2018-06-23 07:40:00

Sherehe ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji: Shuhuda wa Mwanakondoo!


Utangulizi: Yesu anasema “ Nami nawaambia: katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kliko Yohane Mbatizaji; lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye” (Lk. 7:28). Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tarehe 24 Juni Kanisa huadhimisha sherehe ya kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji. Kwa kawaida Kanisa huwaenzi watakatifu katika liturujia siku ya kumbukumbu ya vifo vyao. Lakini kwa Yohane Mbatizaji, Bikira Maria na Bwana wetu Yesu Kristo tu huenziwa pia siku za kuzaliwa kwao, na hii ni kwa sababu ya nafasi walizonazo katika historia ya ukombozi wa mwanadamu. Leo tunaadhimisha kuzaliwa kwa mtangulizi wa mkombozi ambaye kuzaliwa kwake kuliashiria kuwa sasa ukombozi umefika.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Is. 49:1-6) Nabii anaalika visiwa kusikiliza.Visiwa hivi ni akina nani? Kwa kufuata kitabu cha Mwanzo 10:5, visiwa au mataifa ya pwani ni watu wa mataifa, wasio wayahudi. Na hawa wanaalikwa kusikiliza nini? Wanaalikwa kusikiliza habari njema ya mkombozi na ukombozi wao. Mkombozi huyu anapata mamlaka yake kutoka mbinguni. Ni Mungu anayemteua, anamtenga yaani anamweka wakfu na anamwaandaa kwa kazi hiyo anayomwitia. Ni mkombozi anayeitwa tangu akiwa tumboni mwa mama yake kwa sababu Mungu daima huwaandaa watu wake mapema, kabla wao wenyewe hawajapata ufahamu na kabla hata wale anaotumwa kwao hawajajua. Mkombozi huyu atapata faraja yake daima kwa Bwana. Hatataabika bure wala hatajichosha bure kama akifanya  yote yampasayo akiwa na Bwana.

Huu ni unabii wa kimasiha ambao hauzungumzii tu ukombozi dhidi ya utumwa wa kisiasa bali dhidi ya utumwa wa dhambi. Na hauwagusi Wayahudi pekee na kuwabagua watu wa mataifa. Ndio maana unaelekezwa kwa visiwa, yaani watu wa mataifa ukitabiri pia kuwa wale ambao mkombozi atawafikia kwanza, wayahudi, hawatampokea kirahisi na hivi atawageukia mataifa. Kumbe, ni unabii unaomwelekea moja kwa moja Kristo; masiya na mkombozi, aliyewekwa wakfu na kutumwa kuwakomboa watu wote kwa kumwaga damu yake Msalabani.

Somo la pili (Mate. 13:22-26) linaelezwa ushuhuda wa Yohane Mbatizaji. Huyu ndiye mtangulizi wa Masiha ili ujio wake usiwe kama kitu cha ghafla ambacho hakikutegemewa kwa watu wake. Amekuwa mtangulizi wa masiha kwanza kwa kumtengenezea njia. Yohane Mbatizaji amemtengenezea masiha njia kwa kuhubiri ubatizo wa toba kwa wote. Aliwaonesha dhambi zao, akawaonya juu ya adhabu inayowangoja na kuwaonesha matunda ya toba watakayoifanya. Pili amekuwa mtangulizi wa masiha kwa kumtambulisha kwa watu. Masiha alipokuja, Yohane Mbatizaji mwenyewe  alikiri “mimi siye, lakini angalieni anakuja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake”.

Injili (Lk. 1:57-66,80) inaonesha tukio la kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, kupewa jina na baba yake Zakaria kurejeshewa sauti. Tukio la kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, kama kuzaliwa kwa mtoto katika familia, lilileta furaha. Lakini kwa upande wake ilikuwa furaha kubwa zaidi kwa sababu alizaliwa kwa mama aliyekuwa tasa. Akapewa jina Yohane. Baba yake, Zakaria, ambaye kwa kutoamini maneno ya malaika akawa bubu, anarudishiwa sauti baada ya mtoto kupewa jina Yohane.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji tunayo mengi sana ya kutafakari na kujifunza: maisha yake ya kujikatalia, bidii yake ya kujitenga na anasa na malimwengu, kufundisha na kuishi toba, kumshuhudia Kristo na kusimamia ukweli bila kuyumbayumba kitu  ambacho kilimsababisha kuwekwa gerezani na hatimaye kuuwawa kwa kukatwa kichwa kwa amri ya Herode. Leo, lakini, Kanisa linapenda tutafakari zaidi kuzaliwa kwake. Kama tulivyokwisha eleza hapo awali, kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji kuliashiria sasa kutimia kwa ujio wa mkombozi. Manabii wa Agano la Kale waliagua kwa miaka mingi sana ujio wa mkombozi Masiha. Ndio pia unabii tuliousikia katika somo la kwanza. Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji kunakuwa ni ujio wa Nabii wa mwisho  ambaye yeye haendelei kutoa unabii juu ya Masiha bali anawaambia watu kuwa Yule aliyetabiriwa sasa amefika; mpokeeni.

Katika injili kadiri ya Luka, habari za kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji zinawekwa sambaba na zile za kuzaliwa kwa Yesu. Kupashwa habari kuzaliwa Yohane Mbatizaji kunafuatiwa na kupashwa habari kuzaliwa Yesu; Mama Bikira Maria anapokwenda kumtembelea Elizabeti, mama wa Yohane Mbatizaji, Yohane akiwa bado tumboni mwa mamaye anamtambua Yesu na anaruka kwa furaha. Na hatimaye habari ya kuzaliwa kwa Yohane inafuatiwa pia na habari ya kuzaliwa kwa Yesu. Hapa tunaona ukaribu ambao Yohane Mbatizaji alikuwa nao kwa Yesu. Ni ukaribu huu umeupa nguvu utume wake, ni ukaribu huu umemfanya akatoa ushuhuda kwa Yesu na ukaribu huu umefanya Yohane Mbatizaji kuwa mkuu namna hii. Anatuambia mtakatifu Thomas wa Akwino kuwa “kadiri kitu kinavyokuwa karibu na chanzo, ndivyo kinavyonufaika na utendaji wa chanzo hicho”. Aliye karibu na waridi atanukia, aliye karibu na mwanga atang’aa na aliye karibu na joto atapata joto.

Leo tunaalikwa kutafakari ukaribu wetu na Kristo chanzo cha uzima wetu, chanzo cha utume wetu, nguvu na msaada wetu. Hapo ndipo ulipo ukuu wetu na hapo ndipo tunaona fahari ya maisha sisi kama wakristo. Tafakari hii inakuja wakati ambapo ulimwengu unaanza kumtoa Kristo katikati ya maisha na polepole kumsogeza pembezoni. Na kwa bahati mbaya sisi wenyewe wakristo au kwa kujua au kwa kutokujua tunayatenda yayo hayo. Tunaona maadili ya kikristo yanawekwa sambamba na mitindo mingine ya maisha ambapo ni mtu mwenyewe anachagua chini ya mwamvuli wa uhuru usioingiliwa. Tunaona pia urahisishaji wa imani katika mafundisho na hata katika utatuzi wa changamoto za kiimani katika maisha na mambo mengine kama hayo. Tunaalikwa leo turudi kwa Kristo. Tujenge ukaribu naye katika mipango, katika kazi zetu, katika kuiishi imani yetu na daima maishani. Ndipo ulipo ukuu wetu na thamani ya maisha yetu.

Padre William Bahitwa.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.