Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Uhuru wa kidini ni msingi wa haki zote za binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, uhuru wa kuabudu ni kiini cha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. - AP

30/06/2018 08:34

Chuo kikuu cha Kipapa cha Santa Croce kilichoko mjini Roma kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji pamoja na Ubalozi wa Marekani mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 25 Juni 2018 kwa pamoja waliandaa Kongamano la Kimataifa kuhusu “Umuhimu wa kulinda uhuru wa kidini: kwa ushiriki na vitendo”. Wajumbe mbali mbali katika kongamano hili, wamekazia kwa namna ya pekee mambo makuu matatu: umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; kulinda na kudumisha amani na utulivu kama chachu muhimu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi ni mbinu mkakati inayoweza kuleta suluhu ya changamoto mbali mbali zinazoiandama familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia!

Kwa upande wake, Callista L. Gingrich, Balozi wa Marekani mjini Vatican, amekazia kwa namna ya pekee kabisa uhuru wa kidini kama sehemu ya haki msingi za binadamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayopaswa: kulindwa, kuheshimiwa na kudumishwa na wote kama mbinu mkakati wa kupambana na wimbi kubwa la dhuluma, nyanyaso na mauaji kwa misingi ya kidini. Uhuru wa kuabudu ni nguzo msingi inayobaainishwa na Katiba ya Marekani kwani ni sehemu ya utambulisho na vinasaba vyao!

Uhuru wa kidini ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini taarifa zinazonesha kwamba: uhuru wa kidini umeendelea kupuuzwa sehemu mbali mbali za dunia; kumekuwepo na dhuluma na mauaji kwa misingi ya kidini. Baadhi ya viongozi wa kidini, wamejikuta wakiwa na wakati mgumu wakati walipojaribu kutetea uhuru wa kuabudu katika nchi zao, kama ilivyotokea kwa viongozi wa Kanisa Katoliki huko Venezuela kutishiwa maisha na Serikali baada ya kutangaza kwamba, kuna watu wanapoteza maisha nchini Venezuela kutokana na njaa, magonjwa na ujinga!

Makundi ya kigaidi kama vile: Boko Haramu na Al Shabaab yamekuwa ni sababu ya maafa makubwa kwa watu na mali zao Barani Afrika. Kuna makundi ya watu kama vile Rohingya wanakabiliana na nyanyaso na mateso makali. Ikumbukwe kwamba, ubaguzi wa kidini, upo hata miongoni mwa Waislam wenyewe kutokana na Madhehebu yao. Yote haya yanaonesha hatari kubwa wanayokabiliana nayo waamini wa dini mbali mbali duniani. Tamko la Haki Msingi za Binadamu la Umoja wa Mataifa linakazia sana uhuru wa: mawazo na dhamiri; uhuru wa kidini na kwamba, mtu anao uwezo wa kubadili dini kadiri anavyotaka mwenyewe.

Kwa upande wake Monsinyo Khaled Akasheh, Afisa mwandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini kama njia ya kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Waamini wa dini mbali mbali washikamane katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wajenge utamaduni wa kuzungumzana na kuweka katika matendo yale mambo msingi yaliyojadiliwa kwa ajili ya mafao ya wengi. Professa Marco Impagliazzo, Rais wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, kwa muda wa miaka 50 ya uuwepo na huduma yake, imekuwa ni chombo na daraja la majadiliano kati ya watu wa Mataifa ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Hii ni Jumuiya ambayo pamoja na majadiliano, lakini imeendelea kujikita katika huduma kwa maskini, wagonjwa, wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia! Neno la Mungu, huduma kwa maskini na utetezi wa amani ni mambo msingi katika maisha na utume wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kama yalivyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Monsinyo Luis Navarro, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha cha “Santa Croce” kilichoko mjini Roma anakaza kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema, haki ya maisha ni ya kwanza na inafuatiwa na haki ya uhuru wa kuabudu; unaopaswa kulindwa, kuheshimiwa na kudumishwa na wote.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenye kongamano hili amekazia mambo makuu yafuatayo: Kwanza kabisa ni kuondokana na siasa za kutojali mahangaiko ya watu; umuhimu wa kuheshimu utawala wa sheria na usawa wa watu wote mbele ya sheria; kuheshimiana na kuthaminiana. Ikumbukwe kwamba, viongozi wa kidini wanayo dhamana na wajibu wa kukemea vitendo vyote vinavyosigana na sheria kanuni na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu na kwamba, majadiliano ya kidini ni muhimu sana katika kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Amegusia umuhimu wa elimu ya dini kama njia makini ya kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho kwa kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani. Biashara haramu ya silaha haina budi kukomeshwa ili kulinda uhai wa binadamu na hatimaye, kuondokana na utamaduni wa kifo!

Naye Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki anasema, inasikitisha kuona kwamba, uhuru wa kidini ni jambo ambalo linataka kuwekwa pembezoni mwa maisha ya hadhara, ili kuonekana kana kwamba ni jambo la mtu binafsi. Dini zimetumiwa na baadhi ya viongozi kuchochea: vita, ghasia na mipasuko ya kijamii na matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kumbe, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko, waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Uhuru wa kidini usipozingatiwa na kuheshimiwa, matokeo yake ni vita na kinzani mbali mbali.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume “Ecclesia in Medio Oriente” yaani “Kanisa Mashariki ya Kati” anaonesha mateso, dhuluma na nyanyaso wanazokabiliana nazo Wakristo huko Mashariki ya Kati kutokana na utawala wa mabavu na kwa wakati huo, utawala wa Rais Saddam Hussein. Matokeo yake ni kuibuka na kuenea kwa misimamo mikali ya kidini na kiimani; vita na ghasia kati ya watu; hali ambayo sasa imepelekea dhuluma, nyanyaso na mauaji ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Hii ndiyo hali inayowakuta Wakristo huko Siria, Iraq, Misri, Uturuki na Lebanon. Hata katika nchi yao wenyewe, bado wanaendelea kujisikia kuwa ni “watu wa kuja” wageni na wapita njia”. Hawa kimsingi wanaendelea kujisikia kuwa ni raia daraja la pili, jambo ambalo si haki kabisa.

Kardinali Leonardo Sandri anakaza kusema: haki, amani, maridhiano na uhuru wa kidini hauna budi kukuzwa na kudumishwa na Jumuiya ya Kimataifa sanjari na  kulinda haki msingi za binadamu. Kilio na mahangaiko ya wananchi wa Siria ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Wakristo wanayo haki ya kubaki nchini Iraq, ili kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya nchi yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

30/06/2018 08:34