2018-06-21 17:38:00

Papa Francisko: Wakristo wanapaswa: Kutembea, Kusali na Kushirikiana


Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Kiekumene, Alhamisi, 21 Juni 2018, ametumia fursa hii kuwashukuru viongozi wakuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kumwalika ili kushiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, kielelezo cha utimilifu kadiri ya Maandiko Matakatifu! Ni mwaliko wa kusamehe bila kuchoka kwa kujikita katika msingi wa haki, upendo, umoja na mshikamano wa waamini waliojipatanisha na hivyo kumshukuru Mwenyezi Mungu!

Tukio hili ni ushuhuda wa waamini waliothubutu kujizatiti katika upatanisho, ili kutekeleza mapenzi ya Kristo Yesu, ili wote wawe wamoja; kwa kujiaminisha kuhusu umoja, ili kuondokana na hali ya kudhaniana vibaya pamoja na kutingwa na uwoga usikuwa na mashiko wala mvuto! Kwa njia ya upendo wakathubutu kuvunjilia mbali woga kama anavyokaza kusema Mtakatifu Gregory wa Nisa, Mwalimu wa Kanisa. Wakristo katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo wamefaidika kwa imani, matumaini na mapendo ya waamini waliojizatiti, wakaonesha ujasiri hata kubadili mwelekeo wa historia iliyowatumbukiza Wakristo kiasi hata cha kudhaniana vibaya na hatimaye, kusambaratika.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Roho Mtakatifu ni chanzo na mwongozo wa majadiliano ya kiekumene, anayewaelekeza waamini katika njia ya umoja uliopatanishwa, ili kuwa na mwelekeo wa udugu unaowaunganisha Wakristo wote. Miaka 70 ni kielelezo cha Mitume 70 waliotumwa na Kristo Yesu kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hii ina maana kwamba, Wakristo wote wanahimizwa kuwa mitume na wamisionari, ili kuinjilisha, lakini zaidi wakiwa wamoja! Utume wa kimisionari unafumbatwa katika kutangaza na kushuhudia, lakini zaidi kwa njia ya huduma makini ya maendeleo endelevu ya binadamu!

Licha ya mabadiliko ya mahali na nyakati, lakini Kanisa la Kristo linakua na kusambaa kwa njia ya mvuto na wala si kwa wongofu wa shuruti! Huu ni mwaliko wa kutambua nguvu ya ufufuko na umoja katika mateso yake; ili kutangaza na kushuhudia utukufu wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu. Hii ndiyo amana na utajiri ambao Kanisa limepewa na kuuhifadhi katika vyombo vya udongo, tayari kupambana na changamoto mamboleo kwa mwono wa tunu msingi za Kiinjili. Wakristo wanachangamotishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili; kwa kumshukuru Mungu na kuwahudumia jirani.

Ikiwa kama kutaongezeka ari ya kimisionari, kwa hakika, hata mchakato wa umoja wa Kanisa utaongezeka maradufu. Haya yatakuwa ni mapambazuko ya kiekumene kwa kushikamana na Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu mwenye maneno ya uzima! Baba Mtakatifu Francisko anasema, amependa kushiriki kikamilifu katika tukio hili, kuonesha na kushuhudia kwamba, Kanisa Katoliki linapenda kujikita katika majadiliano ya kiekumene kwa kushirikiana kikamilifu na Makanisa mengine, ndiyo maana hata hija yake ya kitume nchini Uswiss inaongozwa na kauli mbiu “Kutembea, kusali na kushirikiana”.

Huku ni kutembea kunakowawezesha Wakristo kutambua asili yao kuwa ni Kristo Yesu, anayewawezesha kuzaa matunda, ikiwa kama watakuwa wameungana na kushibana naye! Kutembea kunawawezesha Wakristo kutoka ili kuyaendea mambo msingi katika maisha, kuwapelekea watu neema ya Injili inayoponya watu wanaoteseka. Kuenenda huku kusiwe kwa maneno matupu, anaonya sana Baba Mtakatifu Francisko, bali kwa kuhakikisha kwamba, wanawapeleka watu wa Mungu kwa Kristo Yesu, bila kufungwa na makandokando yao! Kutembea kwao, kusiwe ni kurejea katika nyayo zao, bali kwenda ulimwenguni ili kumpeleka Kristo Yesu kwa watu!

Kusali kutapata mafanikio makubwa ikiwa kama Wakristo watapendana na kwamba, Sala ya Baba Yetu wa Mbinguni inaonesha kwamba, wao ni watoto wa Baba yao wa mbinguni, wanaopaswa kudumisha udugu. Sala ni oksijeni na kikolezo cha uekumene, kwani inatoa nafasi kwa Roho Mtakatifu kuwasaidia Wakristo kusonga mbele, ili waweze kuwa wamoja! Kanisa Katoliki linatambua na kuthamini mchango wa kufanya kazi kwa pamoja katika: Imani na Katiba na kwamba, linatamani kuona mchango huu unaendelezwa mbele kwa kuwashirikisha mabingwa katika taalimungu, ili kuweza kuwa na mwono wa pamoja kuhusu Kanisa. 

Kanuni maadili na utu wema, ni kati ya changamoto changamani zinazopaswa kuvaliwa njuga katika majadiliano ya kiekumene, kama ilivyo muhimu kujikita katika majiundo ya elimu na Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo. Baba Mtakatifu anaipongeza Taasisi ya Kiekumene ya Bossey inayojishughulisha na majiundo ya kiekumene kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na viongozi wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo, sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa Katoliki pia linashiriki katika utume huu na kwamba, kila mwaka, Baba Mtakatifu anapata nafasi ya kukutana na kusalimiana makundi ya wanafunzi wanaotembelea Roma. Ongezeko la ushiriki wa kiekumene katika maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote ni jambo la kutia moyo!

Huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni njia muafaka ya kumfuasa Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu aliyekuja ulimwenguni ili kuhudumia na wala si kuhudumiwa. Changamoto hii inamwilishwa kwa namna ya pekee katika kauli mbiu hija ya haki na amani, kama njia makini ya kusikiliza na kujibu kilio cha watu maskini kitokana na vita, njaa na umaskini. Leo hii, kuna pengo kubwa kati ya maskini na matajiri duniani. Maskini ni wale ambao wanaelemewa na baa la njaa, wanaokosa fursa za ajira; wanaoteseka na kusumbuka kwa magonjwa; wote hawa wanataka kuonja huruma na upendo wa Wakristo, unaouwezesha moyo kuona mahangaiko ya wengine. Wakristo waungane ili kusikiliza na kujibu kilio hili kwa vitendo!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, lakini zaidi huko Mashariki ya Kati wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mama Kanisa anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa Wakristo wote hawa wanaoteseka. Huu ndio uekumene wa damu, unaowahimiza kusonga mbele katika kukuza na kudumisha umoja. Ni wakati wa kujihusisha na mahangaiko ya watu ambayo kimsingi hayapati nafasi katika vyombo vya mawasiliano ya jamii. Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza, kushuhudia na kuwahudumia watu sanjari na kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wakristo wajitahidi kumfuasa Kristo Yesu, kielelezo cha Msamaria mwema katika kuwahudumia watu wa Mungu. Kwa njia hii, kuna uwezekano mkubwa wa kupanga na kutekeleza mbinu mkakati wa huduma kwa maskini kwa pamoja kama kielelezo cha Injili ya upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.