2018-06-19 14:17:00

Papa Francisko asema: Msamaha, Sala na Upendo ni silaha dhidi ya adui


Mageuzi makubwa yaliyoletwa na Yesu katika Amri kuu ya upendo ni kuwapenda jirani kama nafsi zao; lakini pia kuwapenda adui zao na kuwaombea wale wanaowaudhi; ili wapate kuwa wana wa Baba yao aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Mkiyatenda haya, anasema Kristo Yesu, basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 19 Juni 2018 amesema, hii ndiyo changamoto kubwa inayofumbatwa katika Fumbo la Amri kuu ya Upendo, ili waweze kuwa wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamlifu! Msamaha, sala na upendo ni nyenzo madhubuti katika mapambano na adui na watu wanaosababisha karaha katika maisha ya watu wengine.

Mwinjili Mathayo anaonesha ugumu uliopo kwa binadamu kuweza kumwilisha Amri mpya ya upendo kwa adui, changamoto inayohitaji neema ya kuweza kuwabariki na kuanza kujibidisha kuwapenda adui. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, agizo hili ni sehemu pia ya Sala ya Baba Yetu wa Mbinguni “Utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe wale waliotukosea”. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kusali na kuomba neema ya kuwapenda watu wote bila ubaguzi, ingawa si rahisi. Kuna watu wameteseka na hatimaye, kuonja mkono wa chuma, kwa vile tu walikuwa ni Wakristo! Nchini Urusi, Wakristo walihukumiwa na kupelekwa uhamishoni kwenye Visiwa vya Siberia, ili kufa huko kwa baridi na utupu! Lakini, Wakristo hawa wakageuka kuwa ni chemchemi ya sala kwa watesi wao, kama hata inavyojionesha kwenye kambi za mateso za Auschwitz na mahali pale ambapo kumekuwepo na mauaji ya kimbari. Wakristo waliwaombea watesi wao ili Mwenyezi Mungu aweze kuwabariki, ili watubu na hatimaye kumwongokea!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujifunza mantiki ya Kristo Yesu, wafiadini na waungama imani! Yesu mwenyewe alipokuwa anayamimina maisha yake pale Msalabani, bado alithubutu kuwaombea msamaha watesi wake, kwani walikuwa wanatenda lile wasilolifahamu. Sala hii ikarudiwa tena na Mtakatifu Stefano shahidi wakati alipokuwa “anatwangwa kwa mawe” hadi kifo. Mifano yote hii inafumbatwa katika kanuni ya kusamehe na kupenda!

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, mambo si rahisi sana katika familia, hasa baada ya “kutemeana cheche” na “kupandishiana mashetani”! Kama jambo kama hili ni vigumu kiasi hiki, sembuse adui anayetaka kukufutilia mbali kutoka katika uso wa dunia! Mkazo ni kusamehe na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, zaidi ya hapa anashindwa kuendelea, lakini Neno la Yesu linajitosheleza zaidi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu awakirimie neema, ari na ujasiri wa kuwapenda jirani zao, maadui pamoja na kuwaombea, ili waweze kuwa wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Siku ya leo, iwe ni fursa ya kusali na kuwaombea adui katika safari ya maisha na wala si kuweka kinyongo, ili kulipiza kisasi baadaye. Adui anapaswa kupendwa na kuombewa neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.