Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Sherehe ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji: Nabii wa Aliye Juu!

Mtakatifu Yohane Mbatizaji ni Nabii wa Aliye Juu

22/06/2018 07:44

Mpendwa Msikilizaji wa Vatican News! Mama Kanisa katika dominika ya kumi na mbili ya Mwaka B anatualika kuadhimisha Sherehe ya kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, mtangulizi wa Kristo. Jina Yohane lina asili yake ni kutoka katika lugha ya Kiebrania “Yehohanan” ambalo maana yake ni Mungu ni mpendelevu. Upendelevu wake huo hujifunua katika huruma yake ambayo anatumiminia kwa njia ya Yesu Kristo. Hii humaanisha imani ya watu juu ya neema za Mungu kwa watu, tendo ambalo linaufunua upendo wake wa milele. Mama Kanisa anapoadhimisha sherehe ya kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji anatualika kuitafakari huruma yake aliyoifunua kwa njia ya Yeye ambaye Yohane Mbatizaji alikuwa mtangulizi wake, yaani Kristo Bwana wetu.

Wimbo wa Zakaria unaionesha kazi yake adhimu. Sehemu ya kwanza ya wimbo huo, ambao aliuimba baada ya kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji ni sifa kwa Mungu kwa matendo yake makuu ya ukombozi wa wanadamu. Mungu “atatujalia sisi, tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu” (Lk 1:74). Sehemu ya pili inaimbwa kwa heshima ya mtoto aliyezaliwa, yaani Yohane na uaguzi wa utume wake wa kuwa “nabii wa Aliye juu” (Lk 1:76). Yohane aliaguliwa kuwa atakuwa mtangazaji wa huruma ya Mungu ambayo inajifunua katika huruma ya Mungu kwa wadhambi. Uthibitisho wa huruma hiyo ya Mungu ni ujio wa Maisha. Kwa maana “kwa njia ya rehema za Mungu wetu, mwangaza utokao juu umetufikia, kuwaangazia wakaao katika giza na uvuli wa mauti, na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani” (Lk 1:78 – 79). Jua la haki ambalo linatujia kutoka juu litauchanjilia mbali uzushi wote na ukengemfu wa kimaadili ambao unaletwa na giza la kifo au dhambi na kuwafunulia wanadamu imani ya kweli na kuwapatia amani.

Injili ya sherehe hii inatuonesha tukio la kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji. Wazazi wake Elisabeti na Zakaria walikuwa wazee na kibailojia walikwishapita umri wa kujaliwa uzao. Ndiyo maana majirani na jamaa zake waliungana nao na kuona kuwa “Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye”. Mkono wa Mungu na upendeleo wake umeanza kujionesha tangu namna yake ya kuzaliwa. Ilikuwa ni namna ya kimiujiza na iliyohitaji kuwa na imani kuu kwa Mungu. Hivyo tunaona kwa nafasi ya kwanza kwamba imani inahitajika ili kuupata upendeleo wa Mungu, yaani kupata utendaji wa Mungu ndani wetu. Yeye ndiye muweza wa yote. Tendo la upendeleo wa Mungu katika utendaji ambao haukutegemewa huongeza furaha. Mwanadamu katika mipaka yake ya kiutendaji hujazwa furaha pale rehema za Mungu zinapomjia.

Yohane anazaliwa katika mazingira ya Kiyahudi na hivyo taratibu zote za kimila na kidini zinafuatwa sawasawa. Taratibu hizi zilihusisha kutahiriwa na kupewa jina. Hizi ni taratibu ambazo zilimtambulisha na kumsajili rasmi mtoto anayezaliwa katika jamii ya kiyahudi. Kutahiriwa kwake hakukuwa na shida yoyote ila tendo la kupewa jina linatuonesha tena mazingira yasiyo ya kawaida ya kuzaliwa kwa mtoto huyu. Hapa tunaona pia hitajiko la kutoka katika mazingira na mawazo ya kibinadamu ili kupokea utendaji wa Mungu na upendeleo wake kwetu. Ustaajabisho huu wa utendaji wa Mungu unajidhihirisha kwa namna Zakaria na mke wake Elisabeti walivyosema jina moja. Pamoja na kwamba Zakaria alifanywa bubu wakati wa kupokea taarifa ya kuzaliwa kwa Yohane kutoka kwa Malaika lakini alipoomba ubao ili aandike alisema: “Jina lake ni Yohane”, sawa na pendekezo la mke wake. Haikufuata utaratibu wa kuwa na majina ya ukoo kwa sababu ilikuwa ni kazi ya Mungu kwa ajili ya ukombozi wetu.

Utangulizi wa sherehe ya leo unamtaja Yohane kuwa “ndiye peke yake kati ya manabii aliye mwonesha mwanakondoo aliye Mkombozi”. Manabii wengine wote waliagua ujio wa Masiha na kuwasisitiza watu kubadilisha mienendo yako kwa ajili ya kumpokea Masiha. Namna ambavyo anautimiza wajibu huu unatupatia funzo kubwa katika wajibu wetu kama Wakristo. Yohane alisema wazi wakati akimtambulisha Kristo kuwa yeye siye Kristo; zaidi alipomwona Kristo mbele yake alimtambulisha kama “Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu” (Yoh 1:29) na mwishoni kwa unyenyekevu mkubwa alisema: “Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua”(Yoh 3:30). Haiba hii ilimfanya Kristo kumtaja kama mkuu kuliko watu wote waliozaliwa na mwanamke (Rej Lk 7:28).

Ukuu wa Yohane hauonekani katika aina ya utume wake bali ni namna ambavyo aliutekeleza utume wake. Kristo alisema: “Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye zaidi ya nabii” (Lk 7:26). Si kumtazama tu kama nabii bali kile ambacho kimemfanya kuwa nabii wa kweli na mkuu kuliko wote. Kitu hicho kinaelezewa na Kristo kwa kusema: “aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye” (Lk 7:28). Hapa tunaona tunu ya unyenyekevu ambayo imemtamalakisha Yohane na kuonekana mkuu kuliko wote. Kwa hakika Yohane alionesha hilo. Pamoja na kwamba watu walifikiri kuwa yeye ndiye masiha hakulevywa na sifa hizo bali alijiona kuwa ni kiumbe anayehitaji huruma yake. Wakati wa ubatizo wa toba amelidhihirisha hili kwa namna njema kabisa kama tuonavyo katika somo la pili aliposema: “Mwadhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake”.

Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji kunaunganishwa na kuzaliwa kwa Kristo kunakotokea miezi sita baadaye. Maneno ya Yohane Mbatizaje mwenyewe anayesema “basi hii furaha yangu imetimia, Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua” (Yoh 3:30) yanaonekana kupata mwanga zaidi kwa kadiri ya maelezo ya wataalamu mbalimbali wa maandiko matakatifu. Hili linaelezewa katika majira yanayokuwepo wakati wa kuzaliwa kwa Kristo na Yohane Mbatizaji kwa eneo la kijiografia ya mashariki ya kati. Yohane Mbatizaji alizaliwa mwezi Juni wakati ambapo kimajira mchana au wakati wa nuru ulianza kupungua. Inapofikia kilele cha giza, yaani usiku unapokuwa mrefu zaidi ya mchana wakati wa mwezi wa Desemba ndipo Kristo, Nuru ya ulimwengu anapozaliwa na toka kipindi hicho kipindi cha mchana kinaanza kuongezeka tena. Yaani Kristo jua la haki anaanza kuongezeka na kuwaangazia watu wote huruma ya Mungu.

Kristo anatuhitaji mimi na wewe kuendelea kuwa ufunuo wake. Yeye ndiye anayenenwa katika somo la kwanza kuwa “nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia”. Katika jamii ya mwanadamu wa leo ambaye anasongwa na shida nyingi zinazomwonesha giza nene; mwanadamu ambaye amekengeuka na kuto kupata huruma ya Mungu na msamaha wa dhambi, kiu ya kuiona nuru ya Mungu hakika ipo. Nuru hiyo ambayo ni Kristo imekwisha izukia dunia. Kwa njia ya Kanisa na kazi zake, ambao ni mimi na wewe katika ushuhuda wa imani yetu, tunapaswa kuwa nuru hiyo kwa watu wengine. Yohane Mbatizaji ni kielelezo chetu cha kuwa watangulizi na watengenezaji wa njia kwa ajili ya nuru hiyo. Ni lazima tujiweke katika hali ya kumfanya Yeye aongezeke na sisi tupungue. Ukuu na umaarufu wetu uonekane katika ustawi na uenezaji wa kazi yake ya ukombozi.

Mungu wetu ametuumba na anayo makusudi na kila mmoja wetu. Nafasi zetu mbalimbali tulizonazo katika jamii zinapaswa kuelekezwa katika utimilifu wa makusudi ya Mungu. Hapo huonekana ukuu wetu katika makuu ya Mungu. Matendo ya kujitwalia nafasi ya Mungu na kuweka misukumo yetu ya kibinadamu huongeza taabu na mateso kwa watu na kuzifungia baraka za Mungu. Matendo maovu kama rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, unyonyaji, upendeleo wa kikabila au dini na mengineyo mengi ni dalili za kutokuwa tayari kumfanya Kristo aongezeke nasi kupungua. Tunaendelea kusema “ufalme wake uje, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni” lakini katika uhalisia tunataka tuendelee kutawala na yale tuyatakayo yaendelee kufanyika. Tunapoadhimisha sherehe hii tumpokee Yohane Mbatizaji kama kielelezo chetu ili kwa utume wetu watu wote waendelee kuuonja upendeleo wa Mungu.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha.

Vatican News!

 

 

22/06/2018 07:44