2018-06-22 16:59:00

Papa Francisko: Upendo wa Kristo unawabidisha: Kujipyaisha & kutangaza


Shirika la Wamisionari wa Neno Takatifu “Society of the Divine Word”, SVD, linalotekeleza dhamana na utume wake katika nchi 46 duniani, kuanzia tarehe 17 Juni hadi 14 Julai 2018 linaadhimisha Mkutano wake Mkuu wa 18 unaowashirikisha wajumbe 151, wanaowawakilisha wanashirika 6,000 waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Upendo wa Kristo unatubidisha” : Kwa kujisimika katika Neno na kuwajibika katika Utume wake”. Huu ni muda muafaka wa kusali, kutafakari na kushirikishana mang’amuzi, changamoto na vipaumbele kwa siku za usoni.

Itakumbukwa kwamba, Shirika hili lilianzishwa kunako mwaka 1875 na Mtakatifu Anorld Jannsen huko nchini Uholanzi. Hili ni Shirika ambalo linajikita zaidi katika sekta ya elimu, Utume wa Biblia, Mawasiliano; haki na amani; utunzaji bora wa mazingira na maendeleo endelevu ya binadamu! Babha Mtakatifu Francisko, akizungumza na wajumbe wa Mkutano mkuu wa Shirika, Ijumaa, tarehe 22 Juni 2018 amesema kwamba, maadhimisho ya Mkutano mkuu ni kipindi cha neema kwa familia ya Mungu, Shirika la Wamisionari wa Neno Takatifu, Kanisa na dunia katika ujumla wake kama alivyozoea kusema, Mtakatifu Anorld Jannsen.

Upendo wa Kristo anakaza kusema Baba Mtakatifu, unawabidisha kupyaisha maisha yao binafsi pamoja na maisha ya kijumuiya, ili kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Injili, daima kwa kujikita katika mizizi, tayari kufanya maboresho makubwa katika maisha na utume wa Shirika sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu akiwa na mawazo haya, amependa kukita hotuba katika mambo makuu matatu: Imani, Kutangaza pamoja na Ndugu! Wanashirika wanapaswa kutumainia huruma ya Mungu na kuachilia mikononi mwake maisha yao ya Kikristo na wakfu. Upendo wa Mungu unafumbatwa katika huruma yake, kiasi hata cha kuthubutu kutekeleza dhamana na wajibu wao hata katika mazingira magumu.

Ujasiri na imani mbele ya Mungu inawafanya kuwa wazi na kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, inayowakirimia watu wengi furaha katika maisha yao. Imani inapaswa kupyaishwa kila kukicha kwa njia ya sala, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na kuendelea kuwa wazi katika kufanya mang’amuzi mbali mbali katika maisha, wito na utume wao, daima wakijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao!

Baba Mtakatifu anasema, utangazaji na ushuhuda wa Neno la Mungu ni kiini cha karama ya Shirika la Wamisionari wa Neno Takatifu kwa watu wa nyakati zote na kila mahali sanjari na kuhakikisha kwamba, wanatumia kila nyenzo inayopatikana mbele yao, ili kuunda umoja wa Jumuiya ya wafuasi na wamisionari kati yao na Kanisa zima. Kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu ni moto wa kuotea mbali kwa wamisionari hawa, amana, utajiri na urithi wa Shirika hili tangu mwanzo, changamoto pevu iliyoko mbele yao! Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, wao ni wamisionari wanaotumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema kwa watu ambao bado hawajapata nafasi ya kusikiliza Neno la Mungu; kumbe, Neno la Mungu linapaswa kuwa ni moto unaowaka ndani ya mioyo yao, ili kuwawezesha kuwa wamisionari wa kweli pasi na mawaa, kwa kujichimbia katika Neno, ililiweze kuwatakasa na kuwakatifuza!

Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, wao si kisiwa, bali ni sehemu ya Kanisa, familia ya Mungu na wanao ndugu zao katika Kristo wanaotembea kwa pamoja katika maisha na wito wa kitawa! Wamisionari hawa wajitahidi kuonesha utambulisho wao hata kama wako katika makundi ya watu! Wawe waaminifu katika utofauti, kwa kuheshimiana na kupendana, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha uinjilishaji. Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake, unahitaji shuhuda wa upendo wa kidugu licha ya tofauti msingi na tamaduni mbali mbali zinazowaunganisha, lakini wote wanajisikia kuwa ni sehemu ya familia ya Mungu; inayowawezesha kushirikishana imani na karama kwa ajili ya huduma kwa jirani.

Baba Mtakatifu anawapatia changamoto ya kutoka, ilikuwaendea wale wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii; wanaodhalilishwa na kunyanyaswa haki zao msingi, kwani hata wao, wanahitaji kuonja uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao. Wamisionari hawa wanatakiwa kusikiliza na kujibu kilio cha watu wenye njaa ya chakula na haki, kwa kuwawezesha katika maendeleo endelevu ya binadamu pamoja na maisha bora zaidi. Wawe ni faraja na vyombo vya matumaini kwa wale wote wanaoteseka! Huu ndio ushauri ambao Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwakirimia, ili kuongoza hatua zao za kimisionari!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.