Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Tafakari ya Neno la Mungu: Fumbo la mateso na kifo katika maisha!

Mateso na kifo ni ya changamoto zinazomwandama mwanadamu, changamoto ni kuangalia Fumbo la Pasaka kwa imani na matumaini. - RV

30/06/2018 07:16

UTANGULIZI: Mungu ameumba kila kitu kuwa ni chema. Na alipomaliza kazi yake ya uumbaji “akaona kila kitu alichokifanya na tazama ni chema sana” (Rej. Mwa. 1:31). Hata hivyo mabaya, mateso, adha mbalimbali na kifo ni mang’amuzi ambayo daima yamemwandama mwanadamu kwa maumivu na kwa maswali mengi. Maandiko Matakatifu katika dominika hii ya 13 ya mwaka B wa kanisa yanauangazia uhalisia huu na kutoka katika hekima ya kimungu kutualika tuone kuwa Mungu ametuumbia mema, anatukusudia mema katika maisha yetu na ametuandalia mema zaidi katika makao yake mbinguni.

MASOMO KWA UFUPI: Somo I (Hek. 1:13-15; 2:23-24) ni kutoka katika mkusanyiko wa vitabu vya Hekima, vitabu ambavyo vinaangalia uhalisia wa maisha ya mwanadamu si moja kwa moja kutoka katika ufunuo wa kimungu bali kutoka katika mambo yanayoonwa kila siku maishani. Na hivi kutoka hapo hulenga kufundisha busara ya kuishi vema kwa ustawi na kutoa malezi mema. Katika somo hili la kwanza, mwandishi wa kitabu cha Hekima ya Sulemani anatafakari juu ya fumbo la kifo, jambo linaloleta hofu kubwa katika maisha ya mwanadamu.

Kwa mang’amuzi yake tu ya hekima anaona kuwa haiwezekani Mungu aliyeumba vitu viweze kuwapo halafu huyohuyo alete kifo ili vitu hivyo alivyoviweka viondoke.  Na anang’amua kuwa lazima kutakuwa na kitu kingine nje ya Mungu kinacholeta uharibifu huo. Ni hapo mwandishi anaona kuwa kifo na uharibifu unaletwa na shetani. Anasema “ila ulimwengu uliingiwa na mauti kwa husuda yake shetani” na anaongeza kuwa “nao walio upande wake hupata kuionja”. Hapa tunaona kuwa hata kabla ya ufunuo wa Kristo tayari hekima iliwaongoza watu kung’amua kuwa kifo kwa maana ya uharibifu huwagusa wale walio nje ya Mungu na kumbe walio upande wa Mungu, asiyeharibika, hawataguswa na uharibifu.

Somo II (2Kor. 8:7, 9, 13-15) mtume Paulo anahimiza juu ya fadhila ya kiutu, ukarimu. Anaialika jumuiya ya wakristo wa Korinto kuguswa na mahitaji ya wenzao wa kanisa la Yerusalemu na kufanya harambee au mchango kwa ajili yao. Mchango huo Mtume Paulo hawalazimishi, anawaalika wafanye kwa moyo ili uwe wa Baraka kwao.  Tena anawaalika kujifunza kutoka kwa Kristo ambaye alijitoa kwa kila kitu kwa ajili ya wengine. Yeye Kristo alikuwa tajiri lakini alifanyika masikini kwa ajili yao ili wao wapate kuwa matajiri kwa umasikini wake. Ni ukarimu anaowaalika utakaoonesha kwa matendo pia upendo walionao kwa Kristo. Anaongeza kuwa lengo ni kujenga jumuiya inayojaliana na inayoshirikishana majaliwa ya Mungu ili kwamba yeye aliye na vingi visimzidi kwa maana atamshirikisha yule asiye nacho na yule asiyenacho hatapungukiwa kwa sababu atajaliwa kwa ukarimu wa wengine.

Injili (Mk 5:21-43) Yesu anatenda miujiza miwili. Katika muujiza wa kwanza anamponya mwanamke aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka kumi na miwili na katika muujiza wa pili anamfufua binti wa Yairo aliyekuwa pia na umri wa miaka kumi na miwili. Katika muujiza wa kwanza mwanamke alikuwa ameshahangaika kutafuta tiba kwa matabibu wengi tena kwa kutumia gharama kubwa lakini hakuwa amepata tiba. Hekima na ujuzi wa mwanadamu unaweza kumsaidia mwanadamu katika mambo kadhaa tu na sio yote. Mama huyo kwa kulitambua hilo na akiisha muona Yesu anaamua kuweka imani na matumaini yake yote ya kupona kwa Yesu. Kwa jinsi imani yake ilivyokuwa kubwa hakwenda kama wagonjwa wengine na kuongea na Yesu, yeye alisema tu moyoni mwake “nikigusa tu pindo la vazi lake nitapona” na ndivyo ilivyokuwa alifika, akagusa kwa imani si kama wengine waliomgusa wakimsonga kwa sababu ya umati, akapona. Naye Yesu anauliza “ni nani amenigusa”, si kwa hasira bali ni kwa kujali kama ambavyo daima amejali na kuguswa na mahitaji ya watu.

Katika muujiza wa pili Yesu anapomfufua binti wa Yairo anaonesha kuwa Yeye ndiye Bwana wa uhai na tena wote wanaomwamini hata kama wanakufa wataendelea kuishi. Tunaona alipoambiwa kuwa binti amekwishakufa Yeye alisema “usiogope, amini tu...kijana hakufa bali amelala tu”. Ni wazi wao waliona kuwa amekufa na kweli alikuwa amekufa. Ila katika macho ya Bwana wa uzima, aliye ufufuo na uzima na ambaye kwake wote waliokuwa wanaishi kijana hakuwa amekufa bali alikuwa anaishi. Ndiye anayerudisha uhai pale pasipo na uhai, ndiye anayerudisha matumaini pale pasipo na matumaini, ndiye anayejenga upya pale palipoanguka.

TAFAKARI: Mtakatifu Augostino wa Hippo ni kati ya wanateolojia waliotafakari kwa kina juu asili ya uovu katika maisha ya mwanadamu. Anasema Mt. Augustino “nilijiuliza ubaya watoka wapi sikupata jibu”. Kwake jibu la utafiti huu juu ya asili ya uovu au ubaya katika maisha linapatikana katika kumwongokea Mungu (rej. KKK n. 385). Kwa nini? Kwa sababu uovu au ubaya unapata asili yake kutoka kwa yule mwovu shetani. Ni katika kumwongokea Mungu mwanadamu anaweza kujinasua kutoka katika himaya ya uovu na katika mnyororo wa kuendeleza maovu.

Mawazo haya ya Mtakatifu Augostino tunayaona waziwazi katika maovu yanayotuzunguka. Tutaje uovu upi? Vita vinavyoendelea kila kukicha ulimwenguni? Harakati za kisiasa zinazoleta hofu, mahangaiko ya raia na ukosefu wa amani? Vita vya kiuchumi vinavyomkandamiza zaidi asiye nacho na kuzidi kumneemesha aliyenacho? Chokochoko katika jamii zinazoshabikia utengano, ukabila, ubaguzi na dharau ama kwa jamii moja na nyingine au kwa mtu na mtu katika jamii moja? Je, haya yote hayapati chimbuko katika ubinafsi, choyo, tamaa mbaya ya mali, madaraka au umaarufu? Ni katika kurudi kwa Mungu aliye asili na chemchemi ya mema, ni katika kujifunza hekima yake na katika kumwomba kwa imani ndipo lilipo suluhisho la ubaya unaoleta adha zinazomsonga mwanadamu.

Maandiko Matakatifu siku ya leo yamegusa mambo mawili mahsusi: ugonjwa na kifo. Na haya Je, yanatoka wapi? Magonjwa, kifo pamoja na uchungu katika maisha vinaoneshwa katika sura ya 3 ya kitabu cha Mwanzo kuwa ni matokeo ya yanayoupata ubinadamu ulioanguka katika dhambi ya asili. “Mungu akamwambia mwanamke ‘hakika nitakuzidishia uchungu wako na kuzaa kwako...akamwambia Adamu ‘ ardhi imelaaniwa kwa ajili yako, kwa uchungu utakula mazao yake... na utakufa ... utarudia ardhi ambayo katika hiyo ulitwaliwa” (Rej. Mwa. 3:16-19).

Hata hivyo Kristo kwa kifo na ufufuko wake ameipindua adhabu hii kama ambavyo alikwisha dhihirisha kwa kuponya wagonjwa na kufufua wafu katika maisha yake ya kimwili hapa duniani. Ni hapo akaonesha kuwa magonjwa na hata kifo si tena adhabu kwa wote wanaomwamini bali njia ya wokovu kama njia ile ile aliyoipita yeye akaupatia ulimwengu mzima wokovu. Ndiyo maana Kanisa katoliki linapohubiri uponyaji linahubiri na kujikita katika uponyaji wa nafsi dhidi ya dhambi na utawala wa shetani: na linapohubiri juu ya uzima linatafuta kwanza uzima wa kiroho wa kundi lililokabidhiwa. Ni katika nafsi iliyoponywa dhidi ya dhambi na utawala wake na ni katika roho iliyo na uzima wa kimungu ndani yake ndipo mwanadamu anaweza kuishi vema hapa duniani kama alivyomkusudia Mungu muumba wake. “imani yako imekuponya” ndicho alichokikazia Yesu mwenyewe katika ishara na uponyaji alioufanya.

Mafundisho haya yanatualika tufikiri mara mbili mbili na tena kwa imani juu ya mwelekeo uliopo, mwelekeo unaozidi kukua, mwelekeo unaojijenga juu ya ibada za uponyaji. Yafaa kujiuliza “ninahitaji kuponywa nini?” au “ninatafuta uponyaji upi”. Yafaa kufikiri hivi kwa sababu kuna uwezekano baadhi ya wahudumu wakawa wanatafuta kucheza na hisia za watu kwa malengo wanaoyajua wenyewe kwa mwamvuli wa ibada za uponyaji. Na tena kuna uwezekano waamini wakawa wanatafuta uponyaji kama njia ya mkato wakiruka hatua muhimu kama kukabiliana na uhalisia wa mtindo wa maisha au wa mahangaiko ya imani. Na hii inaweza kuwa ndio sababu ya kuhama kutoka kwa mhudumu mmoja kwenda kwa mwingine na hata kuhama kutoka dini moja kwenda nyingine kana kwamba kuhama toka hospitali moja hadi nyingine kumtafuta daktari bingwa. Ni uponyaji wa namna hii anaoukusudia Kristo? Tuzidi kumwomba Mungu atuongezee imani. Atuimarishe katika tumaini lake na atujalie uzima wake.

Padre William Bahitwa.

Vatican News.

 

 

30/06/2018 07:16