2018-06-22 16:40:00

Papa Francisko: Miaka 50 ya ROACO chombo cha Injili ya upendo!


Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki kunako mwaka 2017 limeadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Tukio hili likapambwa kwa Jubilei ya Miaka 25 tangu kuchapishwa kwa Gombo la Sheria za Makanisa ya Mashariki. Kuanzia tarehe 19-22 Juni 2018 Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO limekuwa likiadhimisha mkutano wake wa 91 wa mwaka sanjari na Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake rasmi. ROACO ni chombo cha matumaini ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, eneo ambalo kwa sasa limegeuka kuwa uwanja wa vita. Jubilei hii ni kipindi cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu na wafadhili mbali mbali waliojisadaka kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye shida mbali mbali katika maisha!

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 22 Juni 2018 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa ROACO kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Huu ni mwaka wa Bwana uliokubalika, mwaka wa ukombozi wa watumwa, ni muda muafaka wa kusamehe madeni na kuanza kumiliki ardhi kwa kutambua zawadi ya Agano la Mungu, alama kwamba, wao ni watu wake. Ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu na kuwaombea wale wote waliotangulia mbele ya haki, ambao wamejisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa ajili ya Kanisa Katoliki huko Mashariki.

Kwa hakika, hawa wamekuwa ni mashuhuda wa Injili ndani na nje ya nchi zao. Ni ushuhuda ambao umetikiswa sana kutokana na mateso, vita, nyanyaso na kinzani; mashambulizi ya kigaidi na misimamo mikali ya kiimani pamoja na vita ya kidini huko Mashariki ya Kati, ambayo kwa sasa inaonekana kana kwamba, hakuna dalili za kusitishwa kwake! Ushuhuda wa Injili ya upendo, umekuwa ni faraja kwa waathirika wa vita; wakimbizi na wahamiaji, lakini zaidi kwa ajili ya maisha na utume wa Makanisa ya Mashariki kama sehemu muhimu sana ya utekelezaji wa shughuli za kichungaji na uinjilishaji sanjari na ustawi wa jamii.

Kwa njia hii, sura ya Kanisa linalotangaza na kuinjilisha inajionesha kwa njia ya matendo, kiasi hata cha kumwilisha upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu. Mwelekeo huu unatoa ukombozi unaompatia mwamini uhuru wa ndani kwa njia ya maondoleo ya dhambi, tayari kujikita katika ujenzi wa amani inayopaswa kutawala nyoyo za watu! Mtakatifu Petro katika hotuba yake kwenye Siku kuu ya Pentekoste anasema, itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono na wazee wenu wataota ndoto! (Mat. 2:17).

Makanisa Katoliki Mashariki yanatakiwa kuwa kweli ni mashuhuda wa kitume, kumbe, yanapaswa  kutunza na kuendeleza moto wa Pentekoste; kila siku yawe tayari kugundua uwepo wake wa kinabii, sehemu mbali mbali yanapofanya hija zake, kuanzia mjini Yerusalemu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni Mji Mtakatifu ambao una wito na utambulisho wake maalum, unaovuka malumbano ya kisiasa, kwani hata kama Wakristo ni kundi dogo, lakini linapata nguvu yake kutoka kwa Roho Mtakatifu, ili kutekeleza utume wake wa ushuhuda, leo hii kuliko hata wakati mwingine wowote. Hapa ni mahali palipofanyika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, changamoto na mwaliko kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati kutambua na kutekeleza wito wao maalum kwa kushuhudia imani na matumaini yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Watoto wa Makanisa Katoliki Mashariki wanapaswa kutunza ndani mwao unabii wa kutangaza na kushuhudia Injili, kati ya watu wanaoteseka na kudhalilishwa kama wakimbizi na wahamiaji. Watoto hawa waonje ukarimu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuendeleza amana, utajiri na Mapokeo yao. Kwa njia ya msaada wa hali na mali, wamekuwa na ujasiri wa kuishi na kuteseka kwa ajili ya Injili ambayo ni chemchemi ya furaha kwa watu wa nyakati zote. Baba Mtakatifu analipongeza ROACO kwa juhudi kubwa ya kulitegemeza Kanisa kwa njia ya matendo ya huruma; mashuhuda wanaothubutu kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, licha ya dhuluma na nyanyaso. ROACO iendelea kujibu kilio na matamanio ya umoja wa Wakristo; kwa kuonesha moyo wa nyenyekevu kwa watu wote, ushuhuda wa Kanisa la Kristo Mfufuka ambalo linapitia changamoto kubwa, mateso ya kiroho na kimwili, huko Mashariki ya Kati na Ulaya ya Mashariki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.