2018-07-02 07:21:00

Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu ni shule ya huruma, msamaha na upendo!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, tafakari ya Sadaka ya Kristo Msalabani inawabidisha waamini kujikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na jirani; tayari kujisadaka kwa ajili ya kuwaganga na kuwaponya wale wote wanaoteseka kutokana na kumong’onyoka kwa sheria kanuni maadili; utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine bila kusahau ulaji wa kupindukia; unaopelekea mamilioni ya watu kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Hiki ndicho kiini cha huduma inayotolewa na Mashirika haya ya kitawa na kazi za kitume kwa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Katika maisha na utume kwa Kanisa na Jamii, Wamisionari wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume katika ushuhuda na kazi zao za kitume anasema Baba Mtakatifu, hawana budi kujikita katika mambo makuu yafuatayo: Ujasiri wa ukweli; Jicho la upendeleo kwa wote, lakini zaidi maskini; mvuto wenye mashiko na uwezo wa kuwasiliana na wengine.

Mwezi Julai ni mwezi ambao Kanisa limeutenga kwa namna ya pekee kama mwezi wa Damu Takatifu ya Yesu. Mwezi huu unaanza kwa adhimisho la Sherehe ya Damu Takatifu ya Yesu siku ya tarehe Mosi, Julai. Sherehe hii imetokana na ombi maalum aliloliwasilisha Mtakatifu Gaspari kwa uongozi wa Kanisa mwaka 1822 ili kuweza kusherehekea sikukuu ya Damu Takatifu mbali na ile sherehe katika kalenda ya Kanisa ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristu. Ilitolewa ruhusa ya kusherehekea sikukuu hiyo siku ya Jumapili ya kwanza ya mwezi Julai lakini ndani ya shirika la Damu Takatifu pekee. Baadaye Baba Mtakatifu Pio wa Tisa akaipangia Sikukuu hiyo tarehe Mosi, Julai ya kila mwaka. Baba Mtakatifu Pio wa Kumi na moja akaikweza kuwa sherehe kwa Kanisa zima mwaka 1934 wakati wa kumbukumbu ya kuadhimisha Karne ya Kumi na Tisa ya Ukombozi.

Mwezi wa Damu Takatifu una uhusiano wa moja kwa moja na mwezi Juni ambao Kanisa limeutenga kwa ajili ya tafakari na ibada ya kuusifu, kuutukuza na kuuabudu Moyo Mtakatifu wa Yesu. Tunautukuza Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa sababu ya hazina mbalimbali zilizomo ndani ya Moyo huu, hasa hazina za Huruma na Upendo usio kipimo wa Mungu Baba na wa Yesu kwa ajili ya ajili ya ukombozi wetu. Mwinjili Yohana anatuthibitishia ukweli huu anaposema, “Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi, hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele.” (Yoh 3: 16). Naye Yesu katika maisha yake hapa duniani aliuthibitisha Upendo huu wa Mungu Baba kama jinsi ambavyo Mwinjili Yohana anavyoendelea kutuambia akisema, “Ilikuwa siku kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alijua kwamba saa yake ya kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ilikuwa imefika. Alikuwa amewapenda daima watu wake walioko duniani, naam, aliwapenda mpaka mwisho”. (Yoh 13:1).

Damu ya Kristo iliyomwagika Msalabani ndiyo namna ya pekee ya kuelezea Huruma na Upendo usiopimika wa Mungu kwa wanadamu. Yesu mwenyewe anadhihirisha hili anaposema, “Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yoh 15:13). Naye Mtume Paulo katika waraka wake kwa Warumi sura ya 5 aya ya nane hadi ya tisa anakazia ukweli huu akisema, “Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu. Kwa kuwa sasa tumefanywa kuwa waadilifu kwa Damu ya Kristo, ni dhahiri zaidi kwamba, atatuokoa katika gadhabu ya Mungu. Damu takatifu ya Yesu ni kiini cha mpango mzima wa fumbo la ukombozi wetu na ndiyo gharama ya Upatanisho kati ya Mungu na sisi wanadamu na kati yetu sisi kwa sisi. Kwa umuhimu huo wa Damu Azizi ya mwokozi wetu, ni jambo la kufaa kabisa kwamba Mama Kanisa ameutenga mwezi wa saba kuwa ni mwezi wa Damu Takatifu ya Yesu. Ni kipindi ambacho wakristu wote tunaalikwa kutafakari kwa undani kabisa nafasi ya Damu ya Kristo katika mpango mzima wa ukombozi wetu, katika maisha ya Kanisa, na maana yake katika maisha yetu ya kila siku kama wakristu na katika ulimwengu wetu wa leo.

Kila mwaka, Wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu wanaadhimisha kwa namna ya pekee mwezi huu kwa sala, mafungo na makongamano. Tasaufi au kwa neno la Kiingereza, “spirituality” ya Damu Takatifu ya Yesu ndiyo inayoongoza maisha na utume wa wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu (C.PP.S.) Pengine wengine watauliza, tasaufi au “spirituality” ni kitu gani? Tasaufi ni neno pana sana na katika dunia ya leo ni ngumu kutoa maana yake ya moja kwa moja hasa kutokana na ukweli kwamba karibu kila nyanja ya maisha inadai kuwa na tasaufi au spirituality yake. Hata hivyo, kwa kifupi tunaweza kusema kuwa, tasaufi ni mtazamo wa jumla unaohuisha na kuongoza maisha ya mtu au jamii ya watu; imani yao, namna yao ya kufikiri, kuchagua, kutenda na tabia kwa jumla. Katika mazingira ya Kikristo tasaufi ni maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu.

Katika Kanisa, kuna tasaufi mbalimbali zenye msingi katika imani kwa Mungu mmoja katika Utatu Mtakatifu, Maandiko Matakatifu na hasa Agano Jipya. Msingi wa tasaufi yeyote ya kikristo ni Injili, yaani maisha na mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kila aina ya tasaufi katika Kanisa inajaribu kuitafsiri Injili na kuiweka katika matendo na maisha ya kila siku. Watu wanaofuata tasaufi fulani wanajaribu kuweka msisitizo kimatendo mafundisho ya Yesu kadiri ya wito wao na kadiri ya mazingira yanayowazunguka.

Msingi wa tasaufi ya Damu Takatifu ya Yesu uko katika mpango wa Mungu wa kuwakomboa watu wote kwani yeye hataki mtu yeyote apotee. Naye Yesu aliukamilisha mpango huu kwa kumwaga Damu yake Msalabani kama jinsi Mtume Yohane katika Kitabu cha Ufunuo anavyoshuhudia akisema, “…Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuifungua mihuri yake, kwakuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu...” (Uf. 5:9-10).

Damu iliyomwagika Msalabani ndiyo hiyohiyo inayotolewa katika sadaka takatifu ya Misa na waamini wanapata kuipokea katika Ekaristi Takatifu. Ni damu ya Upatanisho, yenye kuzika tofauti kati ya pande mbili na kuwafanya kuwa kitu kimoja kama jinsi Mt. Paolo anavyosema katika waraka wake kwa Waefeso sura ya 2 aya ya 13 hadi 14, “Lakini sasa, katika Kristu Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristu. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga.”

Itukuzwe Damu Azizi ya Kristo Yesu!

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.