2018-07-02 10:49:00

Papa Francisko asema: Imani kwa Kristo ni chemchemi ya maisha mapya!


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XIII ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, inaonesha matukio ya kuponywa kwa Binti Yairo na mwanamke mmoja aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Mwinjili Marko anayaweka matukio haya mbele ya macho ya waamini kama ushindi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Yote haya yanawezekana kwa mtu mwenye imani hata pale ambapo matumaini ya kibinadamu yanaonekana kufikia ukomo kama ilivyojitokeza kwa Binti ya Yairo.

Hii ni sehemu ya tafakari ya Injili iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe Mosi, Julai 2018, katika mwezi huu ambao umetengwa na Mama Kanisa kwa ajili ya Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo, Mto wa rehema na kisima cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu.  Yesu akiwa njiani kuelekea kwa Yairo, ujumbe kutoka kwa yule afisa wa Sinagogi, ukafika na kusema kwamba, Binti Yairo alikuwa amekwisha fariki kitambo na kwamba, kulikuwa hakuna sababu ya msingi kuendelea kumsumbua Mwalimu! Lakini, jibu la Yesu liliwakata maini kwani alisema, “Usiogope, amini tu!

Na kweli alipofika nyumbani akakuta kilio na maombolezo makubwa! Akaingia kwenye chumba alimokuwamo yule msichana, kisha akamshika mkono, akamwambia “Talitha kum” maana yake “Msichana ninakuambia inuka”! Mara msichana akasimama na kuanza kutembea, kama mtu aliyeamka kutoka kwenye usingizi mzito! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika muujiza huu, Mwinjili Marko anatumbukiza tena muujiza mwingine, wa mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akaponywa msiba wake kwa kugusa la vazi la Yesu, mara chemchemi ya damu yake ikakauka!

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, imani ya mwanamke huyu ni kubwa kiasi cha kuvuta wokovu ulioko ndani ya Kristo Yesu, aliyeng’amua mara moja kwamba, nguvu zilikuwa zimemtoka na kuanza kuangalia ni nani aliyesababisha tukio hili. Yule mwanamke aliyeponywa, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa chini mbele ya Yesu na kusimulia ukweli wote! Yesu akamwambia “Binti, imani yako imekuponya”. 

Matukio yote mawili yanajikita katika fadhila ya imani kwa kuonesha kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha mapya! Ndiye yule anayewakirimia maisha wale wanaojiaminisha kwake. Mzee Yairo na mwanamke aliyeponywa, hawakuwa ni wafuasi wa Kristo, lakini, Yesu kwa huruma na upendo wake, anawasikiliza na kujibu kwa dhati kabisa kilio cha imani yao! Hawa ni watu waliokuwa na imani kwa Kristo Yesu! Kumbe katika safari ya imani, hakuna mtu awaye yote anayepaswa kujisikia kuwa “Mvamizi au mtu wa kuja”; “Kyasaka au Mnyamahanga” na wala hakuna mtu anayeweza kujidai kwamba, anayo haki ya kuingia katika Moyo Mtakatifu wa Yesu!

Hapa kuna sharti moja tu! Ikiwa kama mtu anajisikia kwamba, anahitaji kuponywa na kwamba, anapaswa kujiaminisha kwa Kristo Yesu! Kwa waamini wanaojisikia kwamba, wanahitaji kuponywa kutoka katika lindi la dhambi, magonjwa au mahangaiko yao mbali mbali, jambo la msingi wanapaswa kuwa kweli ni watu wa imani kwa Kristo Yesu! Huu ndio ufunguo utakaowawezesha kuingia na kukaa katika sakafu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Yesu anawatambua watu kama hawa, wanaojichanganya na wengine kiasi kwamba, wanaonekana kama watu “wasiojulikana” lakini Kristo Yesu, anawaondolea hofu na woga na kuwajengea ari na moyo wa kuthubutu! Yesu anatenda kwa kuangalia na kwa njia ya maneno yake, yanayomwezesha kumwondolea mwamini mateso, mahangaiko na nyanyaso alizokumbana nazo katika safari ya maisha yake! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga mfano wa watu hawa wenye imani, ili kujifunza maneno haya yanayookoa, jicho linalomrejeshea mtu utu na heshima yake pamoja na ari ya kutaka kuendelea kuishi.

Imani na Maisha mpya katika Kristo Yesu ndizo tema kuu zinazofumbatwa katika Liturujia ya Neno la Mungu, Injili ya Jumapili ya XIII ya Mwaka B wa Kanisa. Yesu ni chemchemi ya maisha na matumaini mapya na wala hakuna sababu ya kugopa! Lakini Baba Mtakatifu anakaza kusema, waamini waogope watu wenye shingo na mioyo migumu! Hata katika hali na mazingira kama haya, Kristo Yesu, analo neno la mwisho, kwani Yeye ni chemchemi ya upendo na huruma ya Baba wa milele!

Hata pale wafuasi wake wanapoteleza na kuanguka “chali kama Mende” bado yuko tayari kusema, “Ninakuambia Inuka!” Yesu anakuwa ni chemchemi ya maisha mapya; ujasiri wa kusonga mbele katika maisha na imani! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kukimbilia tunza na ulinzi wa Bikira Maria, ili aweze kuwasindikiza katika imani na upendo mkamilifu, hususani kwa wale wenye shida zaidi. Baba Mtakatifu amewaombea wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili, ili waweze kupata faraja kwa maombezi ya Bikira Maria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.