2018-06-22 10:00:00

Papa Francisko: Sala ya Baba Yetu: Baba! Chakula na Msamaha wa kweli!


Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Alois Gongaza, Myesuit, tarehe 21 Juni 2018, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya familia ya Mungu ndani na nje ya Uswiss kama sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa Sala ya Baba Yetu kwa kujikita katika maneno yafuatayo: Baba! Chakula Msamaha!

Baba Yetu ndio ufunguo wa Sala kuu aliyofundisha Yesu, inayoweza kupenya katika moyo wa Mwenyezi Mungu. Wakristo wanasali na kumwomba Mwenyezi Mungu ambaye ni Baba yao aliye mbinguni! Mungu ni asili na chemchemi ya maisha na kwamba, binadamu ni watoto wake wapendwa wanaotamani kuona Ufalme wa Mungu ukisimikwa hapa duniani na mapenzi yake yakitendeka duniani kama mbinguni. Huu ni mwelekeo wa maisha ya kiroho unaopaswa kufuatwa na waamini wote.

Alama ya Msalaba ni kiini cha maisha ya Kikristo yanayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa katika jamii, ili kuwasha nyoyo kwa moto wa upendo unaowaunganisha wote, kwa kutambua kwamba,  kwa hakika wanapendwa wote kama familia moja. Huyu ni Baba wa wote na wala hakuna mtoto anayepaswa kujisikia kukosa upendo wa kibaba, changamoto ya kusimama kidete kulinda na kutetea udugu wa kifamilia sanjari na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kusimama kidete kuteteta utu na heshima ya binadamu. Mwenyezi Mungu anataka watoto wake kupendana wao kwa wao kama ndugu!

Kristo Yesu anawataka waja wake kuomba chakula cha kila siku, ili kuweza kuishi, kupata mambo msingi pamoja na afya bora; fursa za kazi pamoja na kupambana na baa la njaa linaloendelea kuwatesa na kuwanyanyasa watu wengi duniani! Hapa Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa na matumizi mazuri ya chakula, kwani chakula ni sehemu ya haki msingi za binadamu! Watu wote wanapaswa kupata chakula na lishe bora! Hii ni changamoto pia ya kuishi maisha ya kawaida pasi na kutaka makuu! Changamoto mbali mbali za maisha zinawafanya watu wengi leo hii kuishi kana kwamba, wamelewa na malimwengu, kumbe kuna haja ya kufanya maamuzi na kuwa na mambo kiasi katika maisha, kama alivyotenda wakati wake, Mtakatifu Alois Gonzaga, ambaye, Kanisa linamkumbuka, kila mwaka ifikapo tarehe 21 Juni. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa na chakula cha kawaida ili waweze kupata ujasiri wa ukimya na sala, chachu muhimu sana ya maisha ya kiutu!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema, Kristo Yesu ni mkate wa uzima, chanzo na kilele cha maisha ya waamini pasi yeye, maisha hayana maana! Lakini inasikitisha sana kuona kwamba, adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu linatendeka kwa mazoea, kiasi hata cha kushindwa kumfanya Kristo Yesu kuwa ni chakula chao cha kila siku na kiini cha maisha yao na matokeo yote yanakuwa batili na utupu! Kwa kuomba chakula cha kila siku kutoka kwa Mwenyezi Mungu, waamini wawe na ujasiri kumwomba Mwenyezi Mungu kuwapatia maisha ya kawaida, upendo na huduma kwa jirani zao na kwamba, Kristo Yesu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwani Yeye yote katika yote!

Kusamehe ni mchakato mgumu sana katika maisha ya waamini, lakini wanapaswa kutambua kwamba, kwanza kabisa wao wamesamehewa na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao, wawe na ujasiri wa kuwasamehe jirani zao na kwamba, msamaha ni sehemu muhimu sana ya Sala ya Baba Yetu. Mwenyezi Mungu anawaondolea na kuwasamehe dhambi zao, lakini kwa sharti moja kwamba hata wao wawe na ujasiri wa kusamehe kama wanavyosamehewa.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuchunguza dhamiri zao ili kuweza kuondokana na mambo yale yanawakwamisha kiasi hata cha kushindwa kutoa msamaha kwa wengine. Waamini wawe pia na ujasiri wa kuomba neema ya kusamehe na kusahau katika maisha yao! Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni Sala inayopyaisha na kutenda muujiza kama ilivyotokea kwa Mitume Petro na Paulo, wakazaliwa kutoka juu na kuwa viumbe wapya kwa kusamehewa na Mwenyezi Mungu na kuwapenda ndugu zake. Kwa njia hii, msamaha unauwezo wa kubadili ubaya kuwa wema na hivyo kugundua ile furaha ya kusamehewa na kupewa Roho Mtakatifu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka waamini kuchukua hatua ya kwanza kutoa msamaha, kukutana na ndugu zao katika upendo mkamilifu. Kwa njia hii, wataweza kuwa wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu na hivyo kuwakirimia tena Roho wa umoja!

Na Padre Richard. A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.