Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Familia ya Damu Azizi ya Yesu inakutana na Papa Francisko Vatican!

Familia ya Damu Azizi ya Yesu inakutana na Papa Francisko tarehe 30 Juni 2018 tayari kwa maandalizi ya Mwezi Julai, uliotengwa na Mama Kanisa kwa ajili ya Ibada kwa Damu Azizi ya Yesu.

29/06/2018 07:47

Akiongozwa na tafakari ya kina juu ya: Huruma na Upendo wa Mungu kwa wanadamu, Mtakatifu Gaspari Del Bufalo alianzisha Shirika la kitume la Wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu, tarehe 15 Agosti, 1815. Yeye mwenyewe alipenda kujua lugha elfu ili kuwafikishia watu wote duniani habari njema kwamba Mungu anawapenda wote. Damu Takatifu ya Yesu ndiyo msingi na chemchem ya maisha ya kiroho, kijumuiya na kitume ya Wamisionari. Tafakari ya Neno la Mungu, Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo, yaani: kuziishi vema Sakramenti hasa za Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Ibada ya njia ya Msalaba, kuabudu Ekaristi Takatifu, Sala na nyimbo mbalimbali, Rozari ndogo ya Damu Takatifu, Litania za Damu ya Kristo n.k ni baadhi ya mambo yanayopamba maisha ya kiroho ya wamisionari hao.

Katika maisha ya kijumuiya, Damu ya Kristo ni chachu ya kuishi maisha ya kidugu chini ya kifungo cha Upendo. Kifungo hiki cha Upendo kinadhihirishwa katika maisha ya mshikamano wa dhati wakati wa shida na wakati wa furaha. Damu ya Kristu ndiyo kiini cha umoja na undugu wao bila kujali tofauti zao za utaifa, rangi, na tamaduni wakisisitiza umuhimu wa majadiliano. Katika maisha yao ya kitume, wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu wanashiriki katika kazi ya kitume ya Kanisa ya uinjilishaji wakijitahidi kuitikia kilio cha damu hasa kwa kuwa katika mshikamano na wale waliowanyonge, masikini na wale wanaosahauliwa au kuwekwa pembeni.

Tasaufi ya Damu Takatifu ya Yesu inaongoza pia maisha na utume wa Masista Waabuduo Damu Azizi, ASC, ambao Shirika lao lilianzishwa na Mtakatifu Maria De Mathias ambaye alikuwa mfuasi wa Mtakatifu Gaspari. Mt. Gaspari alimshauri kuanzisha Shirika kwa ajili ya masista. Kutokana na utajiri wa tasaufi hii, kuna mashirika mengine ya kitawa zaidi ya kumi yenye kubeba jina la Damu Takatifu ya Yesu na kuongozwa na tasaufi yake. Hata hivyo tasaufi hii si kwa ajili ya watawa pekee bali inapaswa kuongoza maisha ya kila mkristu kwa sababu chimbuko lake linatoka katika fumbo la Ukombozi wetu. Mbali na mashirika ya kitawa kuna waumini wengi sehemu mbalimbali za dunia ambao wanaongozwa na tasaufi hii. Wako katika vikundi mbalimbali na kwa ujumla wao wanaunda Ushirika wa Damu ya Kristo, “Unione Sanguis Christi” (USC).

Lengo la Ushirika huu ni kuamsha maisha ya ukristu kupitia tasaufi ya Damu Takatifu kwa kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu na kupokea mara kwa mara sakramenti za upatanisho na Ekaristi takatifu. Katika maisha ya kila siku, mwenye kuongozwa na tasaufi ya Damu Takatifu ya Yesu hutambua thamani ya uhai na anakuwa tayari kutetea maisha na kupambana na kuupinga utamaduni wa kifo katika jamii. Kwa kuwa Damu ya Yesu yenye thamani ilimwagika kwa ajili ya wote, anayefuata tasaufi hii atatambua utu, thamani na heshima ya kila mwanadamu na haki yake ya kuthaminiwa na kuheshimiwa. Atakuwa pia mstari wa mbele katika kushirikiana na Kanisa kupigania na kujenga misingi ya haki na amani katika jamii. Hatimaye atakuza umoja na undungu ambao Yesu ameuanzisha kwa kumwaga Damu yake Msalabani.

Ili kuweza kushiriki kikamilifu katika kuuenzi mwezi wa Damu Takatifu ya Yesu, familiya nzima ya Damu Takatifu itafanya maadhimisho maalum ikiwa ni pamoja na hija katika makao makuu ya Kanisa Katoliki yaani mjini Vatican. Tunapoongelea familia ya Damu azizi tunamaanisha wamisionari wa Damu Takatifu, watawa na waamini walei wote wanaoongozwa na tasaufi ya Damu Takatifu. Familia hii itakutana na Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 30/6/ 2018 katika ukumbi wa Mtakatifu Paulo wa Sita kuanzia asubuhi Saa 3:00 – 6:00 kwa saa za Ulaya. Lengo la hija hii, ni kukutana na Mungu, kutaka kukutana na Yesu Kristo Bwana wetu na kumsikiliza kupitia mtumishi wake Papa Francisko.

Tunafahamu kuwa kupitia Baba Mtakatifu, Mungu ana ujumbe maalum wa kutupatia, kwa ajili ya maisha na utume wetu. Mwaka 2001 wakati Wamisionari wa Damu Takatifu walipokutana na Baba Mtakatifu wa wakati huo, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwakumbusha kwamba katika utume wao wanapaswa kwenda kule ambako wengine hawapendi kwenda. Kwa maneno haya, Mtakatifu Yohane Paolo II aliwakumbusha wamisionari juu ya kipaumbele katika utume wao wanachopaswa kuwapa masikini, wanyonge na waliopembezoni mwa jamii. Kwa jinsi hiyohiyo tunasubiri kuupokea ujumbe wa Mungu kupitia kwa Baba Mtakatifu.

Kabla ya kukutana na Baba Mtakatifu, asubuhi kutakuwa na mafundisho au katekesi juu ya Damu ya Kristo yatakayotolewa na Padre Marko Rupnik, S.J na pia kutakuwa na ushuhuda wa walei mbalimbali katika kuishi tasaufi ya Damu Takatifu na wajibu wao kwa kanisa na jamii. Siku hiyo hiyo ya tarehe 30 kuanzia saa moja jioni katika Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane pale Laterano, kutakuwa na mkesha maalum kwa ajili ya sherehe ya Damu Takatifu ya Yesu.Tarehe Mosi Julai ndiyo sherehe yenyewe na Misa Takatifu itafanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Saa:4:00 asubuhi kwa saa za Ulaya, ikiongozwa na Kardinari Angelo Comastri. Saa Sita mchana utakuwa wakati mwingine wa kuungana na Baba Mtakatifu katifu katika kusali sala ya Malaika wa Bwana na kisha kupokea salamu na baraka toka kwa Baba Mtakatifu. Tunategemea kuwa huo utakuwa ni mwanzo mzuri wa kuuenzi mwezi wa Damu Takatifu. Nanyi pia tunawaalika na kuwatakia baraka tele katika mwezi huu mkitafakari na kuiga upendo wa Kristu aliyejitoa kwa ajili yetu.

Itukuzwe Damu Azizi ya Kristo Yesu!

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S.

 

 

29/06/2018 07:47