2018-06-26 09:41:00

Gavana Peter Cosgrove akutana na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 25 Juni 2018 amekutana na kuzungumza na Bwana Peter Cosgrove, Gavana mkuu wa Jumuiya ya Madola nchini Australia, ambaye baadaye pia, alipata bahati ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, aliyekuwa amembatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake; wamegusia kwa namna ya pekee kuhusu changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji katika ngazi ya kitaifa na kimataifa pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Viongozi hawa wamepongeza kwa namna ya pekee, mchango unaotolewa na Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Australia. Wamegusia pia umuhimu wa Jamii kujikita katika ulinzi wa watoto wadogo, dhamana inayopaswa kutekelezwa na wadau mbali mbali katika mazingira ya Kanisa nchini humo. Baadaye, viongozi hawa wamejikita zaidi katika masuala ya kijamii nchini Australia, amani na utulivu katika Ukanda wa Bahari ya Pacific na Asia katika ujumla wake!

Na Padre Richard. A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.