2018-06-25 14:30:00

Yaliyojiri S'wanga wakati wa kuwekwa wakfu na kusimikwa Askofu Urassa


Askofu mahalia anayo dhamana ya kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wote, kwa kutambua kwamba, kimsingi yeye ni mtu wa Mungu, aliyeteuliwa kati ya watu kwa ajili ya huduma, ili kuhakikisha kwamba, anakuza na kudumisha Ibada na Uchaji wa Mungu, mambo msingi katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa kwa damu Azizi ya Kristo Yesu.

Utume huu, umwezeshe Askofu kuwa kiongozi mkarimu na mnyenyekevu, akitambua kwamba, Kristo Yesu ndiye anayewaita waja wake na kuwaweka wakfu ili kuendeleza kazi ya ukombozi! Wakleri wanatambua kwamba, wito ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si kwa ajili ya mastahili yao binafsi, kumbe, wanapaswa kuwa ni watu wa shukrani, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, chemchemi ya amana za maisha ya kiroho na kiutu!

Wito huu ni mwendelezo wa historia ya huruma na mapendo ambayo inapata chimbuko lake katika Daraja Takatifu na kwamba, Mama Kanisa anayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, analea na kupalilia miito mitakatifu ili iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani: toba na wongofu wa ndani, kama sehemu ya mchakato wa utume, umisionari na uinjilishaji unaopaswa kutekelezwa na Wakristo katika ujumla wao kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Kristo Yesu ndiye Kuhani mkuu na kwamba, Uaskofu ni utimilifu wa Daraja Takatifu, tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia!

Hii ndiyo dhamana na utume ambao uko mbele ya Askofu Beatus Christian Urassa wa Jimbo Katoliki Sumbawanga, baada ya kuwekwa wakfu ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Ibada hii imeongozwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, wakati Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Kuzaliwa Yohane Mbatizaji. Ibada hii imehudhuriwa na Askofu mkuu Marek Solczynski, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Maaskofu pamoja na familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania.

Katika mahubiri yake, Kardinali Polycarp Pengo, ameitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kujenga na kudumisha: umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa; utambulisho makini wa watanzania kwa kuondokana na ukabila usiokuwa na mashiko wala mvuto, kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote! Amewakumbusha waamini kwamba, umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini Tanzania unafumbatwa katika Damu Azizi ya Kristo Yesu na wala si makabila ya Maaskofu wa Majimbo mahalia.

Kardinali Pengo amewataka Maaskofu kukazia, kutangaza na kushuhudia kwa vitendo umoja wa kitaifa na wala si ukabila. Kwa Askofu Beatus Urassa kuwa mchaga kamwe hakumzuii kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Sumbawanga kama njia ya kuwaletea ukombozi. Katika ulimwengu wa utandwazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kuna haja ya watu kuwa na utambulisho wao makini na wala hakuna sababu ya msingi kwa Askofu Urassa kuficha utambulisho wake kama mchaga! Kardinali Pengo anakaza kusema, watu wamekombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu, ndiyo inayowapatia mamlaka na nguvu ya kuwa Maaskofu, ndugu na wana wa Mungu.

Kwa kusoma alama za nyakati, huku akiwa na jicho la kinabii, Kardinali Pengo amekaza kusema, katika uongozi wa Tanzania, kuna umuhimu wa Maaskofu kukazia umoja na mshikamano wa waamini, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo. Amekazia umoja wa watanzania na umoja wa Tanzania kama nchi na kamwe ukabila usivunje umoja wa kitaifa. Kardinali Pengo amemhakikishia Askofu Beatus Christian Urassa sala kama ilivyo hata kwa Maaskofu wengine, waliohudhuria sherehe ya kuwekwa kwake wakfu na hatimaye, kusimikwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Amemtaka kutunza umoja wa watanzania na umoja wa Tanzania!

Askofu mkuu Marek Solczynski, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, katika hotuba yake kwenye sherehe hii, ameitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, kwani migawanyiko na mipasuko ya aina yoyote ile, inalitendea Kanisa la Kristo! Amesikitika kusema kwamba, madhara ya ukabila ni makubwa mno katika maisha na utume wa Kanisa na wala hili si jambo ambalo linapaswa kuendekezwa, kwani hata Kristo Yesu mwenyewe hapendi mambo haya kwani yanalikwamisha Kanisa. Askofu mkuu Marek Solczynski amewashukuru waamini wa Jimbo Katoliki Sumbawanga kwa mapokezi makubwa na idadi kubwa ya waamini waliohudhuria katika Ibada ya Misa Takatifu ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu Beatus Urassa kuwa kiongozi mkuu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Shamra shamra zilizokuwepo tangu wakati wa kumkaribisha Askofu Urassa hadi kuwekwa kwake wakfu ni mwanzo mzuri wa maisha na utume wa Askofu Beatus Urassa.

Askofu mstaafu Damian Kyaruzi ambaye kwa muda wa miaka 21 ameliongoza Jimbo Katoliki la Sumbawanga na sasa anajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, anapenda kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake katika maisha yake. Ameishukuru familia ya Mungu Jimbo Katoliki Sumbawanga kwa umoja, na ushirikiano waliomwonesha wakati wa maisha na utume wake kama mchungaji mkuu wa Jimbo Katoliki Sumbawanga. Ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano na mshikamano katika kuwahudumia watu wa Mungu nchini Tanzania. Amemwomba Askofu Beatus Urassa ambaye pia anajulikana kama Msafiri, kutambua kwamba, sasa amefika! Jimbo Katoliki la Sumbawanga ndio makazi yake mapya!

Kwa upande wake, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais mstaafu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, amemshukuru na kumpongeza Askofu Damian Kyaruzi kwa mchango wake makini katika maisha na utume wa Kanisa la Tanzania katika kipindi cha miaka 21 ya utume wake kama Askofu. Baraza la Maaskofu linapenda kumkaribisha Askofu Beatus Urassa katika urika wa Maaskofu wa Tanzania na kwamba, wanaahidi kumpatia ushirikiano pamoja na kumsindikiza kwa sala katika maisha na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, Jimbo Katoliki Sumbawanga.

Askofu Beatus Urassa wa Jimbo Katoliki Sumbawanga, ametumia fursa hii kuwashukuru Mungu na wazazi wake kwa malezi makini; Shirika pamoja na wageni mbali mbali waliokuja kutoka Ujerumani na Italia. Lakini, ametoa shukrani za dhati kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki Sumbawanga kwa mapokezi ya kishindo na mahudhurio makubwa katika Ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwake kama Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Amemwomba Askofu mstaafu Damian Kyaruzi aendelee kumwongoza katika maisha na utume wake mpya na kwamba, yuko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Sumbawanga.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mh. William Vangimembe Lukuvi, kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, amelishukuru Kanisa kwa mchango wake katika kukuza na kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania. Amelipongeza Kanisa kwani limekuwa mdau mkuu wa maendeleo endelevu na huduma kwa watanzania kwa takbribani miaka 150 tangu wamisionari wa kwanza walipoingia nchini Tanzania. Serikali inatambua mchango huu na kwamba, itaendelea kutoa ushirikiano na Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote!

Jimbo Katoliki la Sumbawanga lilianzishwa kunako tarehe 10 Mei 1946 na Hayati Askofu James Holmes Siedle, akawa Askofu wake wa kwanza na kubahatika kuliongoza Jimbo kuanzia mwaka  1946 hadi mwaka 1958. Akafuatia Askofu Charles Msakila, aliyeongoza Jimbo kuanzia mwaka 1958 hadi mwaka 1994. Kuanzia mwaka 1997 hadi tarehe 23 Juni 2018, Jimbo limekuwa chini ya uongozi wa Askofu mstaafu Damian Kyaruzi. Kuanzia sasa Jimbo Katoliki Sumbawanga linaongozwa na Askofu Beatus Christian Urassa.

Itakumbukwa kwamba, Askofu Beatus Christian Urassa alizaliwa tarehe 2 Agosti 1965 huko Keni, Mashati Rombo, Jimbo Katoliki la Moshi. Alipata majiundo na masomo yake ya kifalsafa kutoka Seminari kuu ya Shirika la Mitume wa Yesu, Lang’ata, Jijini Nairobi nchini Kenya. Baadaye akajiunga na Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu na kupelekwa kuendelea na masomo yake ya kitaalimungu kwenye Seminari kuu ya Mtakatifu Charles Lwanga, maarufu kama Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania.

Baadaye, alitumwa mjini Roma kuendelea na masomo ya taalimungu maisha ya kiroho kwenye Taasisi ya Kipapa ya Teresianum, iliyoko Roma na hapo akajipatia shahada ya uzamivu katika maisha ya kiroho! Tarehe 12 Julai 1997, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tangu wakati huo, kama Padre na Mtawa, amefanya kazi mbali mbali. Kati ya mwaka 1997-1998 alikuwa ni Katibu mkuu wa Halmashauri kuu ya Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu (ALCP / OSS) yenye Makao makuu yake Jimbo Katoliki la Moshi. Kati ya mwaka 1998-1999, alikuwa ni Paroko usu, Parokia ya Mwananyamala, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kati ya mwaka 1999-2000 akateuliwa kuwa ni mlezi katika nyumba yao ya malezi, iliyoko Jimbo Katoliki la Morogoro. Kati ya mwaka 2000 hadi mwaka 2003 akatumwa Roma kuendelea na masomo ya juu na huko akajipatia Shahada ya uzamivu. Kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2015 amekuwa ni Padre mkuu wa Kanda Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu (ALCP / OSS).

Shukrani za pekee zinamwendea Askofu Flavian Matindi Kassala, wa Jimbo Katoliki Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa utayari wake wa kufanya mahojiano kwa njia ya simu na Vatican News kutoka Mbeya, akiwa njiani kurejea kutoka Jimboni Sumbawanga, walikohudhuria: Mapokezi na Ibada ya Kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Beatus Christian Urassa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.