2018-06-20 15:30:00

Mshikamano wa upendo na udugu kwa wakimbizi na wahamiaji!


Kuna haja ya kuwa na mtazamo uliopyaishwa kuhusu mahusiano na mafungamano na wahamiaji pamoja na wakimbizi, kwa kujenga na kudumisha umoja na udugu. Hiki ni kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliowaandikia wale wote walioshiriki chakula cha mchana, Jumanne, 19 Juni 2018, kilichoandaliwa kwa ajili ya kuenzi kampeni ya “Shiriki safari na wakimbizi”. Wadau wakuu wa tukio hili wamekuwa ni Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis pamoja na Shirika la Misaada ya Kanisa Catoliki nchini Italia, Caritas Italiana.

Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime, katika ushirikiano na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Anawashukuru kwa kugaribisha kampeni hii katika ngazi ya kimataifa, tukio ambalo, tarehe 27 Septemba 2017, alilizindua rasmi. Leo hii kwa namna ya pekee, anapenda kuwaalika wadau mbali mbali kupokea ndani mwao matukuo muhimu yaliyowagusa kwa namna ya pekee, wakati wote wa  safari na kwa sasa wana matumaini kiasi gani? Baba Mtakatifu anawaalika wakimbizi na wahamiaji kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yao, ili kusherehekea yale mambo msingi yanayowaunganisha.Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa ujumbe wake, anapenda kuwahimiza Caritas, Jumuiya za waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujitahidi kujenga na kudumisha mchakato wa watu kukutana, ili kupyaisha udugu na wakimbizi pamoja na wahamiaji.

Itakumbukwa kwamba, kuanzia tarehe 17- 24 Juni 2018 ni juma la utekelezaji wa sera na mikakati ya Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji kwa vitendo. Mwezi Septemba 2018, Caritas Internationalis itahamishia mchakato wa uragibishaji wa kampeni hii kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, ili kuweza kupitisha miswada miwili ya kimataifa kwa ajili ya ulinzi, usalama na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji duniani. Mwishoni mwa mwaka 2019, Caritas Internationalis itakuwa inahitimisha kampeni hii ya Shiriki safari na wakimbizi pamoja na wahamiaji: “Share the journey”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.