Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Siku ya Wahamiaji Duniani 2018: Wanawake waibuka na waraka mzito!

Shirikisho la Wanawake Waprotestanti nchini Uswiss, linawataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kutoa ulinzi, usalama na hifadhi zaidi kwa wanawake wakimbizi na wahamiaji. - REUTERS

19/06/2018 11:00

Kanisa katika maisha na utume wake, daima limekuwa likitoa kipaumbele cha kwanza katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, kwani hii ni changamoto ambayo inafumbatwa pia hata katika Maandiko Matakatifu. Hawa ni watu wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Ni watu wanaokimbia: vita, nyanyaso, majanga asilia, umaskini na ukosefu wa fursa za ajira. Wakimbizi na wahamiaji ni hazina na amana kubwa kwa nchi zinazotoa hifadhi na hata kwa zile nchi zao za asili. Kanisa linakazia sana utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazofumbatwa hasa katika changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko yaani: hawa ni watu wanaopaswa: kupokelewa, kulindwa, kuendelezwa na kuhusishwa katika sera na mikakati ya jamii inayowahifadhi.

Katika maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani kwa mwaka 2018, Shirikisho la Wanawake Wakiprotestanti nchini Uswiss, lililoanzishwa kunako mwaka 1947, limechapisha Waraka unaoongozwa na kauli mbiu “Mimi ni mwanamke, niliyekimbia nchi yangu”. Shirikisho hili linawataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi katika ulinzi na usalama wa wanawake wakimbizi, pamoja na kuwapatia msaada wa hali na mali wanaouhitaji ili kuanza kuandika kurasa mpya za maisha yao.

Bi Dorothea Foster, Rais wa Shirikisho la Wanawake Wakiprotestanti nchini Uswiss anasema, wanasikitishwa sana na nyanyaso za kijinsia wanazotendewa wanawake na kwamba, wanapaswa kupewa huduma makini zaidi, ikilinganishwa na wanaume katika hali na mazingira kama yao. Kuna sababu mbali mbali zinazowafanya wanawake kuzikimbia nchi zao, ukatili wa majumbani, ndoa za shuruti na utumwa mamboleo; mambo yanayodhalilisha utu na heshima yao kama binadamu. Katika hali na mazingira kama haya, wanawake wanajikuta wakiwa wamechukua maamuzi magumu, ambayo wakati mwingine yanahatarisha hata maisha yao kwa siku za usoni.

Wanawake wanalazimika kukimbia na watoto wao, kumbe mambo kama haya yanahitaji kuangaliwa na vituo vinavyowahudumia wakimbizi na wale wanaoomba hifadhi ya kisiasa. Mfumo wa Sheria kuhusu wahamiaji nchini Uswiss bado una mapungufu makubwa na ambao umekuwa ukilalamikiwa na Baraza la Umoja wa Ulaya. Wanawake wanapaswa kupewa hifadhi zaidi, ili kuwasaidia kuvuka ombwe la aibu na majonzi katika maisha! Haya ni mambo ambayo wakati mwingine si rahisi sana kufutika. Shirikisho hili limekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya huduma kwa wanawake wanaojikuta katika mazingira magumu na hatarishi; limeendelea kuwa mstari wa mbele kupigania haki, usawa na wajibu wa wanawake katika ustawi na maendeleo ya jamii zao. Shirikisho hili limeendelea kuwa ni Jukwaa la  mawazo na maoni ya wanawake wa kiprotestanti nchini Uswiss.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican Ndews!

19/06/2018 11:00