kwamba, mshikamano kwa njia ya sala ni muhimu sana, kama ushuhuda wa umoja wa Wakristo katika kupambana na changamoto mamboleo. Ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inafumbatwa katika: ukweli na uwazi; haki, upendo na uhuru. Ushuhuda huu ni muhimu sana katika ngazi ya kimataifa, ili hatimaye, kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani.

Na Padre Richard A, Mjigwa. C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.