Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Wekezeni matumaini yenu kwa Mungu! Inalipa!

Kristo Yesu ni nahodha shupavu wa Kanisa lake, hata pale linapokumbana na dhoruba kali, bado liko mikononi mwa kiongozi makini. - REUTERS

19/06/2018 15:52

Jumuiya ya Mwinjili Marko ilikuwa jumuiya iliyokuwa kwenye shida kubwa ya madhulumu dhidi ya waliomwamini Kristo. Kanisa la wakati huo lilikuwa kama mashua katika mawimbi makali. Marko pamoja na watu waliona kama vile Yesu hawasikii na kuwasidia katika shida zao.  Namna ya kwanza ya kupambana na shida hiyo ilikuwa ni kubaki imara katika sala. Mwinjili Marko na wenzake wanamwita Yesu na jibu la Yesu ni dalili tosha kwamba yuko pamoja nao katika mahangaiko yao anayaona na kuwaokoa.

Alipotuliza dhoruba wanashangaa. Huyu ni nani? Hivyo katika injili  yote ya Marko swali hili linabaki – mwinjili Marko anasisitiza juu ya fumbo la Kristo na ufunuo wake. Marko anajua wazi kuwa Kristo ni nani: mwanzoni wa Injili yake aonesha wazi – Kristo ni mwana wa Mungu. Kwetu sisi anatualika nasi tulitambue Fumbo hilo na ufunuo huo, kama walivyofanya wafuasi wake huko Galilaya na Yudea. Tendo la imani kwa Yesu ni zaidi ya tangazo kwamba Kristo ni Bwana. Tunatamka mara nyingi  katika kanuni ya imani.  Zaidi ni wito wa kukutana naye na polepole ...... kutamka wazi toka moyoni – huyu ndiye Kristo mwana wa Mungu.

Injili ya Marko – inatupatia funuo mbili; na zote ni ungamo la imani; Ungamo la Mtakatifu Petro – Kristo ni Mwana wa Mungu, mpakwa mafuta wa Bwana na aliyepelekwa kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu – Mk. 8:9. Ungamo la pili ni la askari chini ya Msalaba kwamba, hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu – Mk. 15:39. Ungamo hizi zimekuja baada ya matendo makuu yaliyoliyofunika hilo fumbo, lakini polepole yakilifunua. Tukiangalia tena injili: ukuu wa habari hiyo tunaona; Yesu anaamua kuvuka bahari, wafuasi tayari wako naye, zipo mashua nyingine, baadaye hatusikii tena habari juu ya mashua hizi halafu; dhoruba, Yesu amelala. Baadaye Yesu anatuliza dhoruba, anawakemea kwa imani haba, hawakumjua vizuri, wana wasiwasi – hutokea mara nyingi kwetu lakini baada ya kujifunua wanamwamini

Hakika maisha yetu yamejaa matukio kama haya katika injili. Mara nyingi tunajiamini wenyewe na kudhani kuujua ukweli wote na kuaamini kuwa mambo yanaenda kwa utulivu. Baadaye, tunapata dhoruba – na tunadhani kuwa Yesu hajali wala haguswi na shida pamoja na mahangaiko yetu! Tukumbuke kuwa adhimisho la liturujia – ni ukumbusho wa uwepo endelevu wa Kristo Yesu na muda muafaka wa kuhuisha imani yetu.

Imani yetu ni lazima iwe kama ile ya wale vijana watatu; Shedraka, Meshaki na Abednego katika Dan. 3: 17-18 – kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto, naye atatuokoa na  mkono wako, ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako,  wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. Wakati  mwingine maisha yetu ni kama kuvuka bahari. Bahari yaweza kuwa wewe mwenyewe, familia yako, jumuiya yako, moyo wako n.k. Katika haya yote mawimbi hayakosekani. Ni nani asiyekumbana na mawimbi katika maisha yake? Hata Yesu hakusema kwamba mawimbi hayatakuwepo ila aliahidi uwepo wake. Mtume Paulo katika 2 kor. 12: 7-10 anasema wazi jinsi anavyokumbwa na mawimbi – lakini pia anasema wazi anapokuwa dhaifu ndipo ninapata nguvu.

Matumaini ndiyo yaliyowaokoa wale wafuasi na hii itukumbushe haja ya kusafiri pamoja na Yesu wakati wote katika maisha yetu. Haja ya kumchukua Yesu daima katika maisha yetu, katika mashua ya maisha yetu, katika bahari za maisha ya kila siku – tutupilie kwake mahangaiko yote ya maisha – 1 Pt. 5:7. Yesu anawakemea kwa sababu wao walidhani kwamba hajali mahangaiko yao. Kwa uhakika Mungu ndiye wa kwanza aliyejali hali zetu na akaja kutukomboa. Hivyo hawezi kutuacha sisi tuangamie.

Upo mfano wa mmoja wa mtu anayetembea jangwani na pembeni mwake kuna unyayo mwingine. Baada ya muda anagundua kuwa ni unyayo wa Yesu. Akiendelea na safari ule unyayo ukapotea na akajua kuwa amebaki peke yake na hasa wakati wa mahangaiko. Akamlalamikia Yesu kwa kumwacha peke yake wakati wa shida. Lakini Yesu akamwambia, sikukuacha peke yako kwani ule unyayo mmoja uliokuwa ukiuona haukuwa wa kwako bali wangu kwani nilikubeba mabegani.

Naye Mtakatifu Francis wa Sales anasema; iweni kama watoto wadogo – ambao kwa mkono mmoja hukamata kwa nguvu mkono wa baba/mama na kwa mkono mwingine huokoteza matunda au maua mazuri. hivyo hata sisi jinsi tunavyookoteza mazuri ya ulimwengu, tusiuache kamwe mkono wa mungu ili tusije anguka na kupotea baharini. Tulipoanza karne ya 21 – na katika barua yake kwa waamini = "Novo Millenio Inuente" yaani "Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo" Mtakatifu Yohane Paulo II – alialika taifa la Mungu kujenga ufalme wake Mungu, kuwa na dhamana ya kuujenga ule ufalme – Lk. 5:4 – tupeni jarife. Anatualika tuwekeze kwake Mungu.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa kitume “Dhamana ya Afrika”, Africae munus” anasema Afrika iko mikononi mwa wa Waafrika wenyewe. Mwito unatolewa ukizingatia wajibu wa kwanza kabisa wa mbatizwa – kuutangaza ufalme wa Mungu kwa maneno na matendo.  Maisha ya imani yaonekane katika maisha yetu ya kila siku – kuwa tayari kujifunua kwa Kristo na kuwa pamoja naye. Katika injili ya Yoh. 6:68 – tunasoma kuwa Yesu peke yake ndiye mwenye uzima. Wakifuata mfano wa Kristo – wakristo wote wanaalikwa kutafakari  huruma ya Mungu na mwanga wa Roho Mtakatifu. Uinjilishaji unatakiwa ulete msamaha/upatanisho, haki na amani. Yesu ndiye aliyeleta haya. Ufalme hauji kwa mabavu ila katika unyenyekevu wa huduma, siyo kudhulumu wanyonge bali katika kuwalinda na kuwapatia uzima – Yoh. 10:10. Tunaalikwa kuweka matumaini yetu kwa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

19/06/2018 15:52