2018-06-22 14:18:00

Katibu Mkuu wa UN anasema ukristo ni sehemu kamili ya utamaduni wa Mashariki


Ukristo ni sehemu kamili ya utamaduni wa Mashariki, kwa maana hiyo hatuna budi kuhakikisha wakristo na wahusika wa dini ndogo ndogo wanarudi mara baada ya kwenda mbali na nchi yao asili kwasababu ya hali ya vurugu na mateso hasa hasa kuhakikisha kwa namna ya pekee uhakika wa hali halisi ya kisiasa nchini Iraq na Siria. Hayo yametamkwa na Bwana Antònio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati wa fursa ya mazungumzo aliyofanya Jumatano tarehe 20 Juni 2018, huko Moscow na Patriaki Cyril, Mkuu wa Kanisa la Kiorthodox  nchini Urusi.

Vyanzo vya habari nchini Urusi vinaeleza juu ya pongezi ya Katibu Mkuu kwa Patriaki wa Moscow wakati wa  mazungumzo lakini pia katibu kubainisha juu ya matatizo ya nchi za mashariki kama ile ya Siria na kwamba katika hali yao,ipo haja ya kulinda madhehebu madogo ya dini. Na wakati wa ziara yake mjini Moscow, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekutana hata na  Rais wa Urusi, Bwana Vladimir Putin na Waziri wa Mambo ya nchi za Nje wa Urusi Bwana Sergej Lavrov Alhamisi  tarehe 21 Juni 2018. 

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema, kuwa na taasisi imara duniani ni muhimu katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, ugaidi na changamoto nyinginezo. Na akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Bwana Lavrov, amewaambia waandishi habari mjini Moscow kuwa, “kutokana na changamoto zilizoko, tunahitaji nguvu za pamoja kuweza kuzikabili na hilo linadhihirisha umuhimu wa taasisi imara za pamoja na uwepo wa sheria zenye muundo wa ushirika wa kimataifa zikiambatana na mkataba wa Umoja wa Mataifa.”

Bwana Guterres, vilevile amesema kuwa, yeye na wenyeji wake wamejadili changamoto mbalimbali kuanzia Mashariki ya Kati, sehemu kadhaa za Afrika, Korea Kaskazini na Ukraine na pia kugusia migogoro mingine tofauti iliyoko ulimwenguni hivi sasa. Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa na Urusi zitashirikiana kuhusu mgogoro wa Siria  ambapo amesema, lengo ni kuwa na Siria  ambayo mipaka yake inaheshimiwa na kuweza kujiamulia mustakabali wake na makundi yote kujihisi yanahusishwa. Pamoja na hayo akiwa katika nchi hiyo, amepata kukutana pia na maafisa mbalimbali wa mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa nchini humo na pia mchezaji maarufu wa zamani wa mchezo wa Hockey Vyacheslav Fetisov ambae hivi majuzi aliteuliwa kuwa  mlezi wa ofisi ya mazingira ya Umoja wa Mataifa katika eneo la Polar.

Na Sr Angela Rwezaula 
Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.