2018-06-20 15:14:00

Siku ya Kimataifa ya Mfumo wa Ugonjwa wa Neva mwaka 2018


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza katekesi yake Jumatano tarehe 20 Juni 2018 amekutana na kuzungumza na wagonjwa wa “SLA” yaani “La Sclerosi Laterale Amiotrofica” moja ya magonjwa hadimu yanayoendelea kuwasumbua watu zaidi ya milioni 450 sehemu mbali mbali za dunia. Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Ugonjwa Mfumo wa Neva, Alhamisi, tarehe 21 Juni 2018. Baba Mtakatifu amewahakikishi uwepo wake wa kiroho kwa njia ya sala na kuwaomba hata wao, kusali na kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka katika shida na mahangaiko yao.

Ugonjwa wa Mfumo wa Neva: Ugonjwa huo hatari husababisha mwasho kwenye mfumo wa neva, yaani ubongo na uti wa mgongo. Madaktari wengi wanaamini kwamba ugonjwa huo hutokea wakati kinga za mwili zinaposhambulia chembe fulani za mwili. Kisababishi cha ugonjwa huo hakijulikani lakini inadhaniwa kwamba huenda unasababishwa na virusi. Kisha sehemu fulani za mfumo wa kinga huvamia utando muhimu wenye mafuta unaofunika nyuzi za mfumo wa neva, na hivyo kuacha makovu kwenye utando huo.

Utando huo hukinga nyuzi fulani za neva. Kwa hiyo unapoharibiwa, mawimbi ya umeme yanaweza kuzuiwa kabisa au yanaweza kupenya kwenye neva zilizo karibu na kutoa ujumbe usiofaa. Kwa kuwa utando wa mfumo wa neva unaweza kuharibika mahali popote, wagonjwa huwa na dalili tofauti. Hata mgonjwa anaweza kuwa na dalili tofauti kila mara anapougua ugonjwa huo, ikitegemea sehemu ya mfumo wa neva iliyoathiriwa. Hata hivyo, kwa kawaida dalili huwa uchovu, unyonge, kufa ganzi kwa mikono na miguu, kushindwa kutembea, kuona kiwi, uchungu, mwasho, matatizo ya kibofu na tumbo, na vilevile kushindwa kukaza fikira na kutofanya maamuzi ifaavyo.

Mama Kanisa anakazia mchakato wa maendeleo ya sayansi na teknolojia inayopania kuboresha afya ya binadamu; kuzuia na kuponya magonjwa; kulinda na kudumisha mazingira bora kwa kuzingatia tamaduni, tunu msingi za maisha ya kiroho na athari zake katika jamii husika! Lengo kuu la maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba iwe ni kwa ajili ya kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Katika shida, mahangaiko na magonjwa ya mwanadamu ni vyema kujenga muafaka kati ya watu na taasisi, hata ikiwezekana kuvuka vikwazo vya maamuzi mbele ili hatimaye, kuweza kuunganisha nguvu kwa ajili ya kumsaidia mgonjwa.

Kuhusu setra na mikakati ya afya ya binadamu Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia mambo makuu matatu: Kukinga, Kurekebisha, Kutibu na Kujiandaa kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu anakaza kusema, magonja na shida nyingi zinazomwandama mwanadamu zingeweza kuepukika, ikiwa kama watu wangekuwa na mfumo na utaratibu mzuri wa maisha na tamaduni wanamoishi. Kumbe, kinga ingelenga zaidi kukuza na kudumisha utu wa binadamu pamoja na mazingira anamoishi kwa kuweka uwiano mzuri wa elimu, mazoezi ya viungo, lishe pamoja na utunzaji bora wa mazingira, bila kusahau kutekeleza kwa dhati “sheria kanuni za afya bora” ambazo zinapata chimbuko lake katika maisha ya kiroho, tafiti na chunguzi za magonjwa. Mambo yote haya yangeweza kumsaidia mwanadamu kuishi vizuri zaidi.

Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna magonjwa ambayo yanasababishwa na mazingira pamoja na tamaduni mamboleo; baadhi yao ni ulevi, uvutaji wa sigara, uchafuzi wa hewa, maji na ardhi. Magonjwa mengi ya Saratani yangeweza kuepukika ukubwani, ikiwa kama kungekuwepo na sera na mikakati ya kukinga, dhamana na wajibu unaopaswa kutekelezwa na wote! Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kinga kama hatua ya kwanza ya kudumisha afya bora! Baba Mtakatifu anapongeza juhudi na jitihada ambazo hadi sasa zimefikiwa katika maendeleo ya sayansi ya tiba ya mwanadamu, hasa kwa kuzingatia magonjwa hadimu, chanjo pamoja na magonjwa yanayoshambulia seli za binadamu. Sayansi imeweza kukinga na kurekebisha seli zinazoshambulia magonjwa haya. Ili kupata ufanisi mkubwa zaidi kuna haja ya kuendelea kuwekeza katika tafiti, jambo muhimu sana katika maendeleo ya sayansi na utu wa binadamu.

Sayansi na mazingira yanategemeana na kukamilishana na kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia yanasaidia kwa kiasi kikubwa maboresho ya afya kiasi hata cha kubadili vinasaba vya watu. Pamoja na maendeleo yote haya ya sayansi na teknolojia, Mama Kanisa anapenda kukazia utu, sheria na kanuni maadili; kwa kutambua uwezo na mapungufu ya sayansi na kwamba, kipimo cha maendeleo ni ustawi, mafao ya wengi na kwa ajili ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.