Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko: Michezo idumishe: amani, utulivu, ufanisi na umoja

Papa Francisko anawataka wanamichezo kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kama kielelezo cha amani, utulivu na weledi katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao katika jamii.

29/06/2018 09:00

Mashindano ya “Sette Colli” yaliyoandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Kuogelea Kitaifa nchini Italia, ni matunda na juhudi za kiufundi zinazowashirikisha wanamichezo kukuza na kudumisha nidhamu, mapambano na umoja wa wanamichezo kama timu. Huu ni mchakato wa sadaka na majitoleo makubwa yanayopania kupata ushindi unaotarajiwa na kwamba, hiki ni kielelezo makini na kivutio kwa vijana wa kizazi kipya, wanapowaona vijana wenzao wakipata mafanikio makubwa katika michezo na maisha!

Mchezo wa kuogelea kama ilivyo michezo mingine yote, kama inatekelezwa kwa dhati kabisa, inakuwa ni fursa ya majiundo makini ya tunu msingi za kiutu na kijamii, ili kujenga na kuimarisha mwili na utashi; na pia kutoa nafasi ya mtu kujifahamu, kujikubali na kujipokea jinsi alivyo! Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 28 Juni 2018 wakati alipokuwa anazungumza na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Kuogelea Kitaifa nchini Italia. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kucheza kwa pamoja kama timu, kwa kushirikiana na kusaidiana; ili kukuza na kudumisha: amani, utulivu, ufanisi na weledi kwa kuwa kuonesha mambo yanayofanana. Haya ni matunda ya juhudi za mtu binafsi, lakini zinazowashirikisha wengine pia ili kufikia lengo linalokusudiwa. Hapa ni mahali pa kusaidiana kwa kushikamana! Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amemkumbuka na kumwombea mwanamichezo Noemi aliyefariki dunia hivi karibuni hapa mjini Roma.

Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewataka wanamichezo kuwa ni mfano bora wa kuigwa na vijana wenzao, ili kuwasaidia kujenga matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Lugha ya michezo inafahamika na kueleweka vyema na vijana wa kizazi kipya. Kumbe, ni wajibu wa wanamichezo kuwa ni mashuhuda na vyombo vya tunu msingi za maisha ya kijamii, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya jamii wanamoishi. Amewatakia wanamichezo wote kujisikia furaha wanaposhiriki katika mashindano mbali mbali kwani michezo inajenga moyo wa udugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

29/06/2018 09:00