2018-06-21 16:56:00

Papa Francisko asema, Wakristo wanahimizwa kuenenda katika Roho!


Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Geneva, nchini Uswiss, Alhamisi, tarehe 21, Juni 2018 amepokelewa na viongozi wa Serikali na Makanisa na baadaye kufanya mazungumzo ya faragha na Mama Alain Berset, Rais wa Shirikisho la Uswiss. Viongozi hawa wamepata nafasi ya kubadilishana zawadi mbali mbali kama sehemu ya ukumbusho wa tukio hili muhimu katika maisha na historia ya familia ya Mungu nchini Uswiss.

Baadaye, Baba Mtakatifu pamoja na ujumbe wake wameelekea kwenye Kituo cha Kiekumene cha Baraza la Makanisa Ulimwenguni na huko amepokelewa na Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni aliyekuwa ameongozana na Dr. Agnes Abuom, Mratibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni pamoja na wajumbe wa Kamati kuu. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni yamefunguliwa kwa Ibada ya Kiekumene, ambamo waamini wamesali sala ya toba, upatanisho na umoja wa Makanisa.

Baba Mtakatifu Francisko amepata nafasi ya kutoa tafakari yake katika Ibada hii kwa kuwataka Wakristo “kuenenda katika  Roho” Mwanadamu hapa duniani ni hujaji, tangu pale anapotoka tumboni mwa mama yake, tayari kusonga mbele na changamoto za maisha. Kutembea ni kazi inayohitaji nidhamu, unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kukumbatia na kuambata furaha na amani ya ndani, kwa kumtegemea na kumtumainia Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Abrahamu, Musa, pamoja na akina Petro na Paulo, Mitume. Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho ni kielelezo makini cha mshikamano na binadamu, kiasi hata cha kuacha Umungu wake, Yeye ambaye ni Bwana na Mwalimu, ili kuja kuenenda na binadamu katika Roho!

Kuenenda katika Roho anakaza kusema Baba Mtakatifu ni kiini cha wito na maisha ya Kikristo, ili kujipatanisha pamoja na kutekeleza dhamana ya Ubatizo, kwani hawatazitimiza kamwe tamaa za mwili. Hii ni changamoto ya kuondokana na ubinafsi, ili kumwachia Mungu nafasi aweze kumwongoza na hatimaye, kuondokana na tabia ya kushindwa kuwaona wandani wa safari, kwa kugeuka kuwa walaji wa kupindukia; kwa kuzuia sauti ya Mungu isiweze kusikika hata kidogo na matokeo yake ni utamaduni wa kifo, dharau kwa utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, kuenenda katika Roho kuna maanisha kujikita katika huduma na msamaha; kwa kuondokana na yale ya kale, tayari kufumbata Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani. Tunda la Roho anasema Mtakatifu Paulo ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi! Hii ni safari inayojikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa kuondokana na malimwengu yanayovuruga hata maisha ya Kijumuiya na matokeo yake ni utengano wa Kanisa.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limechangia sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kielelezo cha neema ya Mungu, ili kutekeleza mapenzi ya Kristo, ili wote wawe wamoja, kwa kuenenda chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, kwa kutoa kipaumbele kwa mafao ya wengi. Hapa kuna haja ya kubomolea mbali makundi ya waamini ndani ya Kanisa, kwa baadhi ya watu kudhani kwamba, wao wameendelea zaidi na wengine wamepitwa na wakati kwa kujikita katika Mapokeo yao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu, Injili na Jirani, wapewe kipaumbele cha kwanza, kama utekelezaji wa mantiki ya Fumbo la Pasaka, ambalo kwalo, Kristo Yesu, anaendelea kujisadaka kila siku kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu!

Baba Mtakatifu anasema, umefika wakati wa kung’oa ndago za chuki, uadui na utengano kama ulivyojionesha kwenye Jumuiya ya Wagalatia na kuanza kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa umoja, ili kuenenda na kukaa na waamini wengine; kwa kuambatana na Kristo Yesu kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili. Waamini wanahamasishwa kuenenda katika Roho, kwa kujitakasa kutokana na dhambi na ubaya wa moyo; kwa kuchagua na kuambata kwa ushupavu njia ya Injili, ili kukwepa njia za mkato zinazoweza kuwatumbukiza katika malimwengu! Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo kumwomba Roho Mtakatifu aweze kuimarisha hatua zao, ili kuenenda katika Roho kwa: kusali, kuinjilisha na kuhudumia kwa pamoja, mambo yanayompendeza Mwenyezi Mungu. Kumbe, mkazo lazima uwekwe kwenye kutembea, kusali pamoja na kufanya kazi kwa pamoja, dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo kuelekea kwenye umoja.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kinyume cha hapo ni utengano unaowatumbukiza watu katika vita, majanga na maafa makubwa mambo ambayo yanapingana wazi na mapenzi ya Kristo na kikwazo kwa ulimwengu na hudhuru tendo takatifu la kuhubiri Injili kwa kila kiumbe! Yesu anawataka wafuasi wake kujikita katika umoja, ili kuwalinda maskini na wanyonge ndani ya jamii. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawashukuru wote waliomwezesha kufanya hija hii ya kiekumene na hapa Geneva amekutana na ndugu zake ambao wako katika hija, kielelezo cha utii kwa Kristo Yesu na upendo kwa walimwengu. Msalaba wa Kristo, uwe ni dira na mwongozo wa kuenenda kwao, kwani Msalaba umevunjilia mbali ukuta wa utengano na uadui kati ya watu. Licha ya udhaifu wao wa kibinadamu, lakini bado upendo wa Mungu utaendelea kuwafunika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.