2018-06-19 15:13:00

Miaka 50 ya ROACO: Ushuhuda wa huduma kwa Makanisa ya Mashariki


Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki kunako mwaka 2017 limeadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Tukio hili likapambwa kwa Jubilei ya Miaka 25 tangu kuchapishwa kwa Gombo la Sheria za Makanisa ya Mashariki. Kuanzia tarehe 19-22 Juni 2018 Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO linaadhimisha mkutano wake wa 91 sanjari na Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake rasmi! Hiki ni kipindi cha sala, tafakari pamoja na kushirikisha mang’amuzi kuhusu: matatizo, changamoto na fursa zilizopo kwenye Makanisa ya Mashariki kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina.

Taarifa inaonesha kwamba, kati ya wawezeshaji wakuu kwenye mkutano huu ni pamoja na Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria, Askofu mkuu Paul Russel, Balozi wa Vatican nchini Uturuki pamoja na Askofu mkuu Alberto Ortega, Balozi wa Vatican nchini Iraq na Yordan. Wengine ni Monsinyo Segundo Tejado Munoz, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher atapata nafasi ya kuzungumzia hali halisi ilivyo katika Nchi Takatifu kwa wakati huu.

Wajumbe watahakiki Mchango wa Ijumaa kuu uliotolewa na waamini kutoka Makanisa mbali mbali kama kielelezo cha umoja na mshikamano na familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati! Wakristo wa Mashariki ya Kati na changamoto ya diaspora; changamoto za mikakati na shughuli za kichungaji kwa wahamiani na wakimbizi kutoka Mashariki ya Kati ni kati ya mada ambazo zinafanyiwa kazi. Wajumbe wa Mkutano huu, Ijumaa, tarehe 22 Juni 2018, wanatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.