2018-06-20 15:46:00

Hija ya Kiekumene ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Uswiss, 2018


Hija ya Kiekumene ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Geneva, huko nchini Uswiss Alhamisi, tarehe 21 Juni 2018, inaongozwa na kauli mbiu “Kutembea, Kusali na Kushirikiana” muhtasari wa dhamana na malengo makuu ya majadiliano ya kiekumene kwa wakati huu Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapoadhimisha Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. Akiwa mjini Geneva, Baba Mtakatifu atakutana, atasali na kutafakari pamoja na wajumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ambalo kwa sasa lina zaidi ya waamini milioni 500. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kanisa linapomkumbuka Mtakatifu Aloyce Gonzaga. Ibada hii inatarajiwa kuhudhuriwa na waamini kutoka ndani na nje ya Uswiss.

Hii itakuwa ni nafasi pia kwa Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na wajumbe wa Makanisa kutoka Korea ambao wamekuwa mstari wa mbele kusali kwa ajili ya kuombea: haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa baina ya Korea ya Kusini na Korea ya Kasikazini. Hafla ya chakula cha mchana kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko anasema Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican imeandaliwa na Taasisi ya Kiekumene ya Bossey.

Baba Mtakatifu, atatembelea Kikanisa cha Bossey, mahali ambapo wanafunzi hupata nafasi ya kusali na kutafakari matendo makuu ya Mungu katika maisha yao pamoja na kukutana na Padre Lawrence Iwuamadi, Dekano wa kwanza kabisa kutoka Kanisa Katoliki. Vatican News kama kawa itakuwa nawe bega kwa bega kukujuza kile kinachojiri wakati wa hija ya kiekumene ya Baba Mtakatifu Francisko huko Geneva, Uswiss! Ukiwa na haraka zako, tembelea tovuti ya Vatican News kwa habari za uhakika zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.