2018-07-03 09:06:00

Siku ya Sala ya Kiekumene Bari: Kuombea amani na umoja wa Wakristo!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 7 Julai 2018 atatembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari, ili kusali na kutafakari juu ya mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Hawa ni Wakristo wanaolazimika kuyakimbia makazi na nchi yao kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wakuu wa Makanisa ya Kikristo wamekubali kushiriki katika tukio hili la maisha ya kiroho linaongozwa na kauli mbiu “Amani ikae nawe: Umoja wa Wakristo kwa ajili ya Mashariki ya Kati”.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe Mosi, Julai 2018, amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza viongozi wa Makanisa katika tafakari na sala kwa ajili ya amani, utulivu na umoja huko Mashariki ya Kati, ikizingatiwa kwamba, eneo hili limegeuka kuwa ni uwanja wa vita! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, matukio kama haya yataendelea kuongezeka siku kwa siku, ili kukuza na kudumisha uekumene wa huduma, sala sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa, kama sehemu ya mchakato wa umoja na neema ya Mungu inayowaunganisha!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, anafarijika sana kuona kwamba, wanashirikiana kwa karibu sana na Patriaki Bartolomeo kwa kwanza; kwa kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya maendeleo endelevu yenye umuhimu wa pekee katika maisha ya watu kama: vile mapambano dhidi ya mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; ulinzi na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote; kutafuta, kulinda na kudumisha amani duniani. Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa kukubali kushiriki katika mkutano wa Sala kwa ajili ya kuombea Amani Mashariki ya Kati.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika ujumbe aliomwandikia Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani iliyoadhimishwa tarehe 29 Juni 2018 anasema, anatarajia kushiriki kikamilifu katika Siku ya Tafakari na Kuombea Amani huko Mashariki ya Kati, iliyoandaliwa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 7 Julai 2018, huko Bari, Kusini mwa Italia. Anasema, itakuwa ni Siku maalumu ya kusali na kutafakari kuhusu haki, amani na upatanisho, mambo msingi yanayoonesha utume wa Kanisa hapa duniani. Amani ya kweli inajikita katika: uhuru, haki na mshikamano.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaendelea kufafanua kwamba, walimwengu wanatarajia kuona Makanisa yakiwaongoza kuelekea katika undani wa ukweli huu, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu kwani majadiliano ya kweli yanakuza na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho. Amani ya kweli haiwezi kupatikana kwa njia ya mtutu wa bunduki, bali kwa njia ya upendo usiotafuta mafao yake binafsi. Mafuta ya imani yatumike kuganga na kuponya madonda ya binadamu! Maadhimisho haya yawe ni kikolezo cha hija ya kiekumene kuelekea umoja wa Kanisa!

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Jumamosi, tarehe 7 Julai 2018 baada ya viongozi wakuu wa Makanisa kuwasili mjini Bari na kupokelewa na viongozi wa Kanisa nchini Italia, wote kwa pamoja watasali mbele ya Masalia ya Mtakatifu Nicolaus wa Bari. Baadaye, viongozi wote watapanda Bus kuelekea kwenye Ufukwe wa Bahari kwa ajili ya Sala ya Kiekumene itakayoanza saa 3:30 kwa Saa za Ulaya. Baadaye, watarejea tena kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicolaus wa Bari kwa kikao cha faragha.

Siku ya Kiekumene imetengwa maalum kwa ajili ya kuombea umoja unaopaswa kububujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kukuza na kudumisha umoja na udugu, msingi wa amani ya kudumu. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, limeandaa mkesha wa sala kwa ajili ya Siku ya Kiekumene huko Bari, Kusini mwa Italia.

Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo alisikika akisema, watakatifu na wafiadini ni vielelezo na mifano bora ya kuigwa katika maisha na maombezi yao. Wanaonesha dira na mwongozo wa kufuata katika maisha kama wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa mifano na maombezi yao, wanawasaidia waamini katika mchakato wa kuwa watakatifu, kama kielelezo cha kutangaza na kushuhudia: ukuu, uweza na utakatifu wa Mungu. Kwa kuwaheshimu watakatifu, waamini wanamtukuza na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika utakatifu wake, ambao umemwezesha kuwatembelea na kuwatakatifuza waja wake. Kimsingi, watakatifu ni mng’ao wa utukufu wa Mungu.

Ibada ya kuheshimu masalia ya Mtakatifu Nicolaus wa Bari  yanayohifadhiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicolaus wa Bari, Jimbo kuu la Bari-Bintonto, Italia, inayotekelezwa na Wakristo ambao bado wamegawanyika ni changamoto ya kumwomba asaidie kuganga na kuponya kashfa ya utengano kati ya Wakristo wa Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Kwa waamini wa Makanisa haya mawili kuendelea kuonesha Ibada kwa watakatifu hawa ni kielelezo cha utashi wa watu wa Mungu kutaka kuungana tena ili kukuza na kudumisha umoja, ushuhuda na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Eneo la Mashariki ya Kati na Bahari ya Mediterrania yamegeuka kuwa ni uwanja wa vita, vinavyotokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani; vitendo vya kigaidi, chuki na uhasama; mambo ambayo yanapaswa kurekebishwa kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi; upatanisho, haki na amani! Kuna haja ya kujenga “Tasaufi ya Amani Ukanda wa Mediterrania", ili kuliwezesha Kanisa kushiriki kikamilifu katika mahangaiko na matumaini ya watu waliokata tamaa ya maisha.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuamua kwamba, tarehe 7 Julai 2018 iwe ni Siku ya Kiekumene: ili kusali na kutafakari juu ya mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Hawa ni waamini wanaolazimika kuyakimbia makazi na nchi yao kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kardinali Gualtierro Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, ana matumaini kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika tukio hili, ataweza kuwaonesha dira na mwongozo sahihi wa kufuatwa katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.