2018-06-28 06:56:00

Mambo msingi ya kuzingatia ili kudumisha uhuru wa kidini duniani!


Chuo kikuu cha Kipapa cha Santa Croce kilichoko mjini Roma kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji pamoja na Ubalozi wa Marekani mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 25 Juni 2018 kwa pamoja waliandaa Kongamano la Kimataifa kuhusu “Umuhimu wa kulinda uhuru wa kidini: kwa ushiriki na vitendo”. Wajumbe mbali mbali katika kongamano hili, wamekazia kwa namna ya pekee mambo makuu matatu: umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; kulinda na kudumisha amani na utulivu kama chachu muhimu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi ni mbinu mkakati inayoweza kuleta suluhu ya changamoto mbali mbali zinazoiandama familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenye kongamano hili amekazia mambo makuu yafuatayo: Kwanza kabisa ni kuondokana na siasa za kutojali mahangaiko ya watu; umuhimu wa kuheshimu utawala wa sheria na usawa wa watu wote mbele ya sheria; kuheshimiana na kuthaminiana. Ikumbukwe kwamba, viongozi wa kidini wanayo dhamana na wajibu wa kukemea vitendo vyote vinavyosigana na sheria kanuni na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu na kwamba, majadiliano ya kidini ni muhimu sana katika kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Amegusia umuhimu wa elimu ya dini kama njia makini ya kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho kwa kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani. Biashara haramu ya silaha haina budi kukomeshwa ili kulinda uhai wa binadamu!

Kardinali Parolin, amewashukuru wadau wote waliowezesha kongamano hili ambalo limetoa fursa ya kuweza kusikiliza hata shuhuda kwa waamini wanaoteseka kutokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani; umuhimu wa kukuza na kudumisha uhuru wa kidini kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, serikali mbali mbali zina wajibu na dhamana ya kulinda na kudumisha uhuru wa kidini. Sheria ya Kimataifa ya Uhuru wa Kidini, iliyopitishwa kunako mwaka 1998 na Rais Bill Clinton wa Marekani inakazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa kulinda na kudumisha uhuru wa kidini kimataifa, kama sehemu ya sera na mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa kutoka Marekani.

Sheria hii ni muhimu sana kwa nyakati hizi kutokana ongezeko kubwa la mauaji, dhuluma na nyanyaso zinazofanywa na waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani; Ubaguzi kwa misingi ya kidini pamoja na mateso yanayofanywa kwa makusudi na baadhi ya viongozi wa kisiasa ili kuweza kujijenga kisiasa. Katika changamoto hii kubwa ya ukosefu wa uhuru wa kidhamiri na uhuru wa kidini, Kanisa Katoliki, linapenda kuwatia shime waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kidini na kwamba, hii ni dhamana inayopaswa pia kushuhudiwa katika maisha ya hadhara na wala si jambo la kuonewa aibu hata kidogo. Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja ya kwa viongozi wa serikali, viongozi wa kidini, viongozi wa Jumuiya na Mashirika ya Kimataifa bila kuwasahau viongozi wa vyama vya kiraia, hawana budi kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa kufanya hivi ni kutambua na kuthamini usawa, utu na heshima ya kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, kuvunja uhuru wa kidini ni sawa kabisa na kuvunjwa kwa haki msingi za binadamu.

Shuhuda za nyanyaso na dhuluma za kidini zilizotolewa na mwanachama wa Jumuiya ya Yazidi kutoka Iraq ni ushuhuda kwamba, uhuru wa kidini uko mashakani katika baadhi ya nchi. Kardinali Parolin anasikitika kusema kwamba, Jumuiya ya Yazidi imekuwa ikukumbana na matukio ya uvunjwaji wa haki msingi za binadamu; utekaji nyara, utumbukizwaji wa watu katika mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, mateso, wongofu wa shuruti pamoja na mauaji kwa misingi ya kidini. Nyumba za Ibada pamoja na madhabahu ya Jumuiya ya Yazidi yamebomolewa, ndiyo maana, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana ili kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu , msamaha, upatanisho na maridhiano kati ya watu.

Vatican inapenda kukazia kwa namna ya pekee kabisa: umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani; umuhimu wa kukuza na kudumisha haki, amani na utulivu kama chachu muhimu sana ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, waamini waendelee kujikita katika majadiliano ya kidini kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi; ili kujenga umoja na mshikamano kwa ajili ya huduma makini kwa familia ya binadamu. Waamini wa dini mbali mbali waheshimiane na kuthaminiana na kwamba, elimu makini ni nyenzo madhubuti kabisa kwa ajili ya kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni miongoni mwa vijana wa kizazi kipya!

Umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii anasema Kardinali Parolin ni muhimu sana katika kupambana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, kwa kutambua kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Hii ni changamoto kwa wadau mbali mbali kupambana na utamaduni wa kifo unaoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Misimamo Mikali ya kidini na kiimani ni hatari sana kwa maendeleo ya familia ya Mungu duniani. Inasikitisha kuona kwamba, kuna harakati za makusudi kabisa za kutaka kuwafutilia mbali Wakristo huko Mashariki ya Kati! Lakini, ikumbukwe kwamba, Wakristo ni utambulisho na sehemu ya vinasaba vya Mashariki ya Kati.

Vatican inapenda kuchangia mambo muhimu yafuatayo ili kukuza na kudumisha uhuru wa kidini: Kwanza kabisa: Wamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuheshimiana, kuthaminiana, kulindana na kusaidiana kwa hali na mali pamoja na ushiriki mkamilifu katika maisha ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kuhakikisha kwamba haki, amani na maridhiano vinatawala miongoni mwa watu! Pili: Utawala wa sheria, usawa wa watu wote mbele ya sheria ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu na kwamba, uhuru wa kidini hauna budi kutambuliwa na kudumishwa na wote bila ubaguzi!

Tatu; waamini wa dini mbali mbali waheshimiane na kushirikiana na Serikali zao; kila taasisi ikitambua dhamana na majukumu yake ndani ya jamii, ili kutekeleza yote haya bila kuingiliana wala kubezana kwa misingi yoyote ile! Nne, viongozi wa kidini watambue kwamba, wanao wajibu wa kukemea na kulaani matumizi mabaya ya dini na mambo yote yanayochochea kinzani, mipasuko na mashambulizi ya kigaidi ambayo yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao sehemu mbali mbali za dunia. Tano, waamini wa dini mbali mbali waendelee kujikita katika majadiliano ya kidini ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, daima wakipania kutoa huduma makini kwa familia ya binadamu! Kuwepo na tafsiri sahihi ya vitabu vitakatifu, ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani!

Sita, Kardinali Parolin anasema, kuna haja ya kuwepo na elimu ya dini, ili kuzuia uwezekano wa baadhi ya waamini kujikuta wakitumbukia katika misimamo mikali ya kidini kutokana na tafsiri potofu ya vitabu vitakatifu. Waamini wafundishwe kuthamini tofauti msingi za kiimani na kwamba, huu ni utajiri unaopaswa kuheshimiwa na wala si sababu ya chochoko, kinzani na vita! Saba, inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi wafanyabiashara haramu wa silaha wanaotumia mianya ya kinzani na mipasuko ya kidini kama chambo cha kujitafutia faida kubwa na matokeo yake ni mauaji kwa misingi ya kidini.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, ikiwa kama kuna uzalishaji, usambazaji hatimaye, kutakuwepo na matumizi ya silaha hizi. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, amewashukuru na kuwapongeza  wadau mbali mbali kwa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu zinazofumbatwa katika uhuru wa kidini. Juhudi hizi zisaidie kuondoa mateso na mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia, wanaoteseka kutokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Ni watu wanaodhulumiwa na kunyanyasika na hata kukumbana na kifodini au ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko! Ni matumaini ya Kanisa kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuweka msingi thabiti ambamo watu wanaweza kuishi kwa kuzingatia misingi ya haki, amani na maridhiano kati yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.