Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Sumbawanga inasema, kumekucha!

Askofu mteule Beatus Christian Urassa, tarehe 24 Juni 2018 anawekwa wakfu kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Sumbawanga, Tanzania.

22/06/2018 17:25

Mhashamu Askofu mteule Beatus Christian Urassa wa Jimbo Katoliki Sumbawanga, Tanzania, katika maadhimisho ya Siku kuu ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji, anatarajiwa kusimikwa rasmi kuongoza Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Ibada ya Misa Takatifi unatarajiwa kuanza saa 3:00 za Asubuhi kwenye Viwanja vya Kanisa kuu la Jimbo Katoliki Sumbawanga. Ibada hii, itatatunguliwa makesha, Jumamosi, kwa Askofu mteule kukabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu; adhimisho la Masifu ya jioni, kiri ya imani pamoja na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.  

Askofu mteule Beatus Christian Urassa alizaliwa tarehe 2 Agosti 1965 huko Keni Mashati Rombo, Jimbo Katoliki la Moshi. Alipata majiundo na masomo yake ya kifalsafa kutoka Seminari kuu ya Shirika la Mitume wa Yesu, Lang’ata, Jijini Nairobi nchini Kenya. Baadaye akajiunga na Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu na kupelekwa kuendelea na masomo yake ya kitaalimungu kwenye Seminari kuu ya Mtakatifu Charles Lwanga, maarufu kama Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania.

Baadaye, alitumwa mjini Roma kuendelea na masomo ya taalimungu maisha ya kiroho kwenye Taasisi ya Kipapa ya Teresianum, iliyoko Roma na hapo akajipatia shahada ya uzamivu katika maisha ya kiroho! Tarehe 12 Julai 1997, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tangu wakati huo, kama Padre na Mtawa, amefanya kazi mbali mbali. Kati ya mwaka 1997-1998 alikuwa ni Katibu mkuu wa Halmashauri kuu ya Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu (ALCP / OSS) yenye Makao makuu yake Jimbo Katoliki la Moshi.

Kati ya mwaka 1998-1999, alikuwa ni Paroko usu, Parokia ya Mwananyamala, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kati ya mwaka 1999-2000 akateuliwa kuwa ni mlezi katika nyumba yao ya malezi, iliyoko Jimbo Katoliki la Morogoro. Kati ya mwaka 2000 hadi mwaka 2003 akatumwa Roma kuendelea na masomo ya juu na huko akajipatia Shahada ya uzamivu. Kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2015 amekuwa ni Padre mkuu wa Kanda Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu (ALCP / OSS).

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

22/06/2018 17:25