2018-06-25 14:30:00

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lapata sululu mpya za uongozi


Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mpanda, amechaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki Geita, amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Mheshimiwa Padre Charles Kitima kutoka Jimbo Katoliki la Singida ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Padre Kitima, amewahi kuwa Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino cha Tanzania, SAUT, Mkuu wa Tawi la SAUT, Mtwara na Mkuu wa Tawi la SAUT, Dar es Salaam.

“Sululu mpya" ya uongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, yatakayokuwepo madarakani kwa muda wa miaka mitatu kuanzia sasa, yametangazwa rasmi na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa aliyemaliza muda wake, baada ya Ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu Beatus Christian Urassa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Sumbawanga, Ibada ambayo imehudhuriwa na umati mkubwa wa watu wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki Sumbawanga na kufuatiliwa kwa makini kwenye vyombo vya mawasiliano, kutokana na umuhimu wa tukio hili katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Wachunguzi wa masuala ya uongozi wanakaza kusema, hii ni “Timu ya Ushindi” iliyokiwezesha Chuo Kikuu cha SAUT, kupata mafanikio makubwa katika kipindi cha muda mfupi wa uhai wake! Hii ni Timu ya Maaskofu vijana wanaotambua changamoto za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.