2018-06-29 08:00:00

Makardinali dhamana yenu ni: Uaminifu, uwajibikaji na utume kwa Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 28 Juni 2018 amewatunukia heshima Makardinali wapya 14 na kuwakumbusha kwamba, Kristo Yesu alipokua anatangaza kuhusu mateso, kifo na ufufuko wake, aliwaambia kwamba, anawatangulia na mtu yoyote anayetaka kuwa mkubwa kati yao, anapaswa kuwa mtumishi wao! Ujumbe huu ni matokeo ya malumbano yaliyojitokeza miongoni mwa Mitume wa Yesu, waliokuwa wanatafuta nafasi za kwanza; wengine wakaelemewa na wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko! Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kipaumbele cha kwanza kinatolewa kwa ajili ya utume wa Kanisa! Malumbano kama haya anasema Baba Mtakatifu si ajabu yakajitokeza hata kwenye nafasi mbali mbali za uongozi ndani ya Kanisa.

Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kujikita katika toba na wongofu wa ndani; mabadiliko ya maisha ya kiroho na mageuzi ya Kanisa mintarafu mwanga wa umisionari, ili kuondokana na tamaa ya mambo binafsi, tayari kuanza kuangalia, ili hatimaye, kuanza kujikita katika utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha. Toba na wongofu wa ndani, uwasaidie waamini kuondokana na dhambi pamoja na ubinafsi, ili kujikita katika uaminifu na uwajibikaji, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Changamoto hii ni kubwa hasa nyakati za mateso kwa watoto wa Kanisa, ambao wanapaswa kuwawajibikia, kuwapokea pamoja na kuwasindikiza, bila ya kujitafuta wao wenyewe pamoja na mambo yao! Utume wa Kanisa uwawezeshe viongozi wa Kanisa kuona sura za watoto wa Kanisa wanaoteseka badala ya kujifungia katika tamaa na usalama wa maisha binafsi. Matokeo yake ni chuki, hasira pamoja na kukosa utulivu na amani ya ndani, hali inayopelekea mtu kushindwa kutoa nafasi kwa ajili ya wengine, maisha ya Kikanisa, maskini pamoja na kushindwa kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema: Unyenyekevu katika huduma; Heri za Mlimani pamoja na Utenzi wa Bikira Maria, “Magnificati” ni tunu msingi zinazopaswa kumwilishwa kila kukicha! Uongozi wa Kanisa unajikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha utu wa jirani. Viongozi wa Kanisa wawe ni mafuta ya faraja na divai ya matumaini kwa jirani zao katika kuganga na kuponya madonda yao! Makardinali wakumbuke kwamba, wanatumwa kuwahubiri maskini Habari Njema, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha waliosetwa na kutangaza Mwaka wa Bwana!

Baba Mtakatifu Francisko amewaambia Makardinali kwamba, wakati huu wakiwa njiani kuelekea Yerusalemu, Kristo Yesu anawatangulia na kwamba, uongozi wenye mvuto na mashiko unajikita katika unyenyekevu na huduma kwa Kristo na Kanisa lake. Kristo Yesu, kabla ya kuinamisha kichwa na kukata roho pale Msalabani, alijinyenyekesha na kuwaosha miguu Mitume wake! Hii ndiyo heshima ya hali ya juu kabisa ambayo Makardinali wanaweza kupewa yaani: kumhudumia Kristo Yesu kwa njia ya uaminifu kwa watu wa Mungu: miongoni mwa watu wanaoteseka kwa baa la njaa, wanaosahaulika na kutelekezwa na jamii; wagonjwa na wafungwa; waathirika wa dawa haramu za kulevya; hii ni huduma makini inayofumbatwa kwa watu halisi wenye historia na matumaini yao; matarajio yao halali na wasi wasi; kwa mateso na madonda ya maisha. Kwa njia hii, Makardinali wataweza kutangaza na kushuhudia maana halisi ya uongozi ndani ya Kanisa, ili kusaidiana na kunyanyuana badala ya kuwabeza wengine!

Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha wosia ulioandikwa na Mtakatifu Yohane XXIII aliyemshukuru Mungu kwa kuzaliwa kati ya watu maskini na kupewa heshima na watu hawa na kwamba, anayo furaha ya kuitupa mkono dunia katika hali ya umaskini, baada ya kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na Kanisa baada ya kutajirishwa kupita kikomo katika maisha na utume wake kama Padre na Askofu. Katika nadhiri ya ufukara aliyojiwekea tangu ujana wake, anamshukuru Mungu kwa moyo wa ufukara ulimwezesha kutekeleza utume wake kwa furaha, kiasi hata hakuwa na sababu ya kuomba nafasi ya upendeleo na fedha kwa ajili yake, ndugu wala marafiki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.