Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Uekumene unajielekeza katika: Umoja wa imani na dhana ya Sinodi

Uekumene unajielekeza katika ushuhuda wa imani na utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. - AP

29/06/2018 13:51

Katika mkesha wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 29 Juni, Kila mwaka, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 28 Juni 2018 amekutana na kuzungumza na Ujumbe wa wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza, wa Kanisa la Costantinopoli kielelezo makini cha umoja wa Kanisa hilo na Kanisa Katoliki. Wajumbe hao wamemkabidhi Baba Mtakatifu Francisko ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza uliojikita zaidi katika kumbu kumbu ya Wakristo! Anasema, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe kubwa ya Watakatifu Petro na Paulo, waliovishwa taji ya kifodini na kwa njia hii, Habari Njema ya Wokovu imeweza kutangazwa na kushuhudiwa sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni wakazi wa Yerusalemu ya mbinguni, miamba wa imani, watangazaji na mashuhuda wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, waliosadaka maisha yao, kwa kuacha yote, ili kuambata ukweli kuhusu Mwenyezi Mungu.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaendelea kudadavua kwa kusema, ushuhuda wa maisha na mahubiri yao hadi kumwaga damu kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, ni changamoto na mwaliko kwa Wakristo wa nyakati hizi, kuwakumbuka wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowatangazia Neno la Mungu, tena kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wa maisha yao,  ili Wakristo waige imani yao! Huu ni mchakato wa uinjilishaji unaosimikwa katika ushuhuda wa miamba ya imani unaowataka Wakristo kujikita katika kuwatangazia Habari Njema wale wote ambao bado hawajabahatika kuisikia pamoja na kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya, dhamana na utume nyeti kwa watu wa ulimwengu mamboleo!

Umoja na mshikamano wa Wakristo ni nyenzo msingi katika kutangaza na kushuhudia: Uekumene wa huduma na mshikamano wa upendo; Majadiliano ya kiekumene kama chemchemi ya matumaini ya umoja wa Wakristo na kwamba, kwa sasa mwelekeo ni kwa Makanisa kujikita katika umoja wa imani unaofafanuliwa mintarafu Sheria kanuni za Kanisa pamoja na taalimungu. Muswada wa hati hii unaendelea kuboreshwa. Dhamana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo ni muswada mwingine, unaofanyiwa kazi kwa sasa, ili kuvuka vikwazo na mipasuko ya Makanisa iliyosababishwa na historia pamoja na mapokeo mbali mbali. Lengo ni kutaka kuhakikisha kwamba, kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja, Wakristo wanapata kumtukuza Mwenyezi Mungu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Utangazaji na ushuhuda wa Injili unapaswa kujikita si tu katika majadiliano ya kitaalimungu, bali pia kuangalia changamoto mamboleo na kuzipatia ufumbuzi kadiri ya mwanga wa Injili, kama ajenda ya Wakristo wote kwa ajili ya mafao ya wengi. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha uekumene wa mshikamano, ili kujenga na kuimarisha utamaduni wa mshikamano katika masuala ya uchumi, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; katika maendeleo ya sayansi na teknolojia na hata katika masuala ya kijamii na kisiasa; ili medani zote hizi za maisha, ziweze kupambwa na ushuhuda wa upendo wa Kikristo. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakaza kusema, anatarajia kushiriki kikamilifu katika Siku ya Tafakari na Kuombea Amani huko Mashariki ya Kati, iliyoandaliwa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 7 Julai 2018, huko Bari, Kusini mwa Italia. Anasema, itakuwa ni Siku maalum ya kusali na kutafakari kuhusu haki, amani na upatanisho, mambo msingi yanayoonesha utume wa Kanisa hapa duniani. Amani ya kweli inajikita katika: uhuru, haki na mshikamano.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakaza kusema, walimwengu wanatarajia kuona Makanisa yakiwaongoza kuelekea katika undani wa ukweli huu, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu kwani majadiliano ya kweli yanakuza na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho. Amani ya kweli haiwezi kupatikana kwa njia ya mtutu wa bunduki, bali kwa njia ya upendo usiotafuta mafao yake binafsi. Mafuta ya imani yatumike kuganga na kuponya madonda ya binadamu! Maadhimisho haya yawe ni kikolezo cha hija ya kiekumene kuelekea umoja wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

29/06/2018 13:51